Ushindi wa kishindo ni kitu cha namna gani?

Wednesday October 3 2018

 

By Padri Privatus Karugendo

Katika hali ya kawaida ushindi unaeleweka na kushinda kwa kishindo kunaeleweka. Wanaocheza mpira wa miguu wakifungana mabao mawili kwa moja, aliyefunga mawili anakuwa ameshinda. Lakini wakifungana mawili bila, aliyefunga anakuwa ameshinda kwa kishindo.

Au kama ni suala la kupiga kura, kama kuna wapiga kura 10, (Kumi hawa wana sifa ya kupiga kura na ndio namba inayohitajika kupiga kura), wanawachagua watu wawili, ili kati yao mmoja awe kiongozi; ikitokea mmoja wao akachaguliwa kwa kura tisa au kumi zote, anakuwa ameshinda kwa kishindo. Kama ni ushindi wa sita kwa nne, unakuwa ni ushindi wa kawaida. Na mtu huyo aliyeshinda kwa sita kwa nne, kama ana busara hawezi kuwapuuza wanne ambao hawakumchagua.

Sina lengo katika makala hii kuelezea maana ya neno ushindi na maana ya neno kishindo. Ni maneno yanayoeleweka vizuri kwa kila mtu aliye na akili timamu. Kwingineko, katika nchi nyingine zilizoendelea duniani, kushinda ni kushinda na kishindo ni kishindo.

Ushindi wa kishindo ninaoujadili katika makala hii ni ile kaulimbiu tuliyoizoea hapa Tanzania kila baada ya uchaguzi; uchaguzi mkuu na uchaguzi wa serikali za mitaa na hasa siku hizi chaguzi hizi za watu kuhama vyama vyao vya siasa na kujiunga na vyama vingine na kulazimisha kuurudia uchaguzi.

Ushindi wa kishindo, ushindi wa kimbunga na ushindi wa tsumani ni majigambo tunayoyasikia baada ya chaguzi hizi. Chama kinachotawala, CCM, kimekuwa na utamaduni wa kutamba na kuendeleza mbwembwe za kila aina kusherehekea “Ushindi wa kishindo”.

Ninaandika makala hii nikijua kwamba siasa ni taaluma. Kuna watu wanaisomea hadi kupata digrii ya kwanza, ya uzamili na uzamivu; hawa wana namna ya kujadili hoja ninayojaribu kuibua na wana maneno ya kisomi.

Hata hivyo, mimi ninafikiri mtu haitaji digrii ya chuo kikuu kuelewa mambo ya kawaida kama yale nitakayoyaeleza katika makala hii.

Mfano kama kwenye mtaa au kijiji kuna idadi ya wakazi 1,000. Kati yao 900 wana sifa za kupiga kura. 800 wanajiandikisha kupiga kura na 700 wanajitokeza kupiga kura – na wote 700, wanakuchagua kuwa kiongozi wao. Katika hali ya kawaida ni lazima utangaze kuchaguliwa kwa kishindo.

Lakini kama mtaa au kijiji kuna wakazi 1,000. Kati ya hawa 900 wana sifa za kupiga kura. 100 wanajiandikisha kupiga kura. Wanaojitokeza kupiga kura ni 50, na hawa wanakuchagua wote uwe kiongozi wa wakazi 1,000. Huu ni ushindi wa kishindo?

Kama huu ni ushindi wa kishindo, ni lazima tukubaliane maana hii mpya ya ushindi wa kishindo; vinginevyo tunaonekana hamnazo. Hili ndilo ninalolijadilika katika makala hii. Mtu anayechaguliwa na watu 50 kati ya 1,000 anawezaje kusimama na kujivuna kwamba amechaguliwa kwa kishindo? Je, hili linahitaji maelezo ya kitaalamu kueleweka?

Mtu anaweza kuliangalia hili kutoka upande mwingine. Mtu huyu aliyechaguliwa na watu 50 kati ya 1,000 wanaoishi kwenye kijiji chake, baada ya uchaguzi, badala ya kufanya sherehe za mbwembwe na majigambo ya kutia kichefuchefu; akaanza kutekeleza sera na ilani ya chama, akahakikisha huduma muhimu zinapatikana kijijini; akahakikisha kuna amani na utulivu; akahakikisha raslimali za kijiji zinalindwa na kutunzwa, uchaguzi unaofuata atachagulia kwa idadi ngapi ya watu?

Watabaki wale 50 au wataongezeka? Ni wazi kama mwenyekiti wa kijiji amefanya kazi yake vizuri idadi ya wapiga kura itaongezeka. Kinachotokea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, idadi ya wapiga kura inapungua. Kwanini idadi hii inapungua? Hili ndilo swali la kujiuliza na hiki ndicho kitu muhimu zaidi ya sherehe na mbwembwe tunazozishuhudia.

Kama takwimu za waliopiga kura kule Ukonga ni za kweli, (Ninaogopa kutaja idadi, maana sheria ya takwimu imekuja kivingine) ukilinganisha na waliojiandikisha, mshindi wa Ukonga hata kama angelipata kura zote, hawezi kujigamba kushinda kwa kishindo, maana idadi ya wale waliopiga kura wala si robo ya waliojiandikisha kupiga kura.

Tatizo ni nini? Kwa nini watu hawakupiga kura, wakati ni nafasi ya kumchagua mwakilishi wao? Ni wakati wa mbwembwe na majigambo au ni wakati wa kutafiti tatizo kwenye jamii ya Ukonga?

Uchaguzi wa marudio wa Ukonga, kwa mtu mzalendo, mwenye kulipenda taifa lake na si kuupenda tu ubunge wake, kwa idadi ndogo iliyojitokeza kupiga kura, angeamua kukaa pembeni na kuwapisha wengine. Huo tunauita uungwana, si lazima ufukuzwe, au watu wakwambie waziwazi kwamba hawakupendi, bali wewe unasoma alama za nyakati.

Panahitajika hata elimu ya uraia ili watu watambue umuhimu wa serikali za mitaa na kufahamu dhamani ya kura zao. Ni lazima tutengeneze mazingira ya watu kuamini kwamba kura ni muhimu; lazima tuvunje utamaduni unaojengeka hivi sasa kwamba hata tusipopiga kura, viongozi watapatikana tu; kwamba kura hazina maana yoyote ile, maana nchi hii ina wenyewe. Ni lazima Watanzania wakafahamu kwamba Tanzania ni yetu sote na tunaweza kuishi kwa amani na utulivu tukiwaingiza madarakani na kuwaondoa viongozi wetu kwa njia ya kupiga kura.

Kama CCM, ni chama makini kama kinavyojigamba, kwa nini badala ya kufanya sherehe na majigambo, wasifanye utafiti wa kina ili kubaini ni kwa nini hamu ya kupiga kura inapungua miongoni mwa Watanzania?

Kwa nini watu hawapendi kupiga kura? Na wale wanaopiga kura, kwa nini wanataka wanunuliwe kabla ya kufanya uamuzi wa wamchague nani? Kwa nini ile hali ya kawaida ya kuangalia sifa za mgombea na sera za chama inapungua kwa kiasi kikubwa? Kwa nini watu wengine wakubali kupoteza haki yao ya kupiga kura kwa kuuza shahada zao za kupigia kura?

Haya ndiyo maswali ya kujiuliza kwa mtu yeyote ambaye yuko makini katika siasa. Maoni haya si chuki dhidi ya CCM, bali ni ushauri wa msingi; pia ni ushauri ambao na vyama vya upinzani ni lazima viuzingatie. Idadi ya kupiga kura inapungua.

Watanzania hawapendi tena kupiga kura. Tatizo ni nini? Tatizo ni CCM au tatizo ni kwamba Watanzania hawaoni mwelekeo wa Taifa letu kisiasa? Inawezekana hawana imani tena na wanasiasa? Inawezekana hawaoni tena mchango wa siasa katika maisha yao?

Ushabiki wa kisiasa unatawala na kuwapumbaza hata watu tunaoamini wana hekima na busara. Fedha zinazotumika kutengeneza fulana, kofia na sare za chama, zinatosha kuendesha mradi wa maji katika vijiji kadhaa vya Tanzania au zingetosha kuwalipia wanafunzi wanaosoma vyuoni ili tuwapate wataalamu wengi katika nyanja mbalimbali.

Kwanini fedha hizo zinazotengeneza sare zisitumike kulisafisha Jiji la Dar es Salaam ili kipindupindu kisiendelee kupoteza maisha ya watu wa Dar es Salaam?

CCM ina sera zake, ina ilani ya uchaguzi. Ni kiasi gani CCM, imefanikiwa kutekeleza sera zake na ilani yake kwa kishindo? CCM, ina maadili ya uongozi, ni kiasi gani imetekeleza kwa kishindo maadili yake? CCM, inaamini kwamba “rushwa ni aduia wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa”, imetekeleza vipi kwa kishindo imani hii? CCM ya Mwalimu Nyerere, inaamini kwamba cheo ni dhamana – uongozi ni huduma! Ni kiasi gani haya yanatekelezwa kwa kishindo?

Wataalamu wa siasa watatueleza kwamba lengo la kila mwanasiasa ni kupata “Power” (madaraka). Huu ndio ulevi wa wanasiasa wote. Hata hivyo wanasiasa wenye fikra pevu, wazalendo – wanataka “Power” kwa malengo fulani, mara ya kuihudumia jamii.

Viongozi waliojitokeza kuwa madikteta duniani, wengi wao walikuwa na malengo ya kuwaendeleza watu wao. Walitaka kuwa na “power” ili watekeleze hayo malengo. Kwa mfano Hitler aliyekuwa mkatili kupindukia, alijenga Barabara Kuu za Ujerumani, ambazo leo hii ni muhimu sana kwa kukuza uchumi wa Ujerumani na nchi nyinginezo za Ulaya.

Marekani ni taifa linalopenda “Power”. Inapenda kuwa na “power” kuliko mataifa yote duniani; Inajulikana kama “Super Power”. Lakini jiulize, ni “power” ya nini? Ni “Power” ya kuhakikisha usalama na ustawi wa watu wake.

Kila chama cha siasa kikishinda uchaguzi, uwe wa kishindo au finyu kinasherehekea ustawi na usalama wa watu Marekani. Wanashangilia utekelezwaji wa sera na ilani ya uchaguzi. Na wale walioshinda uchaguzi, wako tayari kuwasikiliza waliowabwaga kwenye mambo yanayogusa ustawi na usalama wa nchi.

Machifu wetu hapa Tanzania, walikuwa mfano mzuri wa mtu anayeitumia “Power” kuwahudumia watu wake. Walihakikisha watu wao wanakula na kushiba. Machifu walihakikisha usalama wa watu wao, walihakikisha umoja wa watu wao. Pamoja na mambo mengine ya kibwanyenye yaliyouzunguka utawala wa kichifu; ni kwamba “Power” ilikuwa ni kuijenga jamii. Chifu aliyekwenda kinyume na huduma ya jamii, aliyeshindwa kuhakikisha shibe na usalama wa watu wake aliondolewa madarakani kwa mbinu zozote zile.

Ushindi wa kishindo, tunaotangaziwa na CCM, una lengo gani? Una lengo la kujenga chama cha mapinduzi au una lengo la kulijenga Taifa letu?

Ni kushinda kwa kishindo ili kufanya nini? Kama asilimia ndogo ya watu ndiyo imepiga kura na kukichagua Chama cha Mapinduzi kuna uhalali wowote chama hiki kutamba kwamba kimeshinda kwa kishindo? Mbwembwe hizi, majivuno na majigambo tunayoyashuhudia ni ya nini? Je, tunahitaji kutangaziwa ushindi wa kishindo au tunahitaji matendo ya kishindo katika kutekeleza sera na ilani ya chama?

Padri Privatus Karugendo

+255754633122

[email protected]

Advertisement