Utalii mchanganyiko Magamba ulivyowakosha wanafunzi Zanaki

Thursday January 3 2019

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Zanaki ya jijini Dar es salaam wakimsilikiza Ofisa utalii wa Hifadhi ya Asili ya Magamba, Samij Mremba. Hifadhi hiyo iko wilayani Lushoto Mkoani Tanga. Picha na Mpigapicha wetu. 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Zanaki ya jijini Dar es Salaam, wamevitaja vivutio vya utalii walivyokutana navyo ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Asili ya Magamba iliyopo Lushoto mkoani Tanga kuwa vya aina yake nchini ambavyo vinapaswa kuvifadhiwa na kutembelewa na Watanzania.

Wanafunzi hao waliotembelea hifadhi hiyo baada ya kushinda tuzo ya ubunifu iliyotolewa na Taasisi ya Great Hope Foundation ya jijini humo, walisema mchanganyiko wa vivutio vilivyopo Magamba unastahili kuenziwa.

“Nilichokiona kwenye Maporomoko ya Maji ya Mkuzu na kupandisha hadi kilele cha mlima Kigulu Hakwewa ni jambo la kipekee, ni vyema Watanzania tukapendelea kutembelea maeneo haya, ni utalii mzuri usiohitaji uhadithiwe,” alisema Ritha Seiya.

Katika ziara hiyo ya utalii iliyoratibiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii (TTB), mbali na wanafunzi hao kutembelea maporomoko hayo, pia walitembelea sehemu mbalimbali katika hifadhi hiyo ikiwamo vyanzo vya maji visivyokauka, maeneo ya miti ya kupandwa na asili, malikale zikiwamo majengo na handaki lililotumiwa na Wajerumani wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia.

Glory Kalenga anayesoma kidato cha sita katika shule hiyo alisema Magamba ina mambo mengi waliyoyaona na kujifunza ikiwamo mbega weupe ambao ni wanyama adimu duniani.

“Nimekuja huku nimeona miti mikubwa ya zamani sana yaani iliota sijazaliwa na sijui hata kama wazazi wangu walikuwa wamezaliwa, vilevile kuna hali ya hewa ya kuvutia sana ukiingia humu ndani (hifadhini) unasahau kabisa hata matatizo yako,” alisema Glory.

Naye Elizabeth Munisi alitaja uhifadhi bora wa mazingira unaofanyika katika hifadhi hiyo kuwa unaovutia zaidi na hasa unapohusishwa na mandhari ya mji wa Lushoto uliopo kilomita chache kutoka ilipo hifadhi hiyo.

“Ukiingia tu humu hifadhini huchoki kuangalia vivutio vilivyomo, pia mandhari ya mji wa Lushoto yanaonekana vizuri ukifika hapa kileleni (kilele cha mlima Kigulu Hakwewa),” alisema.

Kilele cha mlima huo kina futi 1,840 kutoka usawa wa bahari kikiwa na banda la watalii la kupumzikia pamoja na viti kwa ajili ya watalii wanaopenda kupunga upepo unaovuma kutoka pande mbalimbali za hifadhi hiyo.

Hata hivyo, Radhia Akili alitaka uwepo utaratibu utakaoandaliwa na Serikali kwa ajili ya kuwawezesha Watanzania kupenda kutembelea vivutio vya utalii ili kuinua mwamko wa kufanya hivyo.

“Ukiangalia takwimu za Watanzania wanaokuja hapa ni wachache ikilinganishwa na idadi ya watu tunaoishi Tanzania, lakini kama wakielimishwa watakuja kwa wingi na pia kukiwa na utaratibu wa kuwaleta mara ya kwanza, mara zingine watakuja wenyewe,” alisema.

Ofisa Habari wa TFS, Tulizo Kilaga anasema, licha ya kuwapo kwa changamoto ndogodogo, Hifadhi ya Asili ya Magamba ina vivutio vingi vinavyoitofautisha na maeneo mengi na kwamba uhifadhi unaofanyika unalenga kuvifanya vivutio vyake vidumu vizazi vingi vijavyo. “Ndiyo maana watalii hapa wanakuja, lakini pia kwa wananchi wengine wasiopajua Magamba waje waone utajiri ambao Taifa limejaliwa kuwa nao, nina uhakika watapenda kuja kila mara, maana kuna raha ya aina yake hapa,” anasema Kilaga.

Ofisa utalii wa hifadhi hiyo, Samiji Mremba anasema Magamba ina mandhari ya kipekee ya utalii ambayo mgeni anaweza kuyafurahia wakati wowote katika misimu yote ya mwaka.

“Ndiyo maana tunasema Magamba ni tofauti. Hapa mtalii anaweza kuja na kufurahia mandhari ya hifadhi wakati wowote, wapo watalii wanaokuja wakati wa masika wakafurahi na wengine kipindi cha kiangazi wakaondoka wamefurahi,” anasema.

Mremba anasema mfumo wa ikolojia ya Hifadhi Asilia ya Magamba unaundwa na hali ya unyevu usiokwisha kwa mwaka mzima na kwamba, hata kama jua litawaka vipi, hifadhi hiyo haibadiliki kirahisi.

Anasema, hali hiyo inachangia kuwapo kwa mito mingi midogo na maparomoko ya Mto Mkusu usiokauka ambao pia unatumika kama kivutio cha utalii kwa wageni na wenyeji wanaotembelea eneo hilo kutokana na kupita katika sehemu tofauti zikiwamo zenye udongo na mawe. “Huu mto kuna sehemu unapita katikati ya misitu, lakini maeneo mengine kuna mawe na hivyo mtu anaweza kusimama kando na kuangalia namna maji yanavyoporomoka,” anasema Mremba.

Advertisement