Waliojiuzulu ubunge, wapita bila kupingwa

Sunday November 4 2018

 

By Waandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Manyara/Mwanza. Waliokuwa wabunge kupitia Chadema ambao walijizulu na kuhamia CCM, wametetea nafasi zao baada ya kupita bila kupingwa.

Wabunge hao wateule ambao wametetea nafasi zao katika majimbo yaleyale ni James Ole Millya (Simanjiro), Pauline Gekul (Babati Mjini) na Joseph Mkundi wa Ukerewe.

Jana saa 10 jioni ilikuwa siku ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa kugombea ubunge katika uchaguzi mdogo uliopangwa kufanyika Desemba 2 na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Msimamizi wa uchaguzi wa Simanjiro, Yefred Myenzi alisema hadi muda huo unafika aliyekuwa amerejesha fomu alikuwa Millya, hivyo alimtangaza kupita bila kupingwa.

Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Babati Mjini, Fortunatus Fwema alisema Gekul alipita bila kupingwa baada ya kukosa mpinzani.

Alisema mwanachama wa NRA, Feruzi Juma alichukua fomu, lakini hakuirudisha na mwanachama wa CUF, Abubakari Peter fomu yake haikukidhi vigezo.

Naye msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Ukerewe, Ester Chagurani alimtangaza Mkundi kuwa mbunge mteule baada ya waliochukua fomu kutozirejesha.

Kwa upande wa Jimbo la Serengeti, Msimamizi wa uchaguzi, Juma Hamsini alisema licha ya waliorejesha fomu kuwa wanne, lakini mgombea wa CCM, Marwa Chacha huenda akapita bila kupingwa kutokana na dosari za wagombea wengine

“Ninakagua vituo vya uchaguzi, nitatoa taarifa Jumatatu (kesho), lakini kwa kifupi wagombea wengine wa CUF, UDP na NRA fomu zao zina dosari kubwa,” alisema.

Imeandikwa na Joseph Lyimo (Manyara), Anthony Mayunga (Serengeti) na Joviter Kaijage

Advertisement