Usaliti wa Yuda una nafuu kwa huu unaofanyika miaka ya sasa

Muktasari:

  • Lakini yote kwa yote, bora akusaliti kila mtu hapa duniani, kuliko kujisaliti wewe mwenyewe. Na niamini mimi, ukikaa chini, ukatulia, ukajaribu kutafuta uwiano wa kati ya usaliti unaojifanyia mwenyewe na unaopata kutoka kwa wanaokuzunguka – takwimu zitakushangaza. Utagundua kuwa unajisliti kwa kiasi kikubwa zaidi ya wanavyokufanyia wengine.

Mambo yalianza vizuri tu… lakini baadae, Yuda akaachagua kuwa msaliti, Pasaka ikatokea.

Dhana ya usaliti imeendalea kubaki kwenye maisha yetu. Tunaishi na usaliti kila mahali – ofisini, nyumbani, shule, misikitini na makinasani. Na wasaliti wanatuzunguka kote – wazazi wetu wanatusaliti. Watoto wetu wanatusaliti. Marafiki wanatusaliti. Ndugu wanatusaliti. Wapenzi wanatusaliti na hata sisi wenyewe binafasi tunajisaliti.

Lakini yote kwa yote, bora akusaliti kila mtu hapa duniani, kuliko kujisaliti wewe mwenyewe. Na niamini mimi, ukikaa chini, ukatulia, ukajaribu kutafuta uwiano wa kati ya usaliti unaojifanyia mwenyewe na unaopata kutoka kwa wanaokuzunguka – takwimu zitakushangaza. Utagundua kuwa unajisliti kwa kiasi kikubwa zaidi ya wanavyokufanyia wengine.

Tulivyoanza mwaka uliweka lengo la kuacha pombe. Kushituka ukajikuta uko mwezi wa pili na utamu ni kwamba, bado ulikuwa unazichapa kama komba. Ulijisaliti.

Ukasema kuacha pombe sio kazi rahisi, kwa hiyo badala ya kuacha kabisa nitaanza kupunguza. Saa nazo zisivyojua kusimama, zikazunguka, kufumba na kufumbua zikatengenzea siku, siku zikatengeneza wiki, wiki ikazaa mwezi, mara ukajikuta uko mwezi wa tatu, na unywaji wako bado uko juu kama Piere mzee wa Liquid – hapo ulijisaliti mwenyewe. Sio baa, sio baa medi, sio watengeneza bia wala kundi unalokunywa nalo.

Na kujisaliti huku ndo kunakufanya Pasaka hii ikukute huna kitu. Kwa sababu wote tunajua sikukuu sio msiba, kalenda zilikuwa zinafahamu miaka mingi nyuma kwamba leo kutakuwa na pasaka, na hata wewe ulikuwa unafahamu.

Na ukapiga mahesabu vizuri sana kwamba hadi ikifika hii tarehe mbona utakuwa vizuri, uko na pesa za kutosha kuikabili sikukuu. Nyumbani patalika minofu, watoto watapendezaa, mambo yatakuwa mtelezo kama uchaguzi wa vyama vingi wenye mgombea mmoja tu.

Lakini ghafla sijui ni chuma ulete gani akakukumba. Pesa zikaanza kupukutika tu mifuoni kwako kwa kufanya matumizi ya kuparaganya. Matumizi yasiyo na macho, matumizi yanayosaliti mipango yako yote uliyopanga. Halafu ili kuhalalisha usaliti wako, ukajipa mahesabu mapya kwamba hata hela ikiisha mbona utapata tu mahali pa kuazima, kuzibia pengo.

Kuja kushituka sikukuu imefika, huna kitu na uliyemtegemea akukopeshe naye hana kitu kama wewe na hata angekuwa nacho bado ungekuwa umejisaliti tu.

Huku napo tayari Yuda ameshafanya usaliti wake, leo Yesu anapaa na inabidi tusherehekee tu bila kujali uko vizuri kiuchumi au laa. Hapo ndiyo utaelewa kwa nini Biriani ya Dar es Salaam inapendeza kuliwa ijumaa.

Hapa tunasema sio Yesu, sio Yuda, sio pasaka, sio kalenda ambayo imekusaliti. Ni wewe mwenyewe na nafsi yako. Pambana uachane na haka kamdudu ka kujisaliti, ndicho kanachokuzuia kupata vitu vingi vizuri. Uwe na pasaka njema.