UCHAMBUZI: Urafiki huu kwa viongozi wa dini udumu hadi 2020

Kila wakati wa chaguzi hapa nchini kumekuwa kukiibuka mjadala juu ya fungamano la dini na siasa.

Mjadala huu hutawaliwa na wanasiasa wenyewe na huitimishwa na wanasiasa haohao, kuwa haitakiwi kuchanganya dini na siasa.

Baadhi ya viongozi wa dini ambao wana upeo na masuala ya kisiasa hubaki na msimamo wao kuwa huwezi kuwatenga wao na siasa.

Miongoni mwa hoja za viongozi wa dini ambao wamekuwa wakitetea kuhubiri masuala mbalimbali yakiwamo ya kisiasa madhabahuni na misikitini ni kuwa wote wanamuhudumia mtu mmoja – mwili na roho.

Lakini pia viongozi hawa wa dini ambao aghalabu ni wachache, hutoa hoja kuwa kama Siasa ni mbovu wananchi wote wakiwamo waumini wao, wanaathirika sawa, na siasa zikiwa nzuri wote hunufaika.

Wanasiasa ambao hutaka viongozi wa dini kujitenga na siasa ndio haohao utawakuta misikitini na makanisani wakiomba baraka za viongozi wa dini ili kuongoza vyema.

Hivyo ni wazi kuwa hoja ya kuwataka kuwatenga viongozi wa dini kuzungumzia siasa ni upofu.

Nasema upofu kwa sababu huwezi kuwazuia watu kujadili mustakabali wao wa maisha wakiwa ndani ya nyumba za ibada ama kupokea ushauri.

Lakini pia huwezi kuwafunga mdomo viongozi wa dini kuzungumzia mambo ambayo yakifanyika vibaya yataathiri maisha ya waumini wao.

Na kwa bahati nzuri viongozi wa dini ambao nyakati za uchaguzi huonekana ni maadui, mara nyingi wamekuwa wakihubiri wananchi kuchagua viongozi bora wanaomuogopa Mungu.

Viongozi hao wamekuwa wakihubiri kuchaguliwa viongozi wacha mungu ambao lazima watakuwa, wamejitenga na matendo ya wizi, unafiki, rushwa na kuvunja haki za binadamu.

Lakini mwisho wa mahubiri hayo wao huonekana na maadui na kupokea vitisho kuwa wanachanganya dini na siasa.

Ingawa kuna baadhi ya viongozi wa dini ambao hutumia vibaya madhabahu na misikitini kwa kufanya siasa za vyama, lakini ni wachache na wanaweza kudhibitiwa, hivyo isiwe sababu ya wote kufungwa midomo.

Mathalan, hivi majuzi viongozi wa dini waikaribishwa Ikulu kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli. Hili ni jambo kubwa sana na muhimu kwa mustakabali wa taifa, kwani linadhihirisha umuhimu wa dini katika siasa.

Ni jambo linalionyesha umuhimu wa wanasiasa kuwa karibu na viongozi wa dini kwa kuwa wote wanahudumia mtu mmoja na wote wa kuthaminiana.

Hivyo ni imani yangu kuwa urafiki huu baina ya viongozi wa dini na viongozi wa kisiasa utadumu hadi nyakati za uchaguzi na wataendelea kuvumiliana na kuheshimiana bila kujali tofauti zao, za kidini au za mitazamo.

Watanzania walio wengi wana imani kubwa na viongozi wa dini na ndio sababu kila wanapopata misukosuko katika jamii huwakimbilia kwa kuwa maamuzi na matendo yao humtanguliza Mungu.

Kwa sababu hata viongozi hujipambanua kuwa wao wanawajibika kwa Mungu ambaye amewatuma kuhubiri upendo, haki na kweli, ni imani ya wengi kuwa watatumia vizuri kwa manufaa ya watanzania wote fursa ya kuwa karibu na serikali kutoa ushauri mzuri.

Kutokana na ukaribu huo, ni vema viongozi hao wakatumia fursa hiyo kukidhi matakwa ya Watanzania. Kuna mambo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wengi ikiwepo suala la kuwa na Katiba mpya basi viongozi saidieni kusukuma ajenda hii kwa utulivu.

Lakini pia viongozi wa dini saidieni sana kupunguza uhasama unazidi baina ya viongozi wa kisiasa ili baraka za Mungu ziwatangulieni na kila mmoja kutomuona mwingine ni adui.

Viongozi wa dini tusaidieni kuhubiri kuwa tofauti za mitazamo ya kisiasa si uadui kwani nia ya viongozi wengi wa kisiasa na kupata dhamana ya kuongoza.

Itoshe kutoa wito upendo huu wa viongozi wa dini na serikali udumu milele lakini uwe kwa maslahi ya umma ili kuiwezesha Tanzania kuendelea kung’ara kwa mambo mazuri.

Tukifika hapo, naamini upendo na kuaminiana kati ya viongozi wa dini na serikali utadumu, hata kufikia hatua sawa na ya kiongozi mmoja kutoa kauli ya kuwasweka ndani wale wote watakaowabeza viongozi wa dini.

Mussa Juma ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Arusha. Simu: 754296503.