Utafiti: fedha ni mgogoro wa kwanza kwa wanandoa

Sunday January 6 2019

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi

Ukistaajabu ya Musa subiri kuona ya Firauni, unajua kuwa ugomvi unaowafarakanisha wanandoa wengi unatokana na kugombania masuala ya fedha.

Kwa mujibu wa wataalamu wa saikolojia kutoka New York nchini Marekani wakiongozwa na gulu wa fani hiyo, Rachek Sussman aliyeongoza utafiti huo kuhusu migogoro inayojirudia kwenye ndoa, wameeleza kuwa fedha ndiyo sababu ya malumbano, talaka ya ndoa nyingi.

Amesema tofauti na watu wanavyofikiria kuwa kufumaniana, mitandao ya kijamii, kufanya kazi na kuwa na marafiki wengi ni sababu ya migogoro kwenye ndoa.

Ameitaja sababu inayofuatia kuwa ni malezi ya watoto na kukutana kimwili (kujamiiana).

“Nilijaribu kuwauliza watu kama wanajua chanzo cha migogoro mingi ya wanandoa wakajibu kuwa ni mitandao ya kijamii, uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa, lakini kwa upande wetu malalamiko hayo hajazi hata MB moja, linaloongoza ni masuala yanayohusu fedha, malezi ya watoto na kujamiiana,’’ alisema Sussman ambaye pia ni mshauri wa masuala ya ndoa.

Utafiti huo ulichapishwa kwenye majarida mbalimbali yakiwamo ya masuala ya fedha kama The Business Insider la UK, Literary Mama (International) na Not Very Quiet (Australia)

Kuhusu fedha alisema wanandoa wamekua wakilaumiana kuwa mmoja anatuamia zaidi ya mwingine , huku anayepewa akiona hazitoshi na kuamini kuna mahali zinakwenda nyingi tofauti na chache anazopewa yeye.

Rais wa kampuni ya ushauri wa masuala ya kifedha Cloud Financial Inc, Don Cloud akichangia utafiti huo alisema kuwa ili kumaliza tatizo hilo wanandoa wanapaswa kuweka bayana vyanzo vyao vya mapato au wajadili pamoja mambo yanayohusu fedha.

“Fedha ni tatizo, lakini lina dawa inayoliponya haraka, mtu ukitaka kumalizana naye ajue unaingiza kiasi gani, hapo hata ukipata fedha ya ziada hatokuhoji kwa sababu ile ya msingi anaijua na matumizi yake mnapanga pamoja,” alisema Cloud.

Kwa upande wa Suzan Mnzava alisema kuwa pamoja na kujua kila hatua ya matumizi hapo nyumbani hakuna siku aliwahi kupewa fedha inayotosha na mwenza wake.

Alisema wana watoto watatu wanaosoma ambao kila siku analazimika kuwapa nauli kwenye fedha anayopewa kwa ajili ya chakula.

“Hata wakija wageni wawili, mume wangu habadili wala kuongeza kiasi cha fedha anachoniachia kila siku, najikuta mara nyingi nachukia ujio wa wageni japokuwa ni baraka na najikuta nikimchukia yeye pia, ”anasema Mnzava na kuongeza.

“Sijawahi kuwa na furaha na mume wangu kuhusu masuala ya fedha, kila siku ananilalamikia natumia vibaya, ilhali hajawahi kunipa inayotosheleza…tangu nimeolewa sijawahi kupumzika na lawama hizi, ”anasema.

Anasema kuhusu malezi ya watoto kwa kweli baadhi ya wanaume hawaoni kama jukumu lao la moja kwa moja na kusema hana fedha hata kwa mambo ya msingi kama ada na chakula ni jambo la kawaida.

Naye Gabriel Emmanuel (39) mfanyabiashara Tandika anasema mwanamke hawezi kutosheka fedha na siku zote anawaza kupewa na mwanaume hata kama ni mumewe.

Huku akiwashirikisha wenzake Emmanuel alikuwa anajiuliza na kujijibu, “Eti kuna siku mwanamke alisema fedha unayompa inatosha, lakini anavaa anakula na upatu anacheza”.

Anasema kesi yake kubwa na mkewe na kuomba fedha, hataki kulisikia neno hilo ingawa akilala, akiamka ndiyo linaongoza kulisikia.

“Niliwahi kuishi na binti anafanya kazi kwenye kampuni za simu (tuliachana baadaye), huyo alikuwa na tamaa ya fedha hadi nikashindwa …Nikaona nioe mama wa nyumbani ili nimpangie matumizi kumbe nimetimua nyuki utafikiri aliachiwa mwongozo na aliyetangulia wembe ni ule ule, ”analalamika Emmanuel.

Akizungumzia malalamiko ya kulea Sussman alisema wazazi wamekuwa wakitupiana majukumu ya watoto licha ya kuishi nyumba moja.

Alisema wanaume wamekuwa wakiwalaumu wanawake kuwa wanawatumia watoto kama ngao ya kupata fedha nyingi kwa waume wao, huku wanawake wakilalamika kuachiwa majukumu.

Aliongeza kuwa malalamiko mengi ni ya wanaume wanapoona maisha magumu kuondoka nyumbani na kumuacha mama na watoto bila kujali atafanya nini na hana fedha.

Kuhusu chanzo cha malalamiko hayo alisema wanaume huwa wanajitetea kuwa wamekuwa wakitakiwa kutoa fedha nyingi kugharamia watoto waliozaa pamoja, fedha zisizolingana na anachofanyiwa watoto hao.

“Mtoto anakunywa chai ya rangi au uji wa lishe, lakini ukimuuliza mkeo mtoto anahitaji nini, utapangiwa maziwa lita mbili kwa siku, juisi tano sita kwa wiki ilimradi unatajiwa vitu usivyoviona.

“Wake zetu huwatumia vibaya watoto, ikitokea mkatengana ndiyo utajuta kuitwa baba, utalipishwa hadi kodi ya nyumba utadhani mama yao anakaa juu ya paa,” alilalama Emmanuel.

Anasema si hivyo tu wanawake pia hupenda watoto wao waonekane wa kishua hata kama baba yao hana fedha, hivyo kila siku kuwalalamika kuwa hawajaliwi.

“Ifike mahali mkubaliane tuwasomeshe watoto shule ya kulipia kulingana na kipato mlichonacho, mkeo anaweza kukurupuka kumpeleka mtoto shule ya gharama kubwa na madai kuwa atakusaidia, atafanya hivyo muhula wa kwanza inayofuatia utajua mwenyewe na ukifanya masihara anakupeleka ustawi wa jamii kukushitaki hutaki kuhudumia wanao, ”anasema.

Kwa upande wake mtaalamu wa saikolojia Josephine Tesha Mwakipake anasema kuwa wanandoa wengi wanagombana kuhusu fedha, malezi ya watoto na kujamiiana kwa sababu ndio mambo makuu yanayogusa hisia za umoja wa wanandoa.

Anasema muungano wa wanandoa unahitaji ufanisi na utaratibu mzuri katika masuala hayo matatu la sivyo hisia huguswa na kupelekea ugomvi.

Anafafanua kuwa fedha, malezi ya watoto na kujamiiana ni mambo ya muhimu sana katika wanandoa. Kukiwa na matumizi mabaya ya fedha au upungufu ni vigumu kuwa na maelewano, malezi ya watoto ni muhimu kuwa mazuri kwani watoto ndio matunda yatokanayo na ndoa, kujamiiana ndio tendo pekee la kuwafanya wanandoa kuzidi kuwa karibu.

“Suala la malezi ya watoto pia linaleta sana ugomvi sababu kila mmoja anakuja katika ndoa akiwa ana imani jinsi gani anataka kulea watoto kutokana na malezi aliyopata yeye na kila mmoja anaamini makuzi yake ni bora zaidi, tatizo katika fedha mara moja linatokana na kila mmoja kuwa na mtazamo tofauti na kuyapa kipaumbele mambo ambayo pengine si muhimu na lazima kwa mwenza wake,” anasema Tesha.

Tesha anafafanua kuwa mbali na sababu hizo kujamiiana ni miongoni mwa migogoro kati ya wanandoa kwani kunategemea zaidi utulivu wa masuala mawili yaliyotangulia yaani malezi bora ya watoto na upatikanaji au matumizi ya fedha.

Anaeleza kuwa “Iwapo mambo hayo hayapo sawa, hakuna mapenzi na kama hakuna mapenzi kujamiiana ni karaha hususani kwa mwanamke, mwanaume anaweza kufanya hayo mambo hata kama kuna mgogoro na akafurahia tofauti na mwanamke.

“Hali hiyo italeta mgogoro kwa wanandoa mwanaume akiamini labda mkewe ana mtu mwingine ndiyo maana halipi kipaumbele tendo hilo muhimu linalozidi kuwaweka karibu, lakini hali hiyo ikitokea mara moja moja kwa mwanaume, mwanamke huamini mwenza wake ana mtu anayempa huduma hiyo,” anasema.

Anasema kuwa kujamiiana huingia kwenye kila moja ya mambo yanayowagombanisha ambapo mwanamke asipoombwa unyumba na mwenza wake huamini ana mwanamke mwingine ambako pia hupeleka fedha na ndiyo maana hawatunzi watoto ipasavyo lakini hatimizi majukumu ya familia yanayohusu fedha kwa sababu anazipeleka huko.

“Kisaikolojia ili haya yote yakae sawa, wanandoa wanapaswa kuwa wazi katika kila hatua, kukiwa na siri hata kidogo inakuwa ngumu kila mmoja kumuelewa mwenza wake, ” anasema Tesha.

Akitoa majumuisho ya utafiti huo uliochapishwa kwenye jarida la Business Insider UK, Michael McNulty, mkufunzi wa mafunzo wa Chuo cha The Gottman Institute na muasisi wa Chicago Relationship Center alisema ndoa ni makubaliano ya hiyari hivyo hata namna ya kuiendesha inabidi kuwe na uwazi kati ya wawili hao.

“Siri za wanandoa zikizidi huleta uhasama mkubwa kati yao, wapo wanaofikishana polisi, mahakamani na hata kuumizana kuhusu hayo mambo matatu, suluhisho ni kuwa wazi,” alisema akikamilisha utafiti huo uliofanywa kwa mahojiano na nyaraka za kesi za waliokuwa wakitaka ushauri kwenye vituo mbalimbali.

Advertisement