KUTOKA LONDON : Vitu vidogo vidogo mitaani vinavyokudokeza sura ya Serikali

Muktasari:

  • Hizi zana (kama mitandao jamii) zilivumbuliwa na hawa hawa wachapakazi. Rais Magufuli anachojaribu ni kuelekeza Mtanzania kuwa katika nidhamu kuliko kubangaiza na kubabaisha babaisha.

Nilikuwa nikisubiri gari moshi. Tulikaa juu ya viti vilivyojengewa uzio wa glasi kuzuia kibaridi baridi. Maana ingawa msimu wa joto umeshaanza kuchungulia, Uzunguni, msomaji, bado baridi inatesa, penda usipende. Nyumbani tunalalamika joto, mbu na vumbi. Hapa ni baridi, mtetemo (si “tetema”- ule wimbo wa bwana Diamond na mtunzi Skiza) tu....

Wapo Watanzania wakisikia hivyo huuliza sasa mmekwenda kutafuta nini? Ukweli kuna mazuri sana. La kwanza kitaaluma hapa mtu unathaminiwa na ukiipenda kazi yako unapata faraja. Ndiyo moja ya mambo makuu ya Rais Magufuli na awamu ya tano.

Baadhi ya Watanzania tunalalamika Oh huyu Rais mkali “siku hizi hakuna mtu mwenye hela” – Basi siri ni moja. Anachokifanya Magufuli ndiyo sahihi. Huku Majuu kinachoendekezwa ni kazi, elimu na taaluma. Hakuna hela ya ziada. Kwanini?Ukiwa na fedha hujenga faida fulani. Ndiyo sababu wenzetu huendelea na kila siku wanavumbua mapya kisayansi na kiteknolojia. Sisi kazi yetu kufuata mkumbo tu. Waafrika tunapenda kudandia.

Hizi zana (kama mitandao jamii) zilivumbuliwa na hawa hawa wachapakazi. Rais Magufuli anachojaribu ni kuelekeza Mtanzania kuwa katika nidhamu kuliko kubangaiza na kubabaisha babaisha.

Miaka mbeleni tutapomwelewa vizuri. Kama ambavyo Mwalimu Nyerere alitaniwa mchonga meno, leo tunavuna matunda. Tanzania ina amani kubwa (ukilimganisha na mataifa yaliyoboromoka Afrika). Tufungue macho.

Sasa nilisubiri gari moshi. Kuleee, kushoto: kama mita saba, tisa; walisimama akina mama watatu na kundi la watoto. Wamejifunga vilemba kichwani, kuziba vichwa. Ni Waislamu lakini wa Ulaya Mashariki. Watoto waliobebeshana nao ni wengi. Wawili wadogo sana - ndani ya vigari vya kusukumia (“mapram” kwa kimombo), mmoja analilia kitu.

Mmoja wa wale kina mama kainama kumsaili akae kimya maana kile anachokula kimetosha. Ukiona wanawake wa Kizungu wamebeba kundi kubwa la watoto , huku wamejifunga vichwa, ujue hawa si Wazungu tuliowazoea. Bado wana mila za kizamani (kidesturi). Za wanawake kukaa na watoto, watoto kushikiwa viboko nk.

Lakini pamoja na hayo- mmoja wa wale dogodogo kando, mvulana – huenda miaka saba au nane- aliruka ruka na kuhangaika hangaika. Mama akamwita. Mtoto hasikii. Shida nini? Haya magari moshi ni ya mwendo wa kasi sana.Hutokea watu wakajisahau wakaingia njia zake wakagongwa. Ndiyo tahadhari ya Mama. Mtoto kakataa

Analeta nyodo. Anadiriki hadi kumtolea mama yake ulimi nje. Mwishoni mzazi kafura kampigia kelele kikwao ( si Kiingereza)...mtoto karudi lakini badala ya kukaa chini na wenzake, akaketi juu ya kiti- sehemu ya kujiegesha. Akapayuka kwa nguvu. Kiingereza. WEWE MAMA MPUMBAVU! TENA HUJUI KIINGEREZA.

Unasikia changamoto? Mama akafura. Akijijivuta ambabue mtoto.Mmoja wa wale wanawake wenzake akamvuta mama kando. Labda shangazi au mama mdogo. Akamwendea mtoto. Akamwinamia.

“Unawaona wenzako walivyokaa kimya ...wametulia. Wewe huna aibu?”

Kitu kama hicho. Aliwanyoshea mikono wale wengine waliokaa kimya kwa adabu na heshima.

Mtoto akasemaje? NYINYI MNAJIONYESHA TU. Domo kaya. Kule mbali kulikuwa na vichaka. Nikaangaza macho nikijikumbusha ingekuwa Afrika mmoja wa wale akina mama angevunja fimbo amcharaze yule mtoto. Lakini hairudhusiwi kuchapa watoto nchi hii. Ukimgusa mtoto waweza kujikuta gerezani. Wageni huja na desturi wakazifuta kimya kimya.

Tuendelee na mada wiki ijayo