Unavyoweza kusoma vitabu kwa simu

Tuesday January 22 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi

Usomaji wa vitabu kwa Tanzania ni utamaduni ambao haujazoeleka.

Wengi wanaamini kuwa usomaji wa vitabu ni kwa ajili ya wanafunzi au watu wenye uwezo hasa wa kununua machapisho mbalimbali..

Hii inatokana na kile kinachoonekana kuwa vitabu vina gharama kubwa hivyo mtu kushindwa kumudu kusoma vitabu vingi hata kama ana utayari wa kufanya hivyo.

Usomaji kupitia teknolojia

Kisingizio hicho kwa sasa kimepatiwa ufumbuzi; teknolojia imekusogezea vitabu mikononi mwako.

Hivi sasa kupitia simu yako ya mkononi unaweza kusoma vitabu mbalimbali.

Vitabu hivi vinapatikana kwa njia mbalimbali ikiwemo rahisi ya kusoma kwa kupitia ‘Apps mbalimbali ambazo zipo kwa ajili hiyo.

Kwa mfano, watumiaji wa simu za Iphone au Ipads, Kindle ndio app bora ya vitabu.

App hii imefanyiwa maboresho makubwa ambayo yanakufanya usiishie kusoma vitabu bali pia utapata fursa ya kusoma magazeti na majarida baada ya kujiunga kupata huduma hiyo.

Ndani ya app hii kuna kamusi inayokuwezesha pia kupata maana za maneno magumu unayokutana nayo wakati unasoma kitabu.

Hii inakurahisishia pale unapokwama au kushindwa kuelewa maana ya neno ulilosoma.

Unapokutana na neno ambalo linakuwia vigumu kuelewa maana yake, app inakupa maelekezo ya namna ya kufanya kupata maelezo ya kina kuhusu neno au msamiati husika.

Nyingine ni Kobo, hii inatajwa kwenda na kasi ya kidijitali kutokana na sifa yake kubwa ya kumuingiza msomaji wa kitabu kwenye mjadala.

Hata kama hujamaliza kusoma kitabu husika utakuwa na uwezo wa kuungana na wenzio ambapo pia wanasoma mkajadili kwa pamoja.

Pia unaweza kuandika maoni yako kuhusu kitabu katika hatua uliyofikia.

Kupitia Facebook pia unaweza kuwaunganisha rafiki zako ambao watakuwa tayari kusoma kitabu husika nao wakawa sehemu ya usomaji huo pindi watakapojiunga rasmi.

App nyingine inayoshauriwa kwenye usomaji wa vitabu ni Marvin.

Ukitumia ‘app’ hii una uwezo wa kubadili aina ya maandishi kwa kuchagua yanayokupendeza.

Pia unaweza kuongeza au kupunguza ukubwa wa maandishi.

Kwenye app hii unaweza kuchagua kiasi cha mwanga ambacho kitakuwa hakina madhara kwenye macho yako pindi unaposoma wakati wowote iwe mchana au usiku.

Upo pia uwanja unaomuwezesha msomaji kukichambua kitabu kwa kifupi na kueleza maoni yake kuhusu kitabu husika.

Kama unapenda kusoma kitabu kwa mtindo wa sauti, Serial Box ndio uwanja sahih.

App hii imetengenezwa kwa mtindo unaoendana na ule wa TV. Inatoa habari na visa kwa mtiririko wa vipande kwa kila wiki.

Aidha, inakupa fursa ya kuchagua kati ya maneno au sauti kama njia mojawapo ya kusoma kitabu.

Mwandishi Lana Winter-Hébert anasema zipo faida nyingi kwa mtu anayesoma vitabu ikiwemo kuongeza uwezo wa ubongo akiwa na maana kwana kama ambavyo kazi ama mazoezi huongeza uwezo wa misuli ya mwili, basi, ndivyo hivyo kusoma huongeza uwezo wa ubono katika kufanya kazi.

Advertisement