NDANI YA BOKSI; Ulikuwa mwaka wa matukio zaidi ya sanaa

Muktasari:

  • Basata ndiye mzazi na mlezi wa sanaa zote nchini. Ni jukumu lake kulea, kuen-deleza, kukuza, kulinda na kuokoa sanaa inapobidi ili kufanya ien-delee kuwepo, lakini wale wazee pale Ilala wame-amua kujikita kwenye eneo moja tu la kufungia nyimbo au wanamuziki.

Sikuwa na furaha. Lakini nikalazimisha niwe na furaha kinguvu. Nikaagiza kinywaji kinachohifadhiwa ndani ya chupa yenye ustaarabu wa kipimbi sana. Eti haiwezi kukaa kitako mezani mpaka ilazwe. Mwisho wa siku ni wewe mnywaji unaishia kulala ukizidisha.

Katika baa moja maarufu mitaa ya Kurasini. Pembeni yangu kuna mrembo. Ninaposema mrembo nielewe, sijawahi kusifia kiumbe wa kike kindezindezi tu. Wema Sepetu? Labda lugha yake ya Kiingereza ndiyo inaweza kupata heshima ya kukaa kwenye mwili wa kiumbe huyu.

Ni wale warembo ambao unatumia pesa bila kikomo. Ikiisha hujutii kabisa. Na zaidi kesho yake unakopa tena sehemu pesa nyingi ili tu ukatumie naye tena. Shetani hakuwa bwege kumuita Eva kisirisiri na kumrubuni ili aje kumrubuni Adam. Mungu alijua kuumba hawa kina Hawa.

Huyu Eva niliyekuwa naye. Angetumiwa na shetani kunirubuni siyo tu ningekula lile tunda la mti wa katikati. Bali ningekula na mti mpaka mizizi yake ili afurahi. Mimi ‘siwezagi’ kabisa kujivunga mbele ya viumbe uzao wa Eva. Nikipenda nachukia mpaka pesa. Sitaki zikae kwenye akaunti yangu nazitoa zote ili zikakae kwake milele amina.

Watu walikuwa wakicheza na kufurahi utadhani wote matajiri. Watu toka mataifa ya Magharibi wangefika pale usiku ule wangeshangaa kusikia taifa letu ni masikini. Kumbe kando yake pale kuna uwanja wa mpira ambao kuna timu zinautumia bila kulipa wachezaji mishahara miezi na miezi. Maisha yetu tunayajua wenyewe.

Ghafla nikasikia shangwe kubwa la wazee kwa vijana. Wahudumu nao wakihudumia huku wakitikisha viungo vinavyotikisika kwenye miili yao. Kisa ‘Dijei’ kapiga ule wimbo uliofungiwa. Mpaka nikajiuliza kama ndio hivi ni nani sasa ambaye Basata wanadai anaharibika kimaadili kwa huu wimbo?

Maana wale waliofurahia ule wimbo ukiwatazama wengi wao wameharibika kimaadili kuliko maneno ya wimbo wenyewe. Sikujali nikaendelea na kinywaji changu huku macho yangu yakiendelea na utalii wa ndani kwenye mwili wa kiumbe pendwa kando yangu. Naye mwili aliutikisa kufuatisha mapigo ya wimbo ule.

Sikuwahi kuusikiliza wimbo ule kwa umakini. Siku hiyo niliusikiliza vyema maana ulirudiwa zaidi ya mara tatu. Nikagundua kuwa kosa la Diamond na Rayvanny ni kiitikio cha wimbo tu. Bila kiburi chao na sifa za kijinga wasingetumia maneno yale. Bado wimbo ungekuwa bora zaidi. Bonge la ngoma.

Tuachane nao maana mwaka huu wameutumia kwa matukio zaidi ya vipaji vyao. Wasafi Festival ilibamba mitaani kwa malumbano na Clouds zaidi ya ubora wa kazi jukwaani. Hakuna kumbukumbu nzuri ya Wasafi Festival zaidi ya mipasho yao kwa Clouds na Fiesta yao.

Matukio ambayo yaliibua tukio la Fid Q kuwatupia dongo Wasafi. Na kumfanya naye ‘atrend’ mitaani na mitandaoni kwa hilo tu kuliko kazi yake. Watu wa muziki hawana la kukumbuka kwa Fid mwaka unaoisha kupitia kipaji chake zaidi ya malumbano yake na Wasafi. Walioongozwa na Babu Tale kumnanga msela wa Rocky City.

Alikiba katoa nyimbo mbili mwaka huu. Na zaidi katambulisha familia yake ya muziki. Lakini ukweli ni kwamba nyimbo zake zote mbili zimeshindwa kufunika tukio la ndoa yake na kusajiliwa kwake na timu ya Coastal Union. Kipaji kimefunikwa na matukio yake.

Hata waandishi wakikutana na Alikiba wanavutiwa zaidi kumuhoji kuhusu soka. Wakienda mbali zaidi watataka kujua maendeleo ya ndoa yake kuliko kazi inayomlisha. Pengine hili limechangia zaidi nyimbo zake zifunikwe kwa uzito na matukio hayo.

Ommy Dimpoz haukuwa mwaka mzuri kwake baada ya kupata maradhi ya koo. Matibabu yake huko ‘Sauzi’ yaliteka masikio na macho ya mashabiki wa muziki na kusahau kabisa nyimbo zake. Mshikaji aliugua sana na anaendelea na matibabu. Tumuombee arudi katika afya imara zaidi

Mauasama kwa mara ya kwanza toka aanze muziki. Wimbo wake wa ‘iokote’ ulimpaisha matawi ya mbega. Bonge moja la ngoma ambalo ndani ya wiki tu likatuliza kitenesi cha ngoma ya ‘Jibebe’ toka kwa Wasafi. Lakini yeye mwenyewe akauzima moto wa ngoma yake kwa tukio la kusota rumande wiki moja.

Ajabu ni kwamba wakati wanamuziki wengi hubamba sana wakipatwa na tatizo kama hilo. Kwa Mauasama ilikuwa tofauti. Hakupaa sana jina lake ingawa wimbo unaendelea kukimbiza mitaani. Unaweza kupigwa sehemu ukauliza watu 10 wote wasijue mwenye wimbo. Tatizo.

Fiesta ya mwaka huu haikuwa na mvuto uliozoeleka. Achana na ujio wa Wasafi Festival. Na hili watu wengi wanatakiwa wajue, kwamba tatizo la Fiesta kutobamba si ujio wa Wasafi Festival. Kuugua kwa Ruge Mutahaba ndio tatizo zaidi. Huyo ndio kila kitu. Huyo ndo mwamba ambaye angetuliza mchezo wote.

Diamond, Said Fella, Babu Tale, Sallam na wote walio nyuma yao kama ni Kusaga au yeyote, hawawezi kuweka ‘bato’ na Ruge kwa kufanya tukio la burudani kwa wakati mmoja wakamfunika kiasi cha kunyoosha mikono. Ujio wa Wasafi Festival kama Ruge angekuwa kwenye afya yake wangesababisha alete kitu tofauti zaidi.

Tukio kubwa zaidi kwa mwaka unaoisha kwenye familia ya muziki ni ujio wa Wasafi Festival. Zaidi ya hilo hakuna tofauti. Wanamuziki wamekuwa wakifanya vitu vilevile kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo. Hata muziki umekuwa ukifanana. Hakuna jipya lililoleta tofauti.

Washikaji wa Bongo Movie ni tatizo zaidi. Wema ameishia kutamba kwa picha na video za kibwege. Ambazo zimeishia kumtembeza kwenye korido za mahakama badala ya kushinda ‘location’. Inasikitisha sana maana hakuna dalili ya kuipigania sanaa yao. Nao wamekuwa mashabiki wa Sultan.

Irene Uwoya haonyeshi kama staa wa filamu. Haeleweki anafanya biashara gani zaidi kutuua instagram kwa pamba flani amazing za kutugombanisha na kina Eva wetu majumbani. Na hawa ndo mastaa wa kike ambao wakitolea macho sanaa wanaweza kurudi kwenye ubora wao. Wana mashabiki wengi.

Basata kama kawaida wazee wamekula pozi pale Ilala wanasikilizia tu. Bwege gani atoe wimbo wa kibwege wamfungie kibwege. Yaani hawana mchongo mwingine zaidi ya kusikilizia wanamuziki wapotee maboya. Hawana mipango, mikakati wala mizuka ya kuendeleza sanaa.

Wamekuwa kama mgambo wa ‘site’ ambao wanavizia watu wafanye kosa wakamate. Mbali ya kufungia nyimbo na wanamuziki, Basata wamekuwa watu wa kutoa au kufuta vibali vya maonyesho au shughuli za sanaa. Zaidi ya hapo hakuna jipya, sanaa wameiacha ijiendeshe kichokoraa.

Achana na Sinema Zetu International Film Festival ambayo imeanza rasmi mwaka huu. Na mapambano ya Basila Mwanukuzi kurejesha shindano la Miss Tanzania. Ambalo lilipatwa na kifaduro chini ya Ludenga. Bongo Star Search nayo imefanyika kimiujiza tu. Hakuna la zaidi.

Tuzo za Kill zimeuawa, Basata kimya. Bendi za dansi ziko ICU, kama vile Basata hawapo. Hatumaanishi wao ndo watoe tuzo au wakashike magitaa na kuwaandikia mashairi wanamuziki wa bendi. Hapana. Kuna kitu kama Basata wanaweza kusaidia sanaa isife. Wanaweza na lipo ndani ya mamlaka yao.

Basata ni mzazi na mlezi wa sanaa zote nchini. Ni jukumu lake kulea, kuendeleza, kukuza, kulinda na kuokoa sanaa inapobidi ili kufanya iendelee kuwepo. Lakini wale wazee pale Ilala wameamua kujikita kwenye eneo moja tu la kufungia nyimbo au wanamuziki. Hawataki kufanya kazi ya ulezi na wasanii kuishi kiyatima.

Mwaka unaokuja ni juu ya wasanii kupambana wenyewe. Kama Wasafi wameanzisha redio na runinga. Alikiba pita kushoto hata kwa kuanzisha tuzo. Mwaka huu sijaona jipya kwa Kiba zaidi ya kupita njia za Diamond kwa kuanzisha kitu kilekile kama Wasafi. Kumiliki kundi la wasanii. Kazi za sanaa bila tuzo ni bure.

Huu siyo wakati wa kujenga urafiki na matajiri na viongozi wa kisiasa bure tu. Watumieni kukuza sanaa. Kina JB na wenzao wanaona ufahari kualikana kwenye minuso na kina Makonda. Lakini sanaa yao inachechemea huku wakijisaidia mmoja mmoja. Hakuna umoja wala upendo.

Kichekesho ni kwamba wasanii wanawaza siasa muda mwingi. Siasa imekuwa sanaa na sanaa imekuwa siasa. Mwaka unaoanza huenda tukapoteza kila kitu kwenye sanaa kwa sababu sanaa inatelekezwa na wana sanaa wenyewe wakiishi kwa matukio zaidi ya vipaji. Sisi tupo.