Utamu wa Monica na Brandy unanifikirisha Ruby na Nandy

Saturday May 25 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi

Iwe waliotengenezwa kwa uhasimu au vinginevyo. Kiu ya mashabiki siku zote ni muziki unaoakisi maisha yao.

Kizazi cha dot com wanaweza wasielewe hili, lakini cha millennia wanakumbuka ladha ya muziki kama The Boy is Mine, ngoma kali iliyoimbwa na wanadada Brandy Noorwod na Monica.

Wimbo unapopewa sifa ya utamu ulitulia kila idara. Kuanzia kwenye mashairi, muziki, mpangilio wa sauti na namna mabinti hawa walivyoutendea haki kwa ujumla.

Licha ya kuwa kazi hii ilitengenezwa miaka 21 iliyopita lakini ikipigwa hata leo uzuri wake unaonekana dhahiri kutokana na ulivyofanyiwa kazi.

Ukweli ni kwamba hata hapa Bongo tunao mabinti wanaoweza kutengeneza muziki mzuri wa kiwango hiki. Wapo wengi ila kwa sasa macho ya wengi yanawatazama Nandy na Ruby, mabinti hawa wote wamepita kwenye nyumba ya vipaji (THT).

Ni dhahiri kuwa Nandy ndiye msanii wa kike anayefanya vizuri kwa sasa, anajitahidi kuvuka mipaka na kujiimarisha kwenye soko.

Advertisement

Wakati anahangaika kupenya Afrika Mashariki, nyumbani hatuachii upweke, kila kukicha anaachia nyimbo tamu zinazotuburudisha na kusahaulisha matatizo yetu.

Ukisikiliza Kivuruge, Hazipo, Ninogeshe, Aibu One Day na nyingine nyingi za Nandy unaweza ukajikuta umesahau madeni yako kutokana namna binti huyu anavyoweza kuitumia sauti yake tamu.

Kwa upande wa Ruby unaweza kumtambulisha kama mwanamuziki aliyepikwa akapikika. Uwezo wake wa kuimba nyimbo ngumu, sauti yake tamu vinamfanya aendelee kuwa wa aina yake licha ya kuwa huwa anapotea na kurudi kwenye game.

Baada ya Yule akawa anapotea na kurudi lakini ukisikiliza kazi zake ikiwemo Alele, Ntade, Forever, Kelele utabaini uwezo mkubwa alionao binti huyu kwenye muziki.

Hamu ya wengi ni kuwaona hawa wawili wakisimama pamoja kutengeneza kolabo kama ile ya Brandy na Monica si lazima iwe kama The Boy is Mine kimaudhui, naamini inaweza kuwa kazi bora zaidi kuwahi kutokea Afrika Mashariki.

Kwa kifupi wapenda muziki mzuri wengi wanatamani hivyo, lakini matamanio haya yanaweza kuchukua muda mrefu kutimia kutokana na wawili hawa kutokuwa na maelewano.

Ingawa wenyewe hawajaweka wazi chanzo cha tofauti zao lakini ukisikiliza mazungumzo ya kila mmoja kuhusu mwenzake ni rahisi kubaini kwamba hawako sawa.

Ruby anaamini anakwamishwa na watu wanaompandisha Nandy, yaani kung’aa kwa Nandy kuna jitihada za watu wanaolenga kumshusha Ruby.

Katika mahojiano na kipindi cha Block 89 cha Wasafi Fm Ruby alikataa kulinganishwa na Nandy akieleza kuwa yeye ni yeye na ana mashabiki wake.

“Najua hata hao wanaotushindanisha ni kwa sababu hali hiyo imetengenezwa ila ninachofahamu mimi nina mashabiki wangu najua njia ninazopitia na ni namna gani naendelea kuwafanya waendelee kuwa wangu.’’

Nandy naye anaonyesha kutofahamu tatizo lililopo kati yake na Ruby ingawa anakiri kwamba hawako sawa.

Katika mahojiano yake aliyofanya wiki hii na kituo cha redio cha Times, Nandy amesema anatamani kukutana na Ruby uso kwa uso ili amuulize chanzo cha tofauti hizo.

“Nahisi kuna tatizo ila nikiwa tayari kumzungumzia Ruby nitatamani kwanza nikutane naye anieleze shida ni nini, hapo nitakuwa na cha kuzungumza kumhusu ila kwa sasa siwezi.”

“Unapoona msanii mpya u have to pull up your socks (unatakiwa ufanye juhudi) ili pale ulipokuwepo uende mbele zaidi au uwe sawa nae, sidhani kama anguko la mtu ni mtu mwingine, anguko lako ni lako mwenyewe, sijui kama ameanguka kwa sababu namuona bado ni msanii mzuri ni vitu vidogo tu,

“Still ana nafasi kubwa sana ya kujionyesha yeye kama Ruby, akitumia muda mwingi kufikiria kuhusu yeye na kujitahidi afike anapotaka kufika I think atafika,”

Hizo tofauti zao haziwezi kuwa na afya kwa mashabiki kwani tunachokitaka kutoka kwa warembo hawa ni kazi. Ni vyema wakamaliza tofauti zao wakatutengenezea ngoma moja yenye hadhi ya kimamtoni itupe raha, wapenzi wa muziki mzuri.

Advertisement