Wakulima katikati ya sintofahamu ya matumizi ya ‘Round up’

Muktasari:

  • Ni dawa maarufu ya kuulia magugu shambani

Ni kama vile baadhi ya wakulima nchini hawajui kinachoendelea kuhusu dawa ya kuua magugu iitwayo Round up, ambayo mahakama moja nchini Marekani imeiamuru kampuni ya Monsanto inayotengeneza dawa ya hiyo kumlipa fidia mtumiaji aliyedhurika nayo.

Hukumu hiyo imetolewa baada ya mahakama kujiridhisha kuwa mlalamikaji anayeitwa Edwin Hardeman ameathirika kwa kupata saratani kutokana na matumizi ya dawa hiyo.

Mahakama ilijiridhisha kuwa kemikali ya ‘glyphosate’ iliyomo kwenye dawa hiyo husababisha saratani ya matezi aliyougua Hardeman na hivyo kuiamuru kampuni hiyo kumlipa Dola za Marekani 114 milioni (zaidi ya Sh257 bilioni).

Uchunguzi wa Mwananchi katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam ambalo ni eneo lenye maduka mengi ya pembejeo za kilimo, umebaini kuwa dawa hiyo inaendelea kuuzwa tena kwa wingi, huku wauzaji wengi wakiwa hawajui kama inasadikiwa kuwa na madhara.

Katika baadhi ya maduka, dawa hiyo inauzwa kwa Sh 13,000 mengine Sh16,000 huku mengine yakiuza kwa bei ya Sh17,000 na mwandishi wetu alipouliza kuhusu kuwapo kwa tofauti za bei hiyo, wauzaji walieleza kuwa kuna dawa halisi na feki.

Salama Juma ambaye ni mmoja wa wauzaji pembejeo eneo hilo alisema hajui kama ina madhara ila anachokifahamu ni kwamba upatikanaji wa dawa hiyo kwa sasa umekuwa mgumu kwa sababu aliyekuwa msambazaji wa dawa hiyo nchini kuvunja mkataba na kampuni inayotengeneza dawa hiyo na kuanza kuzalisha dawa yake . Dawa hiyo alisema inaitwa Super round.

Muuzaji mwingine Hadija Mohamed alisema japo hajui kama imepigwa marufuku, lakini anakiri kuwa dawa hiyo inaweza kuwa na madhara.

“Kila kemikali ina madhara kwa binadamu kama ikitumiwa vibaya bila kufuata utaratibu. Hivyo hata hii huenda ikawa na madhara kwa sababu ni sumu, na utaratibu ni kwamba mtu akinunua hii dawa anapotaka kuitumia sharti avae vifaa vya kiusalama,’’ alisema.

Inatumikaje?

Jina Round up ni maarufu kwa wakulima hasa wanaotumia viutalifu kuua magugu shambani. Ni vigumu kuwakuta wakulima wa aina hiyo Tanzania wanaosumbuliwa na magugu, lakini wasiwe wamewahi kutumia dawa hiyo.

Ndiyo maana Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu nchini (TPRI) Dk Margaret Mollel anasema matumzi ya kiuatilifu hicho ni makubwa na kinatumika kwa wingi kiasi cha kuvuka asilimia 50 ya matumizi yote vya viuatilifu vya magugu kwenye mazao nchini.

Justine Mvungi ni mkulima katika kijiji cha Kikavuchini mkoani Kilimanjaro. Anasema amekuwa akitumia dawa ya Round up kukausha magugu shambani.

“Hiyo dawa ninaifahamu na huwa ninaitumia kukausha magugu shambani. Dawa hii inatumika kwa njia ya kunyunyiza baada ya kuchangaywa na maji. Inafanya kazi ndani ya siku nne baada ya kupuliza majani ambayo huanza kubadilika rangi na kuwa ya njano na baada ya mwezi mmoja majani hukauka na shamba linakuwa jeupe”anasema na kuongeza:

“Naweza kusema ina madhara kwa sababu dawa hii ukiipuliza shambani wakati kuna jua kali, mara nyingi unajisikia kulewa na kizunguzungu na ina harufu kali.’’

Mvungi anasema wakulima wengi wanatumia dawa za shambani bila kuwa na vifaa vya kiusalama, hivyo kuna uwezekano wa watu wengi kuwa wameathirika kutokana na madawa mbalimbali wanayotumia.

Round up inatambuliwa na Wizara ya kilimo

Uchunguzi mwa Mwananchi umebaini kuwa round up ni moja kati ya viutilifu ambavyo hata Serikali inaitambua matumizi yake hasa katika kupambana na magugu yanayoathiri zao la mpunga.

Kwa mfano, mwongozo kwa maofisa ugani kuhusu uzalishaji bora wa kilimo cha mpunga wa mabondeni uliotolewa na Wizara ya Kilimo na Chakula, unampa mkulima mbinu za kudhibiti punga pori kwa kunyunyuzia dawa ya ‘Roundup’ wiki mbili baada ya magugu kuota.

‘’Dawa hii inaweza kunyunyiziwa kwa kutumia bumu lililofungwa kwenye trekta na mchanganyiko wake unapatikana kwenye maelezo ya dawa pindi uinunuapo, unasema mwongozo huo uliotayarishwa na Kituo cha utafiti wa kilimo KATRIN, Ifakara kwa ushirikiano na taasisi ya Natural Resource International ya Uingereza.

Mwongozo huo unaongeza kuwa atakayetumia dawa hiyo ahakikishe kina jina halisi la kiua gugu ambalo ni ‘glyphosate’ . Glyphosate ndio kemikali ambayo mahakama nchini Marekani ilisema kuwa ndio iliyomsababishia Edwin Hardeman kupata saratani ya matezi.

‘’Kwa Round up, inaagizwa kutumia 1.4 kg a.i/ha sawa na gramu 1400 za glyphosate kwa hekta. Kwa kuwa Round Up ina gramu 360 za glyphosate inabidi kukokotoa kiasi cha dawa ya kutosha kwa hekta moja,’’ unaongeza kusema mwongozo huo uliotolewa Novemba 2005.

Kauli ya TPRI

Kwa mujibu wa TPRI tangu kiutilifu hicho kiliposajiliwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, hakuna taarifa za kiutafiti zilizowasilishwa kwa taasisi hiyo zikionyesha madhara kwa binadamu.

Mtafiti Mwandamzi wa mimea wa TPRI anasema ipo mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeweka saini ukiwamo wa Stockholm unaohusu viuatilifu ng’ang’anizi

“Miaka mitatu iliyopita kuna viuatilifu vilivyogundulika kwamba ni ving’ang’anizi, taarifa za kisayansi za kimataifa zilithibitisha hivyo na sisi kupitia vikao vya kitaifa vya kusajili viuatilifu tulipitia mlolongo wa kisheria kuvifuta. Hii inadhihirisha kwamba nchi yetu inakidhi viwango vya kimataifa kufuta viuatilifu vyenye kuleta hatari, ”alisema Mkaranga pasipo kutaja round up kama moja ya viuatilifu vilivyofutwa kwa sababu ya kuwa hatari kwa watumiaji wake.