Utoaji chanjo kwa watoto, wajawazito waongezeka nchini

Friday May 24 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Moja ya maafikiano ya mkutano wa afya Afrika uliofanyika Machi nchini Rwanda, ‘Africa Health Agenda 2019’ ilikuwa kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa chanjo.

Nchi za Afrika zilijiwekea malengo hayo ukiwa ni mkakati w akufikisha huduma za afya kwa wote. Takwimu za wiki hii za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha upatikanaji wa chanjo umeongezeka duniani na asilimia 85 ya watoto wanachanjwa sasa hivi.

Ripoti ya shirika hilo inaonyesha mwaka 2017, zaidi ya watoto milioni 116 walipata dozi tatu muhimu kuwalinda dhidi ya magonjwa ya kuambukiza ambayo wakati mwingine husababisha ulemavu.

Chanjo ambazo hutolewa kwa watoto ni pamoja na ya homa ya ini, tetenus, surua, polio, kifua kikuu, dondakoo, kifaduro, nimonia na chanjo nyinginezo kulingana na uzito na umri wa mtoto.

Wataalamu wanaeleza kuwapo hatari kubwa mtoto chini ya miaka mitano akikosa chanjo kwani ana uwezekano wa kufariki haraka akishambuliwa na maradhi kwani mwili wake hauna kinga.

Tanzania baadhi ya mikoa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa chanjo kwa watoto hata wajawazito mfano Kagera na Mara.

Advertisement

Mkuu wa kitengo cha afya ya mama, baba na mtoto wa Zahanati ya Mwemage wilayani Misenyi, Neema Rugasiami anasema mafanikio hayo hayakuja siku moja kwani awali wazazi wengi walikuwa wanakwepa chanjo wakihofu kuwa zina sumu.

Neema anasema miaka mitano wazazi wengi hawakuwapeleka watoto wao vituo vya afya kupata chanjo.

“Wao waliamini ukimchanja mtoto anaweza kufariki au akaugua magonjwa mengi zaidi kwa hivyo ni bora asiipate kabisa,” anasema.

Lakini kutokana na mradi wa afya ya mama, baba na mtoto, anasema unaotekelezwa na wizara ya afya, walianza kutoa elimu ambayo iliwezesha kuwafikia wananchi hivyo kufanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya mama na mtoto.

“Mradi umesaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga, pia umbali ulisababisha wengi kutofikiwa lakini tuliwezeshwa kuwafikia na kuwapa chanjo na kutoa elimu kwa wenye imani potofu,” anasema Neema.

Hata hivyo hali ni tofauti katika pande nyingine kwani baadhi ya watoto wakubwa hawakuwahi kupata chanjo. Miongoni mwa watoto hao ni Elisha Rutha ambaye aliyeanza kupewa chanjo akiwa na umri wa mwaka mmoja na miezi saba, Februari mwaka huu.

Mkuu wa kitengo cha huduma ya mama, baba na mtoto wa Hospitali ya Mugana, Widelina Kawegere anasema Elisha ni mtoto wa mfano ambaye ameishi mikononi mwa mama yake kwa kipindi hicho chote pasipo kupewa chanjo.

“Nilimpokea kutoka kwa mtoa huduma ngazi ya jamii kwa sababu alizaliwa nje ya kituo cha afya,” anasema Widelina.

Kawegere anasema hali ya chanjo katika kituo chake ni nzuri lakini kabla ya kuanza kwa mradi huo, baadhi ya wazazi hawakuwapelaka watoto wao.

Mkurugenzi wa mradi wa afya ya mama na mtoto (MCSP) kutoka Shirika la Jhpiego, John George anasema mradi huo ulianza kutekelezwa Juni 2014 na utakamilika Juni mwaka huu.

Kwa kushirikiana na Serikali, anasema mradi huo ulijikita kuzuia vifo vya mama na mtoto vinavyoweza kuzuilika, ukifadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia shirika la kimaendeleo la USAID katika mikoa nane.

Taarifa za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha wajawazito 30 hupoteza maisha kila siku nchini wakati wa kujifungua ambao ni sawa na vifo 11,000 kila mwaka.

Miongonimwa mikoa iliyojengewa uwezo wa kukabili vifo hivyo, George anasema ni Mara na Kagera ambako wameshirikiana na wataalamu waliopo.

“Tunatekeleza shughuli zinazoleta matokeo makubwa, kwa kushirikiana na Serikali, lengo ni kuongeza idadi ya watoto chini ya miaka mitano wanaopata chanjo kuzuia magonjwa kuanzia wanapozaliwa mpaka miaka mitano,” anasema.

Msukumo wa mradi huo ulitokana na ukweli kwamba wilaya 19 zilikuwa chini ya kiwango cha kitaifa cha chanjo cha kutoa huduma hiyo kwa asilimia 80. Hali hiyo, anasema ilitokana na wazazi wengi kuwaficha watoto wao ili wasichanjwe kutokana na imani potofu lakini baada ya kuelimishwa matokeo yameanza kuonekana.

Anasema kazi kubwa ilikuwa kuwafuatilia wanawake na kuhakikisha watoto wanapata chanjo na jamii ambayo ipo mbali na vituo vya afya inapelekewa huduma hukohuko iliko.

Suala jingine walilolipa uzito ni utunzaji wa chanjo, walihakikisha zinawekwa ubaridi unaotakiwa kwa kununua majokofu na kusimamia mfumo wa ufuatiliaji.

Mganga mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dk Marco Mbata anasema utoaji chanjo umepanda kutoka asilimia 80 hadi kufikia 87 mkoani humo kwa miaka ya hivi karibuni. Mabadiliko hayo anasema yamechangiwa na utekelezaji wa mradi huo uliosaidia kuwafuata wananchi wanaoishi maeneo yasiyofikika kwa urahisi ikiwamo Misenyi hali imebadilika hivi sasa.

“Tulikuwa tunashindwa kuyafikia maeneo ya visiwani pia lakini kwa sasa tumefanikiwa kupitia wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao wanaishi kule, wanahamasisha kuwafikisha hospitalini watoto kupata chanjo,” anasema.

Chanjo kitaifa

Licha ya mafanikio katika mikoa hiyo, hali ni tofauti katika Kijiji cha Dakawa, wilayani Morogoro kilichopo kilomita 133 kutoka mjini ambako baadhi ya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano hawapati chanjo.

“Changamoto kubwa tangu nilipokuwa na ujauzito sikuchoma chanjo yoyote na nilipojifungua mwanangu hakuwa amepata chanjo yoyote mpaka anafikisha miezi mitatu. Nilijiongeza kwa kwenda Kituo cha Afya Duthumi (kilomita 7 kutoka kijiji anachoishi) ndipo mwanangu alianza chanjo hizo akiwa na miezi minne,” anasema Hawa Ndede.

Mjamzito mmoja kijijini hapo, Rehema Mkupe anasema mpaka mimbayake inafikisha miezi minane hakuwahi kupata chanjo na alipojaribu kwenda kituo kingine aliambiwa arudi alikotoka.

Wakati kukiwa na mafanikio katika baadhi ya maeneo, Tanzania kwa ujumla ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika kutoa chanjo ikifanya hivyo kwa wastani wa zaidi ya asilimia 90 ikiwa nyuma ya Rwanda inayotoa kwa asilimia 99.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile anasema, “Tanzania tumepiga hatua, hivi sasa tumefika asilimia 97 ya walengwa wote chini ya miaka mitano.”

Advertisement