Utafiti wahusisha uchafu wa kinywa na moyo kushindwa kufanya kazi

Kusafisha meno na kinywa angalau mara tatu kwa siku unajiondoka katika hatari ya moyo kushindwa kufanya kazi.

Korea Kusini. Je, unafahamu kuwa kusafisha meno angalau  mara tatu kwa siku inaweza kupunguza tatizo la moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure) kwa asilimia 10?

Kama ulikuwa hujui,  utafiti mkubwa uliofanywa kuanzia mwaka 2003 umeeleza kuwa kama husafishi meno  upo katika hatari ya kupata matatizo ya moyo.

Watafiti kutoka Korea Kusini wanasema matatizo hayo ya moyo ni pamoja na kushindwa kufanya kazi na kuwa na mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida.

Wanasema usuguaji wa meno wa kawaida kila siku angalau mara tatu unapunguza bakteria wanaoishi katikati ya meno na fizi, hivyo kuwazuia kuingia  katika mzunguko wa damu.

Utafiti huo wa wanasayansi ulioangalia uhusiano uliopo kati usafi wa kinywa na matatizo ya moyo, ulihusisha watu 161,000 wenye umri kati ya miaka 40 na 79 na kueleza kuwa kinywa kichafu husababisha bakteria  kwenye damu ambao pia hufanya mwili kuwasha.

Mwandishi mwandamizi wa utafiti huo, Dk Tae-Jin Song kutoka Woman's University Seoul, Korea Kusini anasema: “Tumefanya utafiti katika kundi kubwa la watu na kwa kipindi kirefu, ambao umeleta nguvu.”

Utafiti huo ulioanza kufanywa kati ya mwaka 2003 na 2004, ulichapishwa hivi karibuni katika jarida la European Journal of Preventive Cardiology. 

 (Daily Mail)