Utitiri wa sherehe chanzo cha watoto kupotea uswahilini

Sunday February 10 2019

 

By Kalunde Jamal

Wazazi na walezi wa watoto kutokuwa makini kumetajwa kuwa miongoni mwa sababu za kupotea kwao.

Sababu nyingi ni kuwapo kwa vigoma vya uruguai, mikesha ya harusi na kwenye mikusanyiko ya watu.

Licha ya Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 inayolenga kuimarisha ulinzi, matunzo na haki za watoto Tanzania Bara, bado kuna wazazi hawatimizi wajibu huo.

Wazazi na walezi wana wajibu wa kuhakikisha kwamba watoto wanapelekwa kwenye chanjo, wanapatiwa huduma za afya, wanaandikishwa na kwenda shule, wanafuatiliwa maendeleo yao shuleni, wanasikilizwa na kupewa miongozo na matunzo.

Kwa mujibu wa takwimu za jeshi la Polisi, Dar es Salaam inaongoza kwa upotevu wa watoto ambapo mwaka jana walipotea 23, ikifuatiwa na Mara walipotea 16, Mbeya watoto 15 na Morogoro watoto 13.

Jeshi hilo lilitaja sababu mbalimbali zinazochangia watoto hao kupotea ikiwamo imani za kishirikina, kulipiza visasi, kujipatia vipato au uzembe wa wazazi au walezi.

Gazeti hili lilitembelea baadhi ya misikiti ambako kunatangazwa watoto kupotea mara kwa mara na kubaini kuwa uzembe wa wazazi, vigoma, mikesha ya harusi/sherehe mbalimbali ndiyo chanzo cha watoto kupotea.

Akizungumza na gazeti hili Juma Hussein Mbonde Imamu wa msikiti wa Rahman uliopo Temeke jijini Dar es Salaam, anasema kuwa kwenye maeneo ya Uswahilini watoto hupotea sana kutokana na kuwapo kwa shughuli nyingi ikiwamo mikesha.

“Wazazi, walezi huja hapa msikitini kuomba kutangaziwa watoto waliopotea, ukiuliza sababu utasikia nilikuwa shughulini na nilimuacha mtoto wangu akicheza na wenzake, nimerudi muda huu kila ninayemuuliza hajui alipo, ”anasema.

Anasema kwa wiki hawakosi matangazo mawili, na kuna wakati yanakuwa mengi zaidi ya hayo kutegemea na kuna tukio gani mitaani.

“Ombi langu ni wazazi kutambua wajibu wao, kwa sababu hakuna mtoto aliyepotea akiwa mikononi mwa mama au baba yake,” anasema Imamu Mbonde.

Mbonde anafafanua kuwa wengi wa watoto wanaotangazwa hupata walezi au wazazi wao na ambao hawajawapata hupelekwa kituo kidogo cha polisi.

Kwa upande wa Omari Ngoyo kiongozi wa msikiti wa Rahim uliopo Tandika Davis Corner, anasema msikitini haparuhusiwi kutangazwa jambo lolote zaidi ya dini, lakini kutokana na kukithiri kwa matukio ya watoto kupotea wamelazimika kusaidia jamii kutangaza.

Anasema wanachofanya sasa kabla ya kutangaza kupotea kwa mtoto huwataka wahusika kwenda kwanza kituo kidogo cha Polisi kutoa taarifa na kupatiwa RB.

“Matangazo hapa ni watoto kupotea ambapo huja mzazi au mlezi kutaka atangaziwe ili atakayemuona huko aliko atoe taarifa kituo cha polisi, au wasamaria wema waliokota mtoto kumtangaza ili familia yake ijue yupo wapi, ”anasema.

“Huku kwetu imani bado haba, watoto wengi hupotea mama zao wanapokuwa kwenye shughuli au watoto wanapokwenda kwenye hizo shughuli wakifuata ngoma hasa hivi vigoma ndiyo zaidi vinawapoteza sana na ukitaka kujua ni uzembe wa wazazi wengi wao hufuata familia zao, ” anasema Ngoyo.

Kwa upande wake Imam Hassan Said wa msikiti wa Ngamia uliopo mtaa wa Nyambwela kata ya Tandika anasema kwa mwezi hupata matangazo ya watoto kupotea yasiyopungua 20.

Anasema sababu ya hilo ni kutokana na spika za msikiti wao kufika mbali hivyo waliopotelewa au kuokota watoto huamini wakitangaza hapo sauti itawafikia wengi.

“Kipindi chenye ndoa nyingi, sherehe zinazoambatana na vigoma ndiyo watoto wengi hupotea, wazazi wanakimbilia na wao wanafuata bila kujulikana matokeo yake wakubwa hurudi na wao huendelea kufuata mdundo hadi wanapotelea mitaa wasiyoijua,” anasema Said.

Anasema licha ya kuwatangazia, pia huwasisitiza wazazi na walezi umuhimu wa kuhakikisha watoto wao wapo kwenye mikono salama.

Akieleza namna ambavyo husaidia kutangaza watoto waliopotea ustaadhi Shafii Issa wa msikiti wa Makuti Ilala anasema kuwa hupata kesi zisizopungua 15 kwa mwezi zikitofautiana wingi kulingana na matukio yaliyopo mitaani.

“Unadhani watoto wanapoteaje, wanaachwa wanazurura wanafuata ngoma, rusha roho na kisha hujikuta wamefika mbali na kwao na hawajui walipo,” anasema na kuongeza.

“Wakiletwa na wasamaria wema kutangazwa au mzazi akija kuomba atangaziwe tukiwahoji tunajua sababu, kina mama wapo bize na mambo yao na kuwasahau watoto, ”anasema.

Anasema kuna mmoja walimtangazia siku mbili mwanaye aliokotwa Bungoni na kuna mtu aliswali maeneo ya huko swala za mchana, aliporudi Magharibi akakuta tangazo likimzungumzia mtoto aliyesikia anatangazwa msikiti alioswali mchana ndiyo ikawa salama ya huyo mtoto.

“Wazazi wawe makini, kuna ambao ukimuuliza ilikuwaje anasema alikwenda kusuka asubuhi akamuacha anacheza na wenzake aliporudi saa 12 jioni kila anayemuuliza hajui alipo, huo si uzembe kitu gani unakwenda kusuka siku nzima na mtoto umemuacha anaranda,” anasema na kuhoji kwa ukali kidogo.

Naye ustadh Issa Khalif wa msikiti wa Al aqsa uliopo Kinondoni, Dar es Salaam anasema kuwa wanatangaza watoto waliopotea ingawa hawana idadi kamili kwa sababu hawaandiki na si jambo linalopaswa kufanywa misikitini kwa mujibu wa maamrisho ya Mtume Muhamad (S.A.W).

Anasema wazazi na walezi wasipokuwa makini suala la watoto kupotea litakuwa linawahusu kwa namna moja ama nyingine.

“Watoto wengi wanaokuja kutangazwa hapa wanakuwa wameokotwa na wasamaria wema, hatari iliyopo ni iwapo wataangukia kwenye mikono ya waasi ina maana hawataonekana tena.

“Kibaya zaidi tukiwatangaza baada ya muda jamaa zao wanapatikana na kwa kweli hakuna mwenye sababu ya msingi, mtoto ana miaka mitano au sita anakwenda shule mwenyewe na kurudi mwenyewe, akiteleza kidogo anapotea huo nauita ni uzembe , huyu anapaswa kupelekwa na kufuatwa kwa sababu bado mdogo, ”anasema Ustaadh Khalif.

Anasema mbali na hilo walezi hawaoni umuhimu wa kujua mtoto yupo wapi, “Kuna wengi wanakuja kuomba kutangaziwa, ukiwauliza wanasema ameondoka tangu asubuhi hadi jioni hajaonekana, ulikuwa wapi muda wote huo, nasisitiza wazazi watambue jukumu lao la msingi ambalo ni malezi ya watoto wao,” anasema.

Anasema jamii itakuwa inalaumu wanaoteka watoto kumbe wengine wanarahisishiwa kazi kwa sababu wanakutana na watoto wakizagaa mitaani.

Anafafanua kuwa kuna baadhi ya maeneo ukipita hadi saa moja usiku watoto wa chini ya miaka minne bado wanacheza nje, “Kwa mzazi au mlezi mweye akili na uchungu na mtoto hilo si jambo jema.

Anasema inajulikana wanawake wengi ndiyo wanatafuta riziki siku hizi, hivyo wahakikishe kabla ya kutoka wanawaacha watoto au mtoto kwenye mazingira mazuri na salama.

“Kwa sababu wapo pia ambao ukiwauliza wanasema walidamka asubuhi mama akienda kununua bidhaa za kuchuuza sokoni na baba kibaruani, bado wana wajibu wa kuhakikisha wanaangalia kwanza usalama wa watoto wao kabla ya kutoka, ”anashauri.

Kamishna wa Ustawi wa Jamii anayeshughulikia masuala ya watoto, Rabikira Mushi anasema mtu wa kwanza anayepaswa kujua usalama wa mtoto ni mzazi.

Anasema kama mzazi anamuacha mtoto wake mahali popote na kwa mtu yeyote ni rahisi kudhurika kwa namna yoyote ile ikiwamo kupotea.

“Ndiyo maana kila siku tunasisitiza watoto wapewe mbinu za kukabiliana na watu waovu, ila na wazazi watambue hilo ni jukumu lao,” anasema Mushi.

Anafafanua kuwa mtoto akipotea linakuwa ni suala la Taifa hususani watu wanaohusika na usalama wa raia, lakini mzazi anakuwa kwenye wakati mgumu zaidi.

“Hakuna wa kumtupia mpira huu, wazazi wengi hulalamika kupotelewa na watoto wao baada ya saa kadhaa kupita, hii inaonyesha namna gani hawakuwa makini, tuachane na wanaotekwa kwa bahati mbaya, tuwalinde hawa wanaopotea mitaani, ”anasema Mushi.

Advertisement