NDANI YA BOKSI: Utabiri wa Steve Nyerere, porojo za JB na harakati za Makonda

Kuna baa Uswahilini. Imechakaa, mazingira mabovu na ustaarabu wa kipuuzi, lakini inajaza wateja balaa. Mwenye nayo akijaribu kuboresha mazingira, wateja hutoweka. Usishangae, hata mwanamke mwenye adabu na mtulivu havutii mbele ya macho ya wanaume wengi. Atapita katikati ya kundi la masela Kariakoo, asitazamwe wala kufuatiliwa.

Hata mademu huvutiwa zaidi na wanaume vicheche. Wakati wanaume huvutiwa na demu kicheche kwa urahisi wa kumng’oa. Mademu huvutiwa na vicheche wa kiume kwa kutaka kujua ana nini mpaka anabeba mademu kila siku. Ndivyo ilivyo. Tunavutiwa na vitu vya kipuuzi zaidi. Akili zetu zina ulevi ndani yake bila hata kunywa pombe.

Steve Nyerere ‘ametrend’ wiki hii. Baada ya Ommy Dimpoz kutoa wimbo wake mpya. ‘Ametrend’ kuliko wimbo wenyewe kwa kauli yake kwamba Ommy Dimpoz asingeweza kuimba tena baada ya maradhi yake ya koo. Hii siyo mara ya kwanza ‘kutrend’ mitandaoni kwa vikauli vyake ambavyo siku zote huvitoa bila sababu za msingi.

Kosa ni kudhani Steve Nyerere anajutia kwa kilichotokea. Naamini na nina uhakika haujutii. Anafurahia kwa sababu anapenda. Wanapenda kuongelewa kwa ubaya au jema. Ndiyo maana vituko vyao haviishi kila siku wanaibua jipya. Siyo ‘mabrazameni’ wala ‘masistaduu’ wote wanapenda ‘kutrend’ kwa baya au jema. Ndo mchongo kwao siku hizi.

Unaitwa ‘Uwema Sepetu’ wa kupenda umaarufu kwa jema na baya. Nadhani kuna faida wanapata wao na marafiki zao. Katika hali ya kawaida kumuamini Steve kwenye mambo ya msingi uwe na akili ya mkopo. Lakini mbali ya viongozi kadhaa wa serikali kumuamini, wasanii walimuamini zaidi kiasi cha kumpa uongozi kwenye Bongo Movie yao.

Sasa mtu wa namna hiyo unadhani alisema bahati mbaya kuwa Ommy Dimpoz hana uwezo wa kuimba tena? Halafu leo hii anakataa kuwa hajasema bali wabaya wake wameungaunga video na maneno? Alikuwa na akili timamu wanazoziamaini mpaka baadhi ya viongozi na wasanii wakubwa kwa umri na majina. Tumeamua kuwa hivi tulivyo sasa.

Steve anaaminika na Jacob Steven a.k.a JB. Ambaye hivi karibuni kwenye kikao cha wasanii na Paul Makonda. Alisema hawezi kuongea hadharani mbele ya makamera na mikalamu ya waandishi matatizo ya wasanii. Madai yake kwamba yeye kuna watu wanamlipa pesa nyingi kiasi kwamba akisema mbele za watu itamharibia yeye.

JB hawezi kulingana hata theluthi na Diamond kimalipo ya shoo au matangazo. Lakini msikilize Diamond anapoongelea matatizo ya sanaa. Anaongea kama ‘andagraundi’ mwenye uchungu bila kuhofia lolote kwa faida ya sanaa. JB analipwa madudu gani mpaka hataki kuongea matatizo ya sanaa hadharani? Alifuata nini kwenye kikao pale?

Huyo ndiye msanii mkubwa kwa jina na umri. Anaongea hayo maneno hadharani tena kwa majigambo. Mambo yanayostahili kufanywa faragha wao huyafanya hadharani na mitandaoni. Yanayotakiwa kufanywa hadharani ndiyo wanataka kuyafanyia faraghani. Tumeamua kuwa hivi wenyewe.

Makonda naye alikatika stimu na maneno ya JB, akaamua kumtoa nishai mtu mzima. Kwamba kama anataka kuzungumza hayo mambo faragha, akafanye na mkewe nyumbani. Jacob matatizo ya sanaa yamekuwa mambo ya kuongea faragha kweli? Kibaya zaidi unaongea kwa majigambo kama wanamuziki wa Kikongo vile. Dah!

Kwenye kikao kile ukimsikiliza Nikki wa Pili alichoongea, utaona tofauti ya elimu yenye busara ndani yake na akili ya kawaida yenye mbwembwe ndani yake. Nikki wa Pili alisema kamera na waandishi mbele yao ni sehemu sahihi ya ‘kujibrand’ kisanii na sanaa. JB anasema mbele ya kamera siyo sehemu sahihi ya kuongea matatizo ya sanaa na wasanii.

JB anataka faragha. Kitu pekee alichoongea cha maana, ni suala la vikao vingi vya wasanii na sanaa kufanyika bila uwepo wa baadhi ya wadau wakubwa.Kama wasambazaji wa kazi za sanaa na wasanii. Ambao hivi sasa nao wameshindwa kuendelea na shughuli hizo bila kueleweke wazi matatizo yaliyochangia wao kuamua kuendelea na shughuli zingine.

Ingawa ukweli ni kwamba wasanii wenyewe ndiyo chanzo cha Steps au kina Mamu na Waswahili kuachana na biashara ya usambazaji wa kazi za wasanii. Kile kilichofanya kina Mamu kuacha kusambaza kazi za Bongo Fleva huku wakisambaza za kina Rose Muhando. Ndicho kilichofanya Steps kuachana na Bongo Movie na kuendelea na biashara zao zingine.

Wasanii na wadau mbalimbali kwa miaka mingi wanalalamika kuwa wasambazaji wa kazi za wasanii ni wezi. Yaani wanatajirika kupitia jasho lao kwa kugonga ‘kopi’ nyingi tofauti na kile wanachowapa wasanii husika. Hili lilianza kwa wanamuziki miaka ile mpaka Mamu na wenzao wakaamua kukaa kando na kuachana na biashara hiyo. Baada ya hapo wasanii wakakosa msambazaji wa kazi zao. Wakakomaa na ‘shoo’ tu ambazo walidai zinalipa kuliko kupeleka ‘albamu’ kwa Mamu anayeneemeka zaidi. Hili liliaminishwa kwa watu na kuonekana wasanii walikuwa wamejikomboa. Ajabu wanamuziki walipigika kimaisha huku Mamu na wenzao wakiendelea kuuza ‘albamu’ za kina Bahati Bukuku.

Mambo yakabadilika, awali wanamuziki walionekana mambo safi kuliko waigizaji. Baadaye waigizaji kupitia mauzo ya filamu pale Steps maisha yao yakawa juu kuliko Bongo Fleva. Walikuwa wanagonga ‘kopi’ na kuendesha magari watakayo huku Bongo Fleva wakisubiri ‘shoo’ za Fiesta. Kina Mamu wakaendelea ‘kudili’ na kina Bonny Mwaitege.

Baada ya Bongo Movie kuvimbiwa na mafanikio kama yale ya Bongo Fleva, nao wakaanza makelele yaleyale ya kina Afande Sele na wenzao. Kwamba wasambazaji wa kazi zao wanawadhulumu. Kwa maana kuwa wanachopata ni tofauti na kile wanachozalisha. Steps na wenzao wakaamua kukaa kando baada ya wingi wa shutuma. Kiko wapi?

Wakati Bongo Fleva wakilalamikia usambazaji wa kazi zao, kuna wadau walikuwa wakiwaunga mkono. Ndivyo ilivyo kwa Bongo Movie nao. Malalamiko yao yaliungwa mkono na wadau wengi mno. Lakini wasambazaji walipokaa kando hao wadau waliowaunga mkono wasanii wamekaa kando na kuwaacha wasanii wakiishi kiyatima mpaka leo.

Tatizo ni kwamba wadau wengi wanasikiliza zaidi malalamiko ya wasanii. Hawana muda wa kutaka kujua matatizo ya biashara ya usambazaji pia. Haiwezekani ‘Wadosi’ waache kibwegebwege tu biashara inayowaingizia mamilioni ya pesa kwa kelele za wasanii. Wangekaa nao wapange namna ya kuendelea kupiga pesa bila kususa jumla.

Kinachoshangaza wadau wengi wanashirikiana na wasanii kwenye malalamiko tu. Lakini wanajitenga katika kutafuta njia ya sahihi ya kujikomboa au kusambaza kazi zao. Siyo wasanii wala wadau wao walioweza kusambaza kazi za wasanii wala kusimamia. Soko limetoweka kama sura ya Lowassa kwenye vikao vya CCM pale Dodoma.

Paul Makonda mara kadhaa amejaribu kutafuta namna ya kusaidia wasanii. Mara ya kwanza alikuja na maandamano ya kupinga uingizaji wa filamu kutoka nje. Hili zoezi lilikufa kibudu. Lilikuwa jaribio la majaribio ya kujaribu jaribio lislilojaribika. Kikao kilichopita alikuja na ‘ajenda’ ya kujenga ukumbi wa kisasa wa maonesho na kazi za sanaa.

Makonda anachofanya anabeba ‘ajenda’ ya kitaifa wakati mipaka yake ya kazi haifiki hata kwa Jojo pale Kisarawe. Vikao vyake hufanya na wasanii tu, bila uwepo wa wawakilishi wa wizara husika wala wale wazee wa Basata pale Ilala. Analivaa jukumu mwenyewe, kwa utashi wake mwenyewe, na linaishia kwenye fikra zake mwenyewe.

Lakini bora yupi? Makonda anayeonyesha kuguswa na matatizo ya sanaa na wasanii. Au wizara na Basata wanaosubiri kufungia wasanii wakikosea? Kumuachia Makonda mwenye mamlaka Dar tu, wakati sanaa inagusa Taifa zima, vikao vyake na wasanii itakuwa kama ‘shoo ofu’ mitandanoni, mitaani na runingani bila utekelezaji.