Unai Emery: Hao Liverpool! Waacheni tu

Monday December 31 2018

 

Kocha wa Arsenal, Unai Emery hakutaka kupepesa wala kusema nini, alichosema ni kwamba hakukuwa na jinsi zaidi ya Liverpool kuwafunga katika mechi yao kwa kuwa walikuwa wazuri kila kona.

Arsenal ilitandikwa mabao 5-1 na Liverpool katika mechi kali iliyopigwa kwenye juzi usiku kwenye Uwanja wa Anfield. “Hii Liverpool, acha kabisa.”

“Nakumbuka hata wakati nilipokuwa Sevilla, nilicheza na Liverpool Ligi ya Mabingwa 2016, walikuwa wazuri. Ninawaheshimu na kutufunga ni kwamba walitimia kila mahali,” alisema.

Wakati Emery akisema hayo, kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp aliwatuliza mizuka mashabiki wake akiwataka wasianze kuwaza wala kushangilia ubingwa kwa kuwa ligi bado mbichi.

Liverpool inawania ubingwa wa 19 wa Ligi Kuu England kwani mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa 1990.

“Tumekuja kuwania nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa, suala la ubingwa kwa sasa hapana. Ninapambana kuingia nne bora,” Klopp alisema. “Unadhani nimeshamaliza ligi? Hapana.”

Mjerumani huyo alisema kuwa hataki kuwathibitishia suala la ubingwa kwa kuwa anawaelewa mashabiki wa Liverpool watawehuka kwa mizuka ya ubingwa.

“Ninataka watu wafurahi lakini wasipige kelele, wasubiri shughuli zima itakuwa Januari 3, tuna mechi na Manchester City.”

Ushindi wa Liverpool umeifanya timu hiyo kuongoza kwa pointi tisa kileleni.

Ainsley Maitland-Niles aliifungia Gunners bao la kuongoza lakini mabao ya Roberto Firmino na Sadio Mane na la penalti la Mohamed Salah yaliipa ushindi mnono Liverpool na kutawala sehemu kubwa ya mchezo.

Mbali na mchezo, kikosi cha Mauricio Pochettino kinazidi kupigwa mawimbi baada ya Wolves kuilaza timu hiyo katika mchezo uliokuwa wa ushindani.

Mapema kabisa, straika wa Tottenham, Harry Kane aliipa timu yake bao la mapema lakini mabao ya Willy Boly, Raul Jimenez na Helder Costa yalibadili kabisa sura ya mchezo.

Naye Aleksandar Mitrovic aliifungia Fulham bao la ushindi dhidi ya Huddersfield.

Ushindi huo unaifanya Fulham kupanda hadi nafasi ya 18 lakini Huddersfield inaendelea kubakia kwenye hatari ya kushuka.

Victor Camarasa aliizima Leicester kwa bao la dakika ya 92 na kuiwezesha Cardiff City kupata ushindi wake wa kwanza msimu huu.

Ushindi huo unakifanya kikosi cha kocha Neil Warnock kupaa hadi nafasi ya 16 ikiwa ni pointi nne zaidi ya anayeburuza mkia.

Watford ilipata pointi kwenye mechi ya Newcastle iliyopigwa Vicarage Road kwa mtokea benchi, Abdoulaye Doucoure kusawazisha zikisalia dakika nane mpira kumalizika.

Salomon Rondon alifunga bao na kuiwezesha Magpies kuwa mbele na matokeo hayo sasa yanafanya kikosi cha Rafael Benitez kushinda mechi moja kati ya saba ilizocheza.

Advertisement