Wadau wakosoa kauli ya Ndalichako makosa vitabuni

Tuesday April 9 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Wadau wa elimu nchini wamemjibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako kuhusu kauli yake kuwa wapo watu ambao kazi yao ni kutafuta makosa vitabuni ili kuikosoa Serikali.

Akizungumza katika uzinduzi wa maktaba mtandao jijini Dar es Salaam mwishoni mwa Machi, Profesa Ndalichako alisema kuna watu wanaotafuta makosa vitabuni kwa lengo la kuichafua Serikali.

Ni kauli iliyoibua mjadala katika mitandao huku wachangiaji wengi wakisema kilichofanyika ni kwa maslahi ya Taifa na sio kumkomoa mtu au Serikali.

Mwananchi limezungumza na baadhi ya wadau wa elimu akiwamo mwalimu mstaafu Bakari Kheri anayesema haoni ubaya kama anatokea Mtanzania anayejipa kazi ya kutafuta makosa ambayo kimsingi yanapaswa kugundulika mapema na wachapishaji kabla ya vitabu kuanza kutumika.

‘’Hiyo kauli niliisoma mitandaoni. Alianza vizuri kwa kuitaka TET (Taasisi ya Elimu Tanzania) isiruhusu makosa kwenye vitabu, lakini mwishoni akaharibu. Hivi anachotaka yeye watu wasitaje udhaifu wa vitabu hata kama wamegundua makosa vitabuni?” alihoji Kheri.

‘’Waziri akumbuke kuwa hao anaodai kazi yao ni kutafuta makosa ndio walioifumbua macho wizara mpaka kipindi kile ikavunjwa bodi inayosimamia ithibati ya vitabu pale wizarani. Kama ni kuichafua Serikali, kwa nini hakupuuzia kauli za kina Mbatia waliogundua makosa kule bungeni, kwa nini wizara yake iliamuru vitabu vyenye makosa virudishwe na watumishi kusimamishwa?’’

Mhadhiri wa masomo ya lugha kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Faraja Kristosmus anasema kama vitabu vina makosa ni muhimu kukosolewa uli kuepusha athari kwa watumiaji.

‘’Vitabu vikikosewa maudhui ni shida kwa wanafunzi na walimu. Mathalani Hisabati ikikosewa kwenye maswali au maelezo ya ukokotoaji, mwanafunzi atashindwa kuelewa na itakuwa vigumu kujua kama amwamini mwalimu au kitabu. Lakini makosa yanayopotosha jambo lazima yaangaliwe. Sasa kama kwenye sayansi kitabu kinatoa maelezo yasiyo sahihi je, jamii iache kukosoa?’’ anasema.

Mratibu wa Mtandao wa Elimu (TenMet) Cathleen Sekwao anasema makosa kwenye vitabu hayatafutwi, bali yanaonekana na wasomaji hivyo ni muhimu kwa waandaaji kuwa makini ili kutengeneza elimu bora kwa jamii kama lilivyo lengo la kutoa vitabu hivyo.

Pamoja na kuamini kuwa Profesa Ndalichako alitoa kauli hiyo ikiwa ni chachu ya kuwataka watendaji wa Taasisi ya Elimu Tanzania kuwa makini katika uandaaji wa vitabu, Mkurugenzi wa asasi ya Furaha Pamoja Foundation, John Paul anasema Taifa makini linaandaliwa na mfumo mzuri wa elimu unaojumuisha vitabu visivyo na makosa.

Kwa hiyo kama kauli kuwa kuna watu kazi yao ni kutafuta makosa ina ukweli, lazima wawepo ili kutengeneza mfumo mzuri wa elimu,” anaeleza.

Kauli ya Profesa Ndalichako imemgsusa pia mchapishaji mkongwe wa vitabu nchini, Abdullah Saiwaad anayesema watu hawavichambui vitabu kwa nia mbaya bali kuisaidia Serikali kuboresha elimu.

“Usipochambua kitabu na kujua kama kuna makosa, watoto wadogo wakisoma wataamini makosa hayo. Kwa mfano, kitabu kikiandika hii ni rangi ya blue wakati ni nyekundu, mtoto ataamini kuwa ni bluu,” alisema na kuongeza kuwa kwa hali hiyo anayelaumiwa ni mwandishi na mchapishaji, sio Serikali.

Alisema watanzania sio watu wa kwanza kufanya hivyo na kwamba jambo hilo lilikuwepo tangu enzi na enzi kwa mataifa yote kwa sababu madhara ya kufanya makosa kwenye vitabu huathiri utoaji wa elimu.

Sakata la makosa vitabuni

Suala la makosa vitabuni limekuwa likiibuliwa mara kwa mara na wadau mbalimbali wakiwamo wabunge.

Kinara wa kuibua makosa haya ni Mbunge wa Vunjo, James Mbatia ambaye tangu akiwa mbunge wa kuteuliwa katika utawala wa awamu ya nne, amekuwa mwiba mkali kwa Serikali kwa kuonyesha udhaifu uliomo katika vitabu vinavyotumika katika shule za msingi na sekondari.

Mwaka 2013 Mbatia aliitaka Serikali kuwachukulia hatua za kisheria wajumbe wa iliyokuwa Kamati ya Ithibati ya Vifaa vya Elimu, (Emac), kwa kuvipitisha na kuruhusu vitabu vyenye makosa kusambazwa.

‘’Hawa ni wahujumu uchumi wa nchi yetu; wanahusika kuididimiza elimu yetu... Inaonyesha wazi kuwa watunzi wa vitabu vile hawakutumia mitalaa,’’ alinukuliwa na gazeti hili Juni sita mwaka huo.

Wizara yachukua hatua

Ni makosa haya ambayo baadhi ya watu waliyabaini vitabuni, ndio yaliyoisukuma wizara ya elimu kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wake.

Kwa mfano, Mei 2, 2018 Waziri Ndalichako akizungumza bungeni alisema wizara yake iliwasimamisha kazi watumishi 22 wa TET kwa kuisababishia Serikali hasara kwa kuchapisha vitabu vyenye makosa.

Awali kelele za wadau wa elimu kuhusu makossa vitabuni ndizo zilizochangia kuvunjwa kwa Emac iliyoanza kufanya kazi tangu mwaka 2005

Advertisement