Vijana milioni 5.7 wasubiri fursa ‘kuonja’ uchaguzi 2020

Saturday January 26 2019

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikisubiriwa kutangaza tarehe ya kuanza uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura, imefahamika kuwa zaidi ya Watanzania 5,700,000 wanasubiri kupata haki hiyo ili waweze kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa mara ya kwanza mwaka 2020.

Haki hiyo vijana hao wataipata endapo NEC itafanya maboresho ya daftari hilo kabla ya uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba mwakani.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ibara ya 5(1) kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofaywa hapa nchini.

Hata hivyo, ibara hiyo inasema Bunge laweza kutunga sheria na kuweka masharti yanayoweza kuzuia raia asitumie haki ya kupiga kura, kama inavyofafanuliwa katika kifungu cha 63 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura 343.

Ni kutokana na matakwa hayo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kati ya uchaguzi mmoja na mwingine hulazimika kuboresha daftari la wapigakura ili kuingiza wapya na kuwaondoa waliopoteza sifa za kunufaika nasuala hilo la kidemokrasia.

Ikiwa NEC itaamua wakati wowote kutekeleza wajibu huo vijana hao zaidi ya milioni 5.7 fursa hiyo wanatarajia kuingizwa katika daftari hilo.

Vijana hao ni wale ambao wakati Uchaguzi Mkuu 2015 walikuwa na umri kati ya miaka 13 hadi miaka 17 ambao mwakani watakuwa na umri kati ya miaka 18 na 22, kwa mujibu wa ripoti ya makisio ya idadi ya watu nchini iliyotolewa Februari mwaka jana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Katika kipindi hicho (Oktoba 2015), makisio ya NBS yanaonyesha kuwa vijana waliokuwa na umri wa miaka 13 walikuwa 1,335,636, wa miaka 14 walikuwa 948,185, miaka 15 (1,438,305), miaka 16 (1,018,587) na miaka 17 (1,029,427). Jumla ya vijana hao endapo wote watakuwa hai hadi 2020 itakuwa ni 5,770,140.

Mwaka 2015 Watanzania 22,750,789 walijiandikisha kwenye daftari hilo wakiwa na sifa stahiki.

Kwa takwimu hizo, bila kuhusisha idadi ya watakaoondolewa katika daftari hilo, idadi ya wenye sifa ya kupiga kura mwaka 2020 inaweza kufikia milioni 28.5 kutoka milioni 22.7 ya mwaka 2015.

Mwaka 2015, NEC iliboresha daftari hilo kwa kutumia mfumo wa teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration (BVR) na kufanikisha idadi hiyo ya wapigakura. BVR ni mfumo wa kuchukua taarifa za mtu za kibaiolojia hasa alama za vidole, ambao unawezesha taarifa za mpigakura kuona na za kitambulisho cha taifa.

Zoezi la uandikishaji

Licha ya umuhimu wa kuboresha daftari hilo, hadi sasa ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu, haifahamiki ni lini haki hiyo ya kikatiba itapatikana kwa mamilioni ya Watanzania.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dk Athuman Kihamia anasema taarifa za uboreshaji wa daftari hilo zitatolewa hapo baadaye.

“Muda ukifika tutasema, kwa hiyo sihitaji kutoa ufafanuzi zaidi wa swali lako lakini muda ukifika tutawaeleza.”

Hata hivyo, Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura 343 inaelekeza kuwa maboresho ya daftari hilo yafanyike mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Mwaka 2015 wananchi waliokuwa na sifa za kupiga kura na wale waliokuwa tayari na kadi za mpigakura za zamani, walilazimika kuandikishwa upya katika vituo 40,015 ngazi za vitongoji, vijiji na mitaa.

Kupiga au kutopiga kura

Pamoja na ‘hamu’ ya vijana wengi kushiriki mara ya kwanza katika uchaguzi, bado kuna mamilioni ya wapigakura ambao hawajitokezi kutumia haki yao. Ripoti ya NEC ya 2015 inabainisha kuwa wapigakura walioandikishwa walikuwa 23,161,440 lakini waliopiga kura katika kiti cha Rais walikuwa 15,596,110 sawa na asilimia 67.34 ya walioandikishwa na ambao hawakujitokeza walikuwa 7,565,330 sawa na asilimia 32.66 ya walioandikishwa.

Katika ufafanuzi wake, Dk Kihamia anasema sababu ya Watanzania kutopiga kura linatokana na kutofahamu umuhimu na uhusiano kati ya kura zao na maendeleo yatakayogusa maisha yao ya kila siku kupitia kiongozi watakayemchagua.

“Ni nature yetu, Watanzania wana tabia ya kupuuza vitu, ingekuwa tatizo la uraia, mbona wakati wa maboresho ya vitambulisho wanakimbilia kujiandikisha wengi? wengi ni wajuaji na hawajajua uhusiano wa maendeleo na uchaguzi. Hawaoni kama jambo kubwa.

“Mechanism (mbinu) ya utoaji elimu si tatizo ila tatizo liko kwenye utamaduni wa Watanzania, mfano hata kulipa kodi ni shida,” anasema.

Ingawa hakueleza ni lini, anasema NEC imejiandaa na utaratibu wake katika utoaji wa elimu ya uraia kwa wananchi ili kumaliza changamoto ya watu wenye sifa kutopiga kura wakati wa uchaguzi.

Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally siku chache zilizopita alinukuliwa na gazeti hili akisema ushindi wa CCM unazidi kupungua siku hadi siku kutokana na wapigakura kukosa imani na mifumo ya uchaguzi, ikiwa pamoja na vyama kutoa rushwa za mavazi na pesa.

Dk Bashiru anasema wapigakura wameanza kuona kituko na mchezo wa kuigiza katika chaguzi zinazofanyika nchini, akitolea mfano wa kujitokeza chini ya asilimia 50 ya wapiga kura walioshiriki katika chaguzi ndogo za marudio.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Utawala Bora kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mohammed Bakari anasema wapigakura wamekuwa na tabia ya kufanya tathmini.

Wanajiuliza, “Je, nikienda kushiriki kura yangu itakuwa na thamani? Au utamaduni ni uleule tu? Mtu anaona hakuna umuhimu wa kupiga kura, anakata tamaa ya kushiriki tena. Ni dalili za kufanya vibaya zaidi kwa chama,” anasema.

Advertisement