KALAMU HURU: Wabunge aina ya Lusinde wazipime kauli zao

Anapoingia bungeni mara ya kwanza, mbunge yeyote hula kiapo cha uaminifu kwa mujibu wa ibara ya 68 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika kiapo hicho, mbunge hutamka “...Nitahifadhi, nitailinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria iliyowekwa...”.

Huo ni utaratibu wa kawaida ambao mbunge huupitia. Hakuna uwezekano wa mtu yeyote kuupiga chenga na akaendelea kuwa mbunge.

Katiba yenyewe inayotakiwa kulindwa na kutetewa ina mambo mengi ya msingi. Ingawa kuna mengine yanayokosolewa kwa namna moja au nyingine, lakini kwa kuwa bado yamo, yanapaswa kulindwa kama yalivyo.

Mathalan, Katiba yetu ya mwaka 1977, ibara ya 38 inazungumzia uchaguzi wa rais unaotakiwa kufanyika baada ya kiti cha rais kuwa wazi kwa sababu mbalimbali.

Kwa kuwa si lengo la makala hii kuorodhesha sababu za kiti cha rais kuwa wazi na kupelekea uchaguzi kuitishwa, nitazungumzia sababu moja tu tuliyoizoea, inayotokea baada ya Bunge kuvunjwa kama inavyofafanuliwa na Ibara ya 38 (2) (a).

Ingawa vilevile kuna mazingira mengine yanayoweza kusababisha Bunge kuvunjwa kama vile kukataa bajeti ya serikali, Ibara ya 65 (1) inasema: “Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba hii, maisha ya kila Bunge yatakuwa ni muda wa miaka mitano.

Maisha hayo ya Bunge yanafafanuliwa na kifungu cha pili cha ibara hiyo ya 65 kuwa ni “ule muda wote unaoanzia tarehe ambapo Bunge jipya limeitishwa kukutana kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi mkuu na kuishia tarehe ya kuvunjwa kwa Bunge kwa ajili ya kuwezesha Uchaguzi Mkuu mwingine wa kawaida kufanyika.”

Hivyo, kwa maisha yake ya kawaida, Bunge linadumu kwa miaka mitano, na huo ndio muda wa rais kuwapo madarakani kwa mujibu wa Katiba ambayo wabunge na viongozi wengine wanaapa kuilinda na kuitetea.

Nimelazimika kueleza yote hayo kutokana na kauli ya juzi ya Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 usiusishe uchaguzi wa Rais badala yake aachwe aendelee hadi mwaka 2025.

Pamoja na uhuru wa mawazo alionao Lusinde kama raia na hasa pale anapokuwa bungeni, haipendezi pale anapotumia uhuru wake huo kutoa mawazo yanayokiuka Katiba, labda kama alikuwa na nia ya kutaka Katiba irekebishwe kutimiza nia yake hiyo.

Pamoja na hoja aliyoijenga kuwa kazi aliyoifanya Rais John Magufuli ni kubwa, hakuna mtu wa kumshinda na kuwa fedha za uchaguzi wake zitumike kwa mambo mengine, bado siamini kama hoja hiyo ina nguvu za kushawishi mabadiliko ya Katiba kwa lengo hilo.

Siamini kama wapo watu wengine wanaoweza kukubaliana na hoja ya namna hiyo kutumika kubadili Katiba wakati kuna mambo mengine mengi yanayolalamikiwa katika hiyo na hayajafanyiwa marekebisho.

Ingawa hoja ya Lusinde ni tofauti kidogo na ile iliyowahi kutolewa na mbunge wa Chemba, Juma Nkamia ya kutaka muda wa Rais kukaa madarakani uongezwe hadi miaka saba badala ya mitano ya sasa.

Hoja zote mbili bila kujali malengo ya waliozitoa au wanaoziunga mkono ni za kukemewa na wenyewe kutakiwa kupima kauli zao kwa kuwa zinalenga kukiuka Katiba waliyoapa kuihifadhi, kulinda na kuitetea.