Ushirikiano mpya upinzani kuzaliwa

Oktoba 26, 2014 katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam, vyama vinne vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD waliandika historia kwa viongozi wake Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Freeman Mbowe (Chadema), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Dk Emmanuel Makaidi (NLD) kuweka sahihi ya makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kuanzia ngazi ya urais, ubunge na udiwani. Picha ya Maktaba

Muktasari:

Hata hivyo, pamoja na kushindwa, umoja huo uliendelezwa ukiwaunganisha wapinzani katika harakati za kisiasa, ingawa chama cha ACT-Wazalendo na vingine havikujumuishwa.

Dar es Salaam. Kuna kila dalili za ushirikiano mpya wa vyama vya upinzani nchini kuzaliwa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 lengo ikiwa ni kuing’oa CCM madarakani.

Ushirikiano huo wa vyama unaelezwa kuwa mbadala ya Ukawa ya sasa unaojumuisha vyama vinne vya CUF, Chadema, NLD na NCCR- Mageuzi vilianza kushirikiana kupigania Katiba mpya na baadaye katika Uchaguzi Mkuu 2015.

Ukawa ni wazo lililoibuliwa na Profesa Ibrahimu Lipumba wakati wa mjadala wa Katiba Mpya, ukilenga kuwaunganisha wajumbe, wakiwamo wa vyama vya upinzani waliokuwa wanataka rasimu iliyotolewa na Tume ya Marekebisho ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba ipitishwe.

Hata hivyo, pamoja na kushindwa, umoja huo uliendelezwa ukiwaunganisha wapinzani katika harakati za kisiasa, ingawa chama cha ACT-Wazalendo na vingine havikujumuishwa.

Huenda hatua ya Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alikuwa muumini wa Ukawa kuhamia rasmi ACT- Wazalendo kumekoleza chachu ya vyama hivyo kutaka kuungana.

Awali CUF chini ya Lipumba na baadaye chini ya Maalim Seif ilikuwa ikiunga mkono Ukawa lakini ACT- Wazalendo haikuwapo katika muungano huo.

Kwa sasa wafuasi waliokuwa CUF wakiongozwa na Maalim Seif wanaona umuhimu wa ACT kushirikiana na vyama vingine vya upinzani ili kuongeza upinzani katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Mwanachama mpya wa ACT, Nassor Ahmed Mazrui anasema kwa sasa chama chake kinaangalia namna bora ya kushirikiana na vyama vingine vya upinzani na kuleta tija.

Kwa mujibu wa Mazrui ambaye kabla ya kuhamia ACT alikuwa naibu katibu mkuu wa CUF, watashirikiana na vyama vyote vya upinzani vyenye nia moja vikiwamo vinavyounda Ukawa.

“Kwa sasa ACT inapaswa kubadilika si kama zamani, sasa ina nguvu kutokana na kupata wanachama wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa, hivyo hatuwezi kubeza ushirikiano wowote wenye tija.

Alisema Ukawa ni jina tu, la muhimu kwa sasa ni malengo ya ushirikiano utakaoanzishwa ili kuitoa CCM madarakani na kuongoza nchi.

Kwa mujibu wa Mazurui, ushirikiano unaotakiwa kujengwa sasa unapaswa uwe zaidi ya vyama vya siasa kutokana na hali halisi iliyopo.

“Sasa waathirika ni wengi ukilinganisha na vipindi vingine, wafanyabiashara, waandishi wa habari, wanawake na makundi mbalimbali yameumizwa; tunahitaji mabadiliko ya haraka na siyo tu kuwa na muungano wa vyama vya siasa pekee badala yake tunapaswa kuhusisha na taasisi za kiraia.

“Si lazima Ukawa, inaweza kuwa chochote tu lengo ni kukomboa watu maana waathirika ni wengi, hivyo yatupaswi kushawishi vyama kuwa na malengo zaidi.

Kwa upande wake Naibu katibu mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu alisema tayari vyama viwili kikiwamo ACT- Wazalendo na Chaumma vimewasilisha maombi ya ushirikiano na vyama vya Ukawa.

Kwa mujibu wa Mwalimu, ombi hilo lilitolewa wakati vyama sita vikiwamo (Ukawa+2) yaani vinne vilivyo katika Ukawa na vingine viwili vya ACT na Chaumma vilipokutana Zanzibar na kutoa Azimio la Zanzibar.

Mwalimu alisema baada ya mkutano huo, makubaliano ilikuwa ni kila kiongozi awasilishe ajenda hiyo ndani ya chama chake na kuijadili kisha kuleta msimamo wake pindi watakapokutana.

“Hatujachelewa wala kuwahi wakati utakapofika vyama vitaleta msimamo wake, naamini hapa ndipo tutapata pa kuanzia,” alisisitiza Mwalimu bila kusema taratibu hizo zitachukua muda gani kukamilika.

Akielezea zaidi Mwalimu alisema kwa sasa majadiliano ni namna gani vyama hivyo sita vitashirikiana kufanya kazi pamoja baada ya azimio lile la Zanzibar.

“Inaweza isiwe Ukawa tena na kuwa kitu kingine kabisa, pengine vyama vikaamua kuongeza chama kimoja au vyote, hii itajulikana baada ya vyama kutoa mapendekezo yake na kujadiliwa kwa pamoja pindi tutakapokutana.”

Kwa upande wake Profesa Ibrahimu Lipumba alisema Ukawa ulikuwa ushirikiano katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 ambako vyama vinne pekee ndiyo vilisaini makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja wa urais na kuachiana maeneo ambayo chama kina nguvu katika nafasi za ubunge na udiwani.

Kwa mujibu wa Lipumba, kwa sasa makubaliano yale yalishamaliza kazi yake kwa hivyo kuna haja ya kuwapo kwa makubaliano mengine katika uchaguzi ujayo na kwamba wao wako tayari katika ushirikiano huo utakaoanzishwa.

Wazo la ushirikiano huo linaweza kufanana na wazo la Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe la kuanzisha muungano mpya wa ushirikiano wa vyama vya upinzani, The United Democratic Front (DeFront).

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini alianza kulinadi wazo hili kwenye mtandao ya kijamii na kutumia msiba wa aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Buyungu, marehemu Kasuku Bilago mwishoni mwa mwaka jana kusisitiza.

Zitto alieleza kuwa ana dhamira ya kuona vyama vya upinzani na taasisi nyingine mbalimbali zikiunganisha nguvu dhidi ya CCM katika chaguzi mbalimbali.

Katika msiba huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe walikubaliana za Zitto (DeFront) kuanzia katika Jimbo la Buyungu.

Mbowe kwa kuonyesha kuunga mkono wazo hilo, alimsimamisha Zitto katika msiba huo na kusema kuwa wako tayari kushirikiana na vyama vingine na muungano huo utakwenda nchi nzima.

DeFront itakavyokuwa

Akizungumzia ushirikiano huo wa kidemokrasia (DeFront), Zitto anasema hilo ni vuguvugu litakalohusisha si vyama vya siasa tu, bali makundi mbalimbali katika jamii.

Alisema wazo la kuanzisha umoja huo limetokana na maazimio ya kikao cha Kamati Kuu cha ACT Wazalendo cha Januari 2018.