Walia uhaba wa maji shuleni

Mwenyekiti wa bodi ya shule ya Sekondari ya Ukwiva wilayani Kilosa Rubanga Mapesi amesema ukosefu wa maji safi na salama kwenye shule hiyo ni kati ya sababu za kushuka kwa kiwango cha elimu shuleni hapo.

Alisema wanafunzi hulazimika kubeba maji kwenye vidumu vya lita tano toka nyumbani kwao kila siku, kwa ajili ya matumizi shuleni jambo ambalo ni hatari kwa afya na linaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko.

Akizungumza na Mwananchi, Rubanga alisema yapo matenki ya maji mawili yaliyojengwa shuleni hapo, lakini hayajaanza kusaidia kwa sababu yanategemea mvua ili yajae maji.

“Haya matenki yalijengwa kupitia miradi ambayo hata sisi hatukushirikishwa, kama tungeulizwa tungeomba vichimbwe visima kumaliza kero ya maji,… matenki yanayotegemea mvua hayawezi kutusaidia kwa sasa,” alisema Rubanga.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Mariam Majaliwa alisema kero ya maji ni kati ya changamoto zinazowakabili shuleni hapo.

“Hali ni mbaya zaidi kwa watoto wa kike hasa wanapokuwa kwenye siku zao, kama hakuna maji mtoto inabidi asije shuleni au hata akija anawahi kuondoka na kukosa masomo,” alisema.

Aliongeza: ‘‘Hata nyumba za walimu hazijakamilika ujenzi wake, halafu eneo hili lina upupu mwingi, unaingia mpaka ndani kiukweli hatuna raha.”

Baadhi ya wanafunzi wa kike walisema wengi wao huwa hawahudhurii masomo siku za hedhi kwa sababu ya uhaba wa maji shuleni.

“Kati ya siku nne ninazo tumia kwenye siku zangu, siku tatu huwa nashindwa kuja kabisa shuleni, hata nikibeba nidumu cha maji bado huwa hakiwezi kukidhi mahitaji yangu yote, tunaomba tuchimbiwe visima,” alisema.

Ofisa Elimu Taaluma wa Wilaya ya Kilosa , Paula Nkane alisema changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya elimu wilayani humo zinashughulikiwa ikiwamo ya maji.

“Hilo la kutowashirikisha itabidi niwasiliane na wahusika, lakini kero nyingi za elimu ila kwa kawaida huduma za jamii shuleni huwa zinawashirikisha wananchi,” alisema.