Wakulima wa mazao mkakati sasa kucheka

Muktasari:

  • Ile hofu ya kukosa masoko sasa inaelekea kuyeyuka baada ya mfumo mpya wa soko la bidhaa kurahisisha upatikanaji wa masoko.

Wakulima wa mazao mkakati pamoja na mazao mengine ya nafaka wana kila sababu ya kuongeza uzalishaji wa mazao yao.

Ile hofu ya kukosa masoko sasa inaelekea kuyeyuka baada ya mfumo mpya wa soko la bidhaa kurahisisha upatikanaji wa masoko.

Mfumo huu mpya ambao utaanza na mazao mkakati (pamba, chai, kahawa, korosho na ufuta) pamoja na mazao mengine yanayohifadhiwa kwenye maghala yanayosimamiwa na Bodi ya Mamlaka ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), utarajiwa kuanza muda si mrefu kutoka sasa. WRRB kwa kushirikiana na Soko la bidhaa Tanzania (TMX) ndio watakaosimamia mfumo huu.

Mkurugenzi Mkuu wa TMX Godfrey Malekano, mfumo huu umekuja kuwasogezea wakulima soko la bidhaa zao karibu, kuongeza uwazi na kupunguza gharama za usafirishaji na usimamizi.

”Tutaanza na minada ya kawaida na kwa sababu mfumo huu utategemea zaidi mfumo wa Tehama tutapata wateja mpaka nje ya nchi” alisema Malekano na kuongeza kuwa kwa kushirikiana na balazi za Tanzania zilizopo nje ya nchi, wanatarajia kupata wateja wengi.

Alisema mfumo wa Tehama utawaunganisha moja kwa moja wakulima, Wanunuzi na wasimamizi.

Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB Augustino Mbulumi, alisema kazi yao kubwa kwa kushirikiana na vyama vya ushirika itakuwa ni kukusanya mazao pamoja na kuyaweka kwenye maghala, huku pia akiwataka wakulima kuondoa hofu pale wanapokuwa wamevuna kwa wingi.

“Sisi tutakusanya mazao, lakini pia niwaombe wakulima waondoe hofu pale wanapovuna kwa wingi kwamba mazao yao hayatopata soko. WRRB tunawaahidi tutapokea mazao yao na kwa kushirikiana na wenzetu wa TMX tunaamini tutapata masoko,” anaeleza.

Kwa kuzingatia ubora wa mazao, WRRB wanajipanga kutumia magunia imara ambayo si rahisi kwa wadudu kupita lakini pia kutumia maghala imara aina ya ‘silos.

Jinsi mfumo unavyofanya kazi

Wakulima watatakiwa kuhifadhi mazao yao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani (WRS) na kisha watapewa risiti. Kuweka mazao ghalani kutajumuisha ukaguzi wa mazao na kuyapangilia kulingana na ubora.

Ili kupunguza gharama za kuhifadhi gharani na muda, WRRB wanafanya kazi na vyama vya ushirika katika kila mkoa wilaya na mpaka vijijini. Kazi kubwa ya vyama hivyo ni kukusanya mazao kutoka kwa wakulima, kuyahakiki na kuyapanga kwa ubora kabla hayajapelekwa kwenye maghala yaliyosajiliwa.

Mkulima sasa atakua akisubiri mazao yake kuuzwa. TMX kwa kushirikiana na wadau wake ambao wapo nchini katika kila mikoa pamoja na wale waliopo nje ya nchi watakua wakitafuta wateja wa bidhaa hizo.

Baada ya biashara kukamilika, ili kuepusha upoteaji wa fedha na matapeli, TMX wataweka fedha za wakulima moja kwa moja kwenye akauti zao za benki siku moja baada ya biashara kukamilika.

Wakulima wasiwe na hofu

Mrajisi mkuu wa vyama vya ushirika nchini (TCDC) Tito Haule aliwaahidi wakulima kuwa mfumo huu utawasaidia kupata kile wanachostahili.

Anawahakikishia pia kwa kutumia mfumo wa Tehama, watakuwa wakifuatilia mwenendo mzima wa bidhaa zao mpaka pale zitakapouzwa.

Alisema licha ya kuwa na kazi ya kukusanya mazao pia wanawaelimisha wakulima juu ya umuhimu wa mfumo wa stakabadhi ghalani, kwa kuwaelekeza kwenye semina zao na kuwaonesha namna wenzao wa sehemu nyingine walivyonufaika na mfumu huo.

“Wakulima wa korosho kiatika mikoa ya kusini walianza kunufaika na mfumo huu tangu mwaka jana na mwaka huu pia wakulima wa ufuta wameanza kunufaika na mfumo huu mwaka huu” alisema akitolea mfano wakulima wa ufuta wilayani Kibiti walivyo nufaika baada ya kuuza zao hilo kwa bei ya mpaka Sh3,100 kwa kilo ukilinganisha na Sh1,200 au chini zaidi katika misimu iliyopita.

Faida ya mfumo

Kwa muda wote ambao mzigo wa mkulima utakua umehifadhiwa, gharama za uhifadhi ni zilezile, na kwa kuitumia stakabadhi aliyonayo, mkulima anaweza kukopa katika benki akitumia stakabadhi hiyo kama dhamana na kupata mpaka asilimia 60 ya mkopo kulingana na thamani ya mzigo wake.

Mbulumi aliongeza kuwa mfumo huu utamsaidia mkulima kuongeza tija katika uzalishaji na kupunguza gharama za miamala ambazo mkulima alikua anapata kabla.

Kwa upande wake Malekano, anawaasa wakulima kuelekeza juhudi zao kwenye uzalishaji ili waweze kupata mazao yenye ubora ambayo yatauzwa kwa bei nzuri.

“Wakulima sasa hawatakiwi kuwaza upatikanaji wa masoko kwani hiyo itakuwa ni kazi yetu kwa kushirikiana na wadau wetu ndani na nje ya nchi. Wanachotakiwa ni kuzalisha bidhaa bora kwa kiwango kikubwa ili tunapoipeleka bidhaa hiyo sokoni iweze kuuzika kwa bei nzuri” anasema.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa kwa kuwa TMX itachukua jukumu la kutafuta masoko, ni wakati mwafaka kwa bodi za mazao nchi nzima kufanya kazi kwa karibu na wakulima, kwa kuwapa elimu ya matumizi ya pembejeo bora za kilimo ambazo zitasaidia upatikanaji wa mazao mengi na bora.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Uratibu na Sera) Faustine Kamuzola alisema soko la bidhaa limekuja kuongeza tija kwa wakulima ikiwemo kuongeza kipato na ajira.

Alisema kutokana na mfumo huu, mnyororo wa thamani kati ya mkulima mpaka mnunuaji utakuwa umeimarika na kwamba hakutakuwa na uvujaji katika mnyororo mzima wa thamani, hivyo kuhakikisha kila mshiriki anapata kile anachostahili.

”Kuwaongezea imani wakulima, taasisi za kifedha zitakazohusika katika mfumo mzima zinatakiwa kuwaunganisha wakulima moja kwa moja na simu zao na kuwapa taarifa zote za miamala ya kifedha inayoendelea,” alisisitiza.