Utata kifo cha Nipsey Hussle, ni Freemason au tiba ya Ukimwi?

Los Angeles. Haikuwa wiki nzuri kwa wapenzi wa muziki wa rap duniani baada ya Nipsey Hussle kuuawa katika shambulizi lililofanyika nje ya duka lake la nguo Machi 31, mwaka huu.

Hakuwa rapa tu bali mwanaharakati aliyepambana kuhakikisha usawa hasa kwa Wamarekani wenye asili ya Afrika. Baadhi ya nyimbo zilizomtambulisha ni Blue Laces, Double Up, Crenshaw na Bullets Aint got No Name.

Akiwa nje ya duka lake la mavazi Marathon Clothing, alivamiwa na kushambuliwa kwa risasi nyingi na mbili zilimpata kichwani na tumboni na kukatisha safari yake ya miaka 33 hapa duniani.

Mshukiwa Erick Holder alikamatwa siku moja baadaye akijaribu kuingia katika hospitali ya wagonjwa wa akili.

Mwanamke aliyeendesha gari alilotorokea Holder alijisalimisha polisi akisema hakujua kama mwanaume huyo alilenga kufanya mauaji na alikimbia kuepuka kuuawa na wananchi wenye hasira.

Katika mitandao hasa Youtube zimekuwapo taarifa kuwa kifo chake kimetokana na kazi alizokuwa akifanya kwamba baadhi ya watu wanaoendesha dunia hawakuzipenda.

Rapa huyo baba wa watoto wawili, amefariki wakati akiendelea kuandaa jarida la Dk Sebi inayedaiwa kuwa aligundua dawa ya Ukimwi na kutibu wagonjwa watatu lakini alifariki katika mazingira ya kutatanisha.

Daktari huyo ambaye jina lake halisi ni Alfredo Darrington Bowman alikuwa raia wa Honduras lakini mara zote alipenda kutambuliwa kama Mwafrika anayeishi nchini humo.

Hussle aliyekuwa mchumba wa mwigizaji Lauren London, alikuwa akiandaa jarida kuhusu kifo cha Dk Sebi akihusisha na tiba zake hasa ile inayotibu Ukimwi.

Inadaiwa kuwa Hussle aliamini kuwa kifo chake kilifanywa na wazalishaji wa dawa hasa zinazohusiana na magonjwa ya Ukimwi, kisukari na sikoseli ambayo alikuwa akiyatibu.

Dk Sebi ambaye alitumia mitishamba kutibu wagonjwa, mara kadhaa alikamatwa nchini Marekani na mwaka 1987 alishtakiwa kwa kutengeneza dawa bila ya kuwa na kibali.

Miongoni mwa watu maarufu wanaotajwa kuwa wateja wa Dk Sebi ni marehemu mwanamuziki Michael Jackson na Lisa Lopez maarufu Left Eye.