Vitambulisho vinavyozikosesha benki wateja

Thursday September 27 2018

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Alipokuwa anaweka juhudi kwenye kilimo msimu wa mwaka jana hakujua kama mambo yatamnyookea na kumpa changamoto mpya.
Joshua Haule (20) anasema baada ya kuona mambo hayaendi vizuri aliamua kwenda Kilombero kulima mpunga ambako milango yake ya kiuchumi ilifunguka.
Anasema alilima eka sita na akafanikiwa kuvuna magunia 40 ambayo yameongeza mtaji wake wa biashara. “Tatizo ni namna ya kutunza fedha nilizopata,” anasema Joshua.
Baada ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2013, Joshua anasema alipata kazi ya kuuza duka la chakula kama vile mchele, unga wa mahindi na ngano, maharagwe, ulezi na choroko hivyo kulazimika kuhamia jijini Dar es Salaam.
Akiwa dukani hapo akafahamiana na wakulima wanaoleta mchele waliompa taarifa za kilimo hicho hivyo kushawishika kwenda kulima mpunga.
“Nilikuja mjini mwaka 2014 na mpaka leo sina akaunti ya benki. Sikuwa kushika hela nyingi kabla ya kuvuna na kuuza mchele huu,” anasema Joshua.
Kilichotokea Joshua aliuza kwa jumla mchele wake na kuingiza Sh5 milioni alizopaswa kulipwa kwenye akaunti ya benki ambayo hakuwa nayo.
Alipoenda benki akakuta masharti magumu kwake kwani alitakiwa kuwa na kitambulisho ambacho hajawahi kuwa nacho. “Niliambiwa niwe na barua ya Serikali za mitaa pamoja na kitambulisho cha Taifa au kadi ya mpiga kura, leseni ya udereva au paspoti ya kusafiria. Sina kitambulisho hata kimoja,” anasema.
Kutokana na changamoto hiyo, alilazimika kuweka fedha hizo kwenye laini yake ya simu aliyonunuliwa na bosi wake lakini hazikuingia fedha zote.

Meneja uhusiano na mawasiliano wa Vodacom, Jackline Materu anasema kipo kiwango cha mwisho ambacho mteja anaweza kutunza kwenye akaunti yake ya M-Pesa kulingana na kanuni za Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

“Mwisho wa kutunza fedha ni Sh3 milioni, huwezi kuzidisha hapo vinginevyo upewe kibali cha kuongeza ukomo huo ambacho ni lazima ulete leseni ya biashara unayofanya,” anasema Jackline.

Kuhakikisha anapata fedha zake zote, Joshua anasema alilazimika kutafuta laini nyingine ya simu na kuweka kiasi kilichobaki.

“Najua zitapungua nitakapozitoa lakini sina namna,” anasema Joshua.

Joshua hatofautiani na Ashura Yamungu (19) anayefanya biashara ndogo ndogo ambaye anasema anashindwa kuwa na akaunti ya benki kutokana na kutokuwa na kitambulisho kinachohitajika.

“Natumia simu yangu tu. Kinachosumbua ni kwamba ukipat amajaribu, unazitoa wakati wowote kwani kuweka hela kwenye simu ni kama umezishika mkononi,” anasema.

Huduma za benki

Ingawa historia ya huduma za benki ipo tangu mwaka 1905 ilipoanzishwa Benki ya Deutsch-Ostafrikanische jijini Dar es Salaam na Wajerumani, bado huduma hizo haziwafikia wengi.

Kukiwa na zaidi ya benki 50 hivi sasa, takwimu zinaonyesha ni mtu mmoja katika kila watano ndiye anayetumia huduma za benki (asilimia 17) nchini hivyo kuifanya Tanzania kuwa ya mwisho ikilinganishwa na majirani zake wa Afrika Mashariki (EAC).

Takwimu za Shirika la Fedha Duniani (IMF) mwaka 2016 zinaonyesha wastani wa matawi mawili ya benki huhudumia 100,000 huku kukiwa na mashine 40,554 za kutolea fedha (ATM) kwa idadi hiyo ya watu.

Mpaka mwaka 2015, kulikuwa na matawi 782 pekee ambayo mengi, yalikuwa yanapatikana mjini hasa Dar es Salaam, Arusha na Mwanza. Lakini, teknolojia ya simu za mkononi imerahisisha upatikanaji wa huduma hizo.

Muongo mmoja tangu huduma za fedha zianze kupatikana kupitia simu za mkononi, maboresho yamefanyika na sasa unaweza kutunza na kukopa fedha hata huduma za bima hivyo kuongeza ushindani kwa benki za biashara zinazolazimika kutafuta mawakala maeneo tofauti, mjini mpaka vijijini.

Mpaka mwaka 2016, benki zilizokuwa zinazoongoza kwa mali nyingi ni CRDB ilikuwa na Sh5.2 trilioni ikifuatiwa na NMB iliyokuwa na Sh5 trilioni na NBC Sh1.7 trilioni.

Nyingine ni Standard Chartered iliyokuwa na mali za Sh1.4 trilioni licha ya matawi zaidi ya 1,200 yaliyosambaa katika nchi saba barani Asia, mashariki ya kati na Afrika. Ya mwisho kwenye orodha hiyo ni Stanbic iliyokuwa na Sh1.1 trilioni.

BoT

Taarifa ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kwa miezi 10 mpaka Aprili, miamala yenye zaidi ya Sh3.3 trilioni ilikuwa imefanyika kupitia simu za mkononi.

Takwimu hizo zilizomo kwenye taarifa hiyo iliyotolewa Juni, zinaonyesha kiasi hicho kilifanywa na zaidi ya watumiaji milioni 19.5 waliosajiliwa ambao waliongezeka kutoka milioni 17.3 waliokuwapo Aprili 2017.

Ongezeko la miamala hiyo, pamoja na mambo mengine, limechangiwa na urahisi wa kutuma fedha kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine. Septemba 2014, Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza duniani kuruhusu miamala ya aina hiyo kwa wateja wa Vodacom, Tigo, Airtel na Zantel.

Kutokana na idadi kubwa ya wananchi wanaotumia huduma za fedha kwa simu za mkononi, mtaalamu wa masuala ya fedha na benki, Asanterabi Joseph anasema endapo kampuni husika zitaomba kibali cha kuwa na benki, huenda zilizopo zikafa.

“Kampuni za simu zimeongeza ushindani. Benki sasa hivi zinalazimika kushirikiana nazo kupata wateja. Zinaenda mpaka mtaani na kuweka mawakala huko. Angalia, kampuni inawateja milioni saba, ikisema iwe benki unadhani itakuwaje,” anasema Joseph.

Finscope 2017

Joshua na Ashura ni miongoni kundi kubwa la vijana ambao wanakutana na changamoto za kutokuwa na kitambulisho kupata huduma kwenye baadhi ya ofisi na taasisi.

Ripoti ya Taasisi ya Uendelezaji wa Huduma za Fedha Tanzania (FSDT) ijulikanayo kama Fincsope ya mwaka 2017 inaonyesha asilimia 65 ya Watanzania wanapata huduma za fedha kupitia simu za mkononi.

Tofauti na hali halisi iliyopo, benki za biashara na taasisi nyingi za fedha zinahitaji kitambulisho cha kila mteja wake kabla ya kumhudumia.

Sio benki pekee ambako wasio na kitambulisho hupata shida kuhudumiwa. Jackline Paschal anasema ukienda kukata tiketi ya treni kwenda Kigoma ni lazima uwe na kitambulisho au barua ya Serikali za Mitaa.

“Kama hauna kitambulisho hupati tiketi. Hata ukisafiri kwa basi, njiani kuna vizuizi ambako askari hukagua kitambulisho kwa kila abiria,” anasema.

Simu

Kutokana na changamoto za utambulisho, ni rahisi kwa mwananchi kumiliki simu ya mkononi hivyo kupata huduma za fedha kuliko kufungua akaunti benki. Takwimu zinaonyesha asilimia 93 ya Watanzania wanatumia simu ya mkononi.

Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) 2018 iliyotolewa Juni inaonyesha ongezeko la asilimia 2.8 la watumiaji wa huduma hizo ndani ya mwaka mmoja uliopita.

Wateja hao wameongezeka kutoka milioni 20.28 waliokuwapo Juni 2017 hadi milioni 20.85 mwaka huu huku Vodacom na Tigo zikihudumia zaidi ya asilimia 74 ya wateja wote. Vodacom ina asilimia 41 ya wateja wote na Tigo asilimia 33.

Wateja wa M-Pesa ya Vodacom wameongezeka kutoka milioni 7.6 Juni mwaka jana hadi milioni 8.6 Juni mwaka huu huku wale wa Tigo Pesa wakiongezeka hadi milioni 6.9 kutoka milioni 6.05 mwaka uliopita.

Mkurugenzi wa usimamizi wa benki za biashara na taasisi za fedha wa BoT, Kennedy Nyoni anasema masharti ya mtu kuwa na kitambulisho ili afungue akaunti benki huwekwa na Wizara ya Fedha na Mipango.

Lengo la ulazima huo ulazima huo ni kuzuia utakatishaji wa fedha na kuhakikisha nchi inakua na mifumo imara ya fedha.

“Kwa kutambua umuhimu na unyeti wa sekta hii, kanuni za uthibiti wa fedha haramu zinaitaka benki au taasisi ya fedha kuwatambua wateja wake kabla ya kuanzisha ushiriakiano wa kibiashara, wakati wa kufanya miamala yeyote na kwa wakati wote wa uhusiano wao kupitia vitambulisho,” anasema Nyoni.

Anasema kanuni inabainisha vitambulisho vinavyotambulika ni kadi ya mpigakura, kitambulisho cha Taifa, hati ya kusafiria, cheti cha kuzaliwa au leseni ya udereva.

“Kama mtu hana hivyo vyote basi barua ya Serikali ya Mtaa anaoishi, mwajiri au mkuu wa taasisi anayosoma vinaweza kutumika,” anaongeza.

Mhadhiri mwandamizi na uchumi katika chuo kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi anasema zipo sababu nyingi za watu kutumia simu za mkononi.

“Ukiwa na simu ya mkononi hauhitaji kuonana na mtoa huduma, unaweza kufanya miamala yako ukiwa kazini au nyumbani,” anasema Profesa Ngowi.Advertisement