Ulinzi hadi nyumba 10 bado muhimu

Wednesday October 31 2018

 

By Sada Amir

Ni wakati wa kujiuliza tumeteleza wapi katika masuala ya kuimarisha ulinzi katika mitaa na vijiji vyetu kwa kutumia mfumo uliokuwapo wa kutumia viongozi kila baada ya nyumba 10.

Enzi za awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere kulikuwa na utaratibu wa kujumuisha na kuwashirikisha wananchi katika ngazi zote, kuanzia juu mpaka chini katika masuala ya ulinzi na usalama.

Utaratibu huo ulijumuisha wajumbe kila mmoja akiwa na nyumba zake kumi katika mtaa na aliwafahamu watu wote hata wageni waliohamia taarifa zilitolewa kwa mjumbe na ilikuwa lazima ajue mgeni huyo ametoka wapi na atakaa kwa muda gani.

Mfumo wa nyumba kumi ulisaidia kulinda usalama wa raia ambapo hata ulinzi wa sungusungu ulikuwa unafanyika katika misingi ya nyumba kumi.

Hata mtoto aliyezaliwa ilibidi aandikishwe kwa mjumbe na hata kwenye cheti cha kuzaliwa kulikuwa kuna sehemu ya jina la mjumbe.

Faida ya kuwa na wajumbe wa nyumba kumi ni nyingi ikiwemo ukusanyaji wa taarifa na data ulikuwa rahisi, usalama wa raia na mali zake ulikuwa wa kuaminika, jamii pia ilikuwa imeshikamana na kuaminiana.

Suala la ulinzi na usalama lilianzia nyumba kumi kwa vile lilikuwa ni rahisi na salama kwa wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama kubaini matendo yote ya kihalifu na lilikuwa jukumu la kila raia kumlinda mwenzake na kutoa taarifa kwa mjumbe kama kulikuwa na tatizo.

Bahati mbaya, ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi wajumbe hao waliokuwa wanafanya kazi za serikali na chama kwa wakati mmoja, wakabaki upande wa chama kwa ajili ya manufaa ya kisiasa.

Kutokana na hali hiyo, kumekuwa na matukio ya ajabu na ya kuogopesha ya kihalifu yanayotia hofu taifa letu.

Matukio hayo ni ya watoto kupotea katika mazingira tatanishi, watu kutekwa, ubakaji, udhalilishaji watoto yanazidi kutia wasiwasi.

Kwa mwelekeo wa matukio haya hata baba wa Taifa aliyeanzisha mfumo wa ulinzi hadi ngazi za chini kabisa angekuwepo sijui angechukuliaje?

Kinachoogopesha zaidi hata watu maarufu wameanza kutekwa kama ilivyotokewa kwa Mohamed Dewji ambaye alitekwa na kupatikana baada ya siku tisa jijini Dar es Salaam.

Unaweza kujiuliza, kama hali ipo hivyo kwa watu maarufu ambao wanapotea au kutekwa, vipi hali ya wananchi huku chini ambao ni wa kawaida?

Wananchi wanajiuliza haya mambo yanatokea wapi? Mbona hawali hayakuwepo na hata kama yalikuwepo mbona hayakushika kasi namna hii? Ina maana watekaji kwa sasa wana uwezo kuliko vyombo ulinzi na usalama?

Licha ya jitihada mbalimbali zinazooneshwa na jeshi letu la polisi kuhakikisha wanatokomeza masuala ya utekaji na kupotea kwa watu kusikojulikana, ni wakati sasa Serikali kuwashirikisha wananchi kwa kufufua mifumo iliyokuwepo awali ukiwemo wa wajumbe wa nyumba kumi.

Japo mifumo hiyo bado hipo kwenye baadhi ya maeneo kwa jina tu, ni vizuri wajumbe wa nyumba kumi wawepo nma watambuliwe kupitia serikali za mitaa badala ya kuwa chini ya chama cha siasa.

Turudi enzi hizo ambazo babu na wazazi wetu walilindana na matukio ya kihalifu kuyasikia ilikuwa kazi. Enzi hizo mtoto wa mwenzio alikuwa wa kwako, si kizazi hiki ambacho kila mtu anakwenda kivyake.

0768920097

Advertisement