Wadau wakumbusha umuhimu wa uwazi mikataba ya madini

Muktasari:

  • Sekta ya madini ni miongoni mwa zinazoongoza kwa kuliingiza Taifa fedha za kigeni lakini changamoto kubwa iliyopo ni kwamba mikataba mingi ambayo Serikali imesainiana na wawekezaji wakubwa waliopo nchini haipo wazi. Wadau wameikumbusha Serikali juu ya umuhimu wa kuiweka wazi ili wananchi wajue namna watakavyonufaika na uvunaji wa rasilimali hizo za asili.

Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zenye hazina ya madini ya aina tofauti ambayo wananchi wake hawaelewi makubaliano yaliyomo kwenye mikataba ya uwekezaji uliofanywa.

Hayo yanaendelea licha ya kuwapo kwa Sheria ya uwazi katika sekta ya madini, mafuta na gesi ya mwaka 2015 (Tanzania’s Extractive Industries; Transparency and Accountability Act, 2015).

Hivi karibuni, Serikali imechukua hatua za kuimarisha usimamizi kuhakikisha rasilimali za Taifa zinawanufaisha zaidi Watanzania lakini hakuna mkataba uliowekwa wazi ili wajue namna masilahi yao yanavyolindwa.

Mwaka jana, Bunge lilifanya marekesho ya sheria tatu zinazosimamia rasilimali za Taifa yakiwamo madini, mafuta na gesi, maliasili kama vile wanyama, miti na viumbehai vingine.

Sheria hizo zilipendekeza mambo kadhaa ikiwamo Serikali kumiliki walau asilimia 16 kwenye kila kampuni itakayokuja kuwekeza kwenye madini, ujenzi wa mitambo ya uchenjuaji nchini pamoja na kuanzisha minada ya madini nchini.

Kwa hatua zaidi, Serikali ilijenga uzio kuzunguka ilipo migodi ya madini ya Tanzanite uliozinduliwa mapema Aprili.

Msemaji mkuu wa Serikali, Dk Abbas Hassan anasema makusanyo ya mapato yameongezeka kwa kiasi kikubwa. “Tumevuka malengo ya ukusanyaji wa mapato kwenye sekta ya madini kutoka Sh154 bilioni hadi Sh301.6 bilioni,” anasema Dk Hassan.

Ingawa makusanyo yanaongezeka kama anavyobainisha Dk Hassan lakini hoja ya wengi ni uwazi katika mikataba iliyopo kuona namna unavyogusa maisha ya wananchi wanaozunguka mahali zilipo rasilimali husika na Taifa kwa ujumla.

Uchimbaji wa madini ya almasi kwa mfano, umeanza miaka mingi hata kabla ya uhuru. Historia inaonyesha mgodi huo ulianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1940. Mwishoni mwa miaka ya 1990, uchimbaji wa dhahabu ulianza pia nchini.

Tangu mwaka 2010, Tanzania iligundua futi trilioni 57.5 za gesi asilia ambayo ni muhimu kwa uzalishaji wa umeme na kutoa malighafi za viwanda vya dawa za binadamu na mbolea. Pamoja na utajiri huo, Watanzania wengi wanaishi katika umasikini.

Takwimu zinaonyesha Watanzania milioni 12 wanaishi chini ya Dola moja ya Kimarekani (zaidi ya Sh2,250) kwa siku. Ufukara unaongezeka licha ya uchumi kukua kwa wastani wa asilimia 7.0 au zaidi ya hapo kwa miaka mitano iliyopita.

Wadau

Kwa kutambua hali hiyo ya wananchi na umuhimu wa madini pamoja na rasilimali nyingine ambazo uvunaji wake una kikomo, asasi za kiraia zinapendekeza Serikali kuhakikisha kunakuwa na uwazi katika sekta za madini, mafuta na gesi.

Meneja kampeni wa Shirika la Oxfam Tanzania, Jovita Mlay anasema rasilimali zilizopo ni za wananchi ingawa zinasimamiwa na Serikali, kwa hiyo mambo ambayo Serikali inayasimamia yanatakiwa yawekwe wazi kwa umma ili waelewe namna makubaliano yanavyofanywa na jinsi watakavyonufaika.

“Hii inaongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao na inaondoa shaka. Pia, iwapo Serikali itaweka wazi baadhi ya makubaliano inayofanya itaisaidia kujenga imani ya wawekezaji pia,” anasema.

Japokuwa Serikali imekuwa ikitekeleza mipango ya kuboresha sekta ya madini, mafuta na gesi, anasema Taifa linatakiwa lione linavyonufaika na mikataba iliyosainiwa hivyo kuitaka Wizara ya Nishati kuipitia mikataba iliyopo ili kuhakikisha wananchi wananufaika kwa kupata mgawo unaostahili.

“Ni wakati sahihi mikataba iwekwe wazi kwa umma ili wananchi waelewe namna wanavyoweza kusaidia kuiboresha. Kuna wataalamu, asasi za kiraia na watu binafsi ambao wanaweza kuitafsiri kwa manufaa ya umma na kusaidia kushauri namna ya kwenda mbele katika masuala yanayohusu rasilimali zao,” anasema Jovita.

Mkurugenzi mwenza wa Taasisi ya Usimamizi wa Maliasili (NRGI) Afrika, Silas Olan’g anasema uwazi wa mikataba ni suala muhimu kwa Serikali inayowajibika kulinda maliasili na rasilimali zake kuhakikisha inakuza uchumi kutokana na matumizi yake.

Iwapo Serikali na wawekezaji watafanya makubaliano yanayohusu umiliki wa rasilimali za umma wananchi wana haki ya kujua vigezo vilivyotumika ikiwamo masuala ya leseni, mikataba, utaratibu wa usimamizi na sheria zilizotumika.

“Bila uwazi katika mikataba, kunakuwa na migogoro inayotokana na hofu na kunaibuka migogoro inayotokana na kutoaminiana miongoni mwa wadau. Si demokrasia mikataba kuwa ya kificho. Mikataba inaongozwa na sheria zinazosimamia miradi ya umma, suala la msingi ni kuheshimu sheria zinazoelekeza iwe hadharani,” anasema Olan’g.

Mkurugenzi wa Shirika la Hakirasilimali Tanzania, Rachael Chagonja anasema Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanznaia inasema rasilimai za Tanzania zinatakiwa ziwanufaishe raia wake ambao ndio wamiliki.

Wakiwa wamiliki wa rasilimali hizo, wanatakiwa washirikishwe katika mipango yote ya uendelezaji kuanzia uingiaji mikataba hata matumizi ya mapato.

“Kwa muda mrefu sasa, uwazi wa mikataba umeendelea kuwa mgumu, ni suala la kificho zaidi. Kutokuwepo namna ya kufikiwa kwa mikataba hiyo kunaweka uzio kwa wananchi kupata taarifa na kufifisha uwajibikaji kwa wamiliki hao wa rasilimali. Pia, kunapunguza uwezo wao wa kujoji na kuzitetea,” anasema Racheal.

Msingi wa asasi za kiraia kutoridhishwa na namna miradi mingi inavyoendeshwa kinyume na sheria ya uwazi na uwajibikaji ni raia kutopewa nafasi ya kujua kilichopo kwenye mikataba kutokana na mikataba hivyo kutonufaika kama invyopaswa kuwa.

Jamii nyingi zinazoishi kuzunguka migodi, miradi ya gesia asilia au mafuta hazijui lolote kuhusu miradi hiyo na hawanufaiki nayo hivyo kuona haja ya mabadiliko ya utekelezaji wa sheria zilizopo.

Serikali

Mapema Septemba, katibu mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk Hamis Mwinyimvua alisema mikataba ya mafuta na gesi inapitiwa na wizara yake ingawa mingi ina vipengele vinavyosisitiza usiri ambavyo vinaweza kuhuishwa iwapo mikataba hiyo itarejewa upya.

Kufanikisha urejewaji wa mikataba hiyo, katibu mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila anasema Serikali inaandaa kanuni za kusimamia uwazi wa sekta ya madini.

“Kwa kweli tutawasiliana na wadau wakiwemo asasi za kiraia kuunda kanuni za kusimamia uwekezaji kwenye sekta ya madini nchini. Hakuna atakayeachwa,” anasema Profesa Msanjila.

Kaimu mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Utafiti wa Mafuta (Pura), Charles Sangweni anasema si taarifa zote zinatakiwa kuwekwa wazi kwa umma kwani baadhi huwa za siri kwa manufaa ya Serikali.

“Suala muhimu hapa ni kuhakikisha mikataba yote inalinufaisha Taifa kwa kuzingatia vigezo kwa kufanya makubaliano ya mikataba mizuri na wawekezaji,” anasema Sangweni.

Kaimu mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli, Kapuulya Musomba anasema sheria ya uwazi na uwajibikaji inahitaji majadiliano kabla mikataba na leseni zote hazijawekwa wazi kwa umma.

Kupitia mikataba

Kaimu katibu mtendaji wa taasisi ya uhamasishaji uwazi katika rasilimali (Teiti), Mariam Mgaya anasema kwa sasa inashirikiana na mamlaka za Serikali kutunga kanuni zitakazoongeza uwazi katika sekta ya madini na gesi asilia.

Anasema utaratibu wa kimataifa unatoa fursa ya mapitio ya sera na kubainisha wajibu kwa kampuni 40 kubwa katika masuala ya mafuta, gesi na madini. Mapitio hayo yaliyosimamiwa na Oxfam Amerika yalikamilika Mei.

“Pamoja na mambo mengine, mapitio hayo yanaonyesha kampuni 18 kati ya zilizopitiwa zimeunga mkono suala la uwazi katika mikataba,” anasema Mariam.