Waeleza walivyobadili maisha kwa kufuga ‘saso’

Sifa mojawapo ya mfugaji makini ni uwezo wa kuchagua aina ya kuku wa kufuga.

Kuna aina nyingi ya kuku wanaotofautiana kwa sifa mbalimbali, lakini katika miaka ya karibuni, macho ya wafugaji wengi yameangukia katika kuku aina ya Saso.

Ana sifa za kipekee ikiwamo kuwa na uzito unaofikia kilo tano anapokuwa na umri wa wiki 70 na kutunzwa vizuri. Lakini pia wana sifa ya kukua haraka na muonekano wa kupendeza.

Wakazi wawachangamkia

Ni kwa sababu hiyo, haikuwa jambo la ajabu kuona baadhi ya wananchi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, wakiamua kufanya ufugaji wa kuku hawa.

Mary Sagamilwa hivi sasa ana kila sababu ya kufurahia matunda ya ufugaji wa saso. Ni kuku waliomwezesha kusomesha mtoto wake elimu ya chuo kikuu ngazi ya shahada ya uzamili na sasa anajipanga asome shahada ya uzamifu.

Mary anayeishi Mbinga mkoani Ruvuma, anaishukuru kampuni ya Sliverland kwa kupeleka mradi huo wilayani Mbinga kwani umesaidia kuwainua watu wengi , hususani wanyonge ambao awali walikata tamaa ya maisha.

Anasema alianza kwa kupokea vifaranga 1000 ambapo alivitunza na baada ya kufikisha siku 30 alianza kuuza kwa wafugaji wadogo waliompatia kipato kikubwa, huku akijipanga kufuga kuku zaidi ya 10,000 kwa mwaka.

’Nimeshafuga kuku wa kila aina kwa muda wa miaka 10 lakini niliambulia maumivu kutokana na kufuga kienyeji tena kwa mazoea hadi binti yangu alipopata mafunzo ndipo mambo yamebadilika. Kwa sasa tunafuga kuku hadi 8000 na vifo vimepungua. Utakuta katika kuku 1000 wamekufa kuku watatu au sita tu , tunaishukuru sana mafunzo ya kampuni hii,’’anasema.

Anasema Saso wana soko la uhakika tofauti wa nyama aina ya ‘broiler’ na kuwa wanapendwa na watu wengi kutokana na kuwa na tabia kama kuku wa kienyeji na wanafugwa pia kama kuku wa kienyeji. Ni kwa kupitia kuku hao anasema sio tu amefanikiwa kumsomesha binti yake lakini pia kuendesha maisha yake, kupanua mabanda na miradi mingine ya maendeleo.

Mfugaji mwingine Matrida Mhelela anayeishi mkoani Iringa anasema kuwa hajutii kuingia kwenye ufugaji na kufuga aina hiyo ya kuku, kwa kuwa umemsaidia kujenga nyumba, kusomesha watoto wake vyuoni pamoja na kuanzisha biashara ndogo ndogo .

Lusekelo Mwasota wa mkoani Mbeya, ni mfugaji mwingine wa kuku hao aliyepata mafunzo ya ufugaji wa kisasa kutoka chuo cha ufugaji kuku cha Makota kilichopo mkoani Iringa.

Anasema, Saso wamebadili maisha yake, awali maisha yake yalikuwa magumu, alishindwa hata kula mlo mmoja lakini kwa sasa mambo yamebadilika, kwa kuwa mbali na kuuza kuku na mayai pia anapata kitoweo mayai na kuboresha lishe. Pia anauza mbolea inayotokana na kuku hao.

Lusekelo anasema, awali alikuwa akijishugulisha na vibarua vya upasuaji mbao, lakini hakuna faida aliyopata hadi alipofanikiwa kupata mafunzo na kuanza kujishugulisha na ufugaji kuku ambapo alikopeshwa kuku na kupewa chakula na kampuni ya Silverlands. Hapo ndipo maisha yake yalipoanza kubadilika na kuwa mazuri.

“Kwa kweli, Silverlands imenitoa kwenye mateso makali, nililala mahali pabaya, niliishi mbali na jamii. Nawashukuru sana sikutegemea kufika hapa nilipo sasa najipanga kuongeza kuku hadi kufikia 9000 kwani nimeona manufaa,’’ anasema.

Sifa za kuku saso

Kuku huyu ana sifa nyingi za kipekee, kutokana na ufugaji wake kuwa rahisi. Kwa mujibu wa Matilda, Saso ana uwezo wa kutaga mayai 240 kwa mwaka ikilinganishwa na kuku wa kienyeji ambaye anataga mayai 50 tu kwa mwaka.

Aidha, Saso anakua kwa haraka na kufugwa kienyeji kwa kuachiwa nje na kurudishwa ndani ambapo kwa umri wa siku 70 anakuwa na uzito wa kilo mbili na nusu hadi tano. Wanaanza kutaga wakiwa na wiki 18 tofauti na wa kienyeji ambao Huanza kutaga wiki ya 32 wakiwa na uzito wa kilo pungufu ya mbili.

Ni kuku asiye na gharama kumtunza, huku wakiwa na tabia kama ya kuku wa kienyeji.

Mradi wa kuku walioboreshwa

Meneja mradi wa usambazaji wa kuku walioboreshwa (APMI )Tanzania Mwanavua Ngocho, anasema lengo la mradi huo ni kusambaza kuku walioboreshwa ili watu wapate tija, kuboresha kipato, lishe na pia watambue kuwa ufugaji ni sawa na biashara.

Anasema kuwa mradi ulilenga kinamama walio kwenye kaya zisizojiweza ili waweze kujikwamua kimaisha.

‘’Hadi sasa zaidi ya wafugaji 400 wamefikiwa katika vijiji vya mikoa 16 ambapo kuna jumla ya vitengo 430. Wafugaji walio kwenye mradi huu wanakopeshwa vifaranga na kupewa chakula. Kwa mfano, akichukua vifaranga 100 anapewa na tani moja ya chakula bure. Pia vifaranga vyake vinapatiwa chanjo zote tatu,’’ anasema na kuongeza:

‘’ Sliverland imejipanga kuhakikisha inaendelea kutoa mafunzo bora ya ufugaji wa kuku kisasa, mikopo ya kuku, pamoja na chakula kwa watu wengi zaidi.’’

Mkuu wa chuo cha ufugaji wa kuku, Sheryl Bradnick anasema chuo hicho kilianzishwa rasmi machi 2016 na tayari watu 1200 wamenufaika na mafunzo huku wakipata mafanikio makubwa.

Anasema, chuo hicho kimekuwa msaada si kwa Watanzania pekee bali hata nchi jirani za Kenya, Uganda, Malawi na Msumbiji.

Wasiliana na mtaalamu wa ufugaji kwa namba 0757900800