Wana-CCM wanawapenda kwa dhati waumini wapya?

Sunday November 4 2018

 

By Idd Amiri

Chama cha Mapinduzi kinaonekana kupendwa na walewale waliokuwa wapinzani wakubwa katika siku za karibuni na wanachama wake kindakindaki kabisa wanaonyesha kufurahishwa na mapenzi yanayotokea upande wa pili.

Wanachama wenye nyadhifa kutoka kambi ya upinzani wanaondoka na wako tayari kabisa kuachia nyadhifa hizo kubwa kama za uwakilishi wa wananchi kwa ngazi ya ubunge na udiwani na mtaa.

Kila anayeondoka anasema kuwa CCM ya leo siyo ile ya jana utafikiri kuwa sera, itikadi na mwelekeo wake umebadilika, wengi wa wanaoingia huko kwa sasa wanaonekana kumfuata mtu mmoja tu, naye ni Rais na Mwenyekiti wa chama hicho John Magufuri kwa sababu anaonekana kuwa ndiyo CCM mpya na sijui kama akimaliza muda wake wataondoka naye? Jibu hatuna kwa sasa.

Malalamiko ya upinzani

Upande wa upinzani unalalamika kuwa siyo kweli kuwa watu wao wana mapenzi mema na CCM na mwenyekiti wake, lakini kuna madai ya fedha kutumika kuwanunua wanasiasa hawa, vilevile kuna wanaodai viongozi wa juu wa upinzani ni tatizo katika uendeshaji wa shughuli za kisiasa na kama vile kuna umangimeza fulani huko na wakienda CCM watapata kile wanachokihitaji.

Jibu jepesi ni kuwa wanasiasa wetu hawana kile wanachoamini kama watu binafsi katika kuwatetea na kuwaletea maendeleo watu wao. Kwa mfano, hakuna mwanasiasa anayeamini kuwa unyanyasaji wa watoto, mauaji ya albino na rushwa visipopiganiwa kwa kiasi fulani katika chama chake atajiondoa.

Tunao wanasiasa wanaofuata mlo, kama chama A hakina pilau ya biriani basi ataifuata chama B ilipo na wala hakuna kitu kinaitwa kuvutiwa na utendaji wa awamu ya tano kwa sababu hii itaondoka na ikija nyingine ikawa haina kasi kama hii utakuwa mwisho wa kufanya siasa, hapana.

Katika nchi ambayo ina matatizo chungu mbovu kama ya umasikini, magonjwa, ujinga na mengine isingekuwa na wanasiasa ambao wanapenda kupoteza mabilioni ya fedha katika chaguzi za marudio kwa visingizio visivyo na mashiko.

Yapo mengi ya kujiuliza miongoni mwao ni kweli wana-CCM kwa moyo wa dhati kabisa wanawakubali waumini hawa wapya wa rangi ya kijani? Au kuna kitu wameambizana kuwa kwa sasa kinaweza kuwa hakina manufaa, lakini kwa siku zijazo kitawanufaisha?

Nauliza hivi kwa sababu kwa yule aliyewahi kufanya kazi na wanasiasa na akawajua vizuri atakubaliana nami kuwa hili ni kundi la watu ambao hawapendani kabisa hata kama ni wa baba na mama mmoja na mifano ipo mingi tu. Sasa iweje leo wageni wapigiwe vigeregere na ngoma?

Tabia za wanasiasa

Wanasiasa ni watu wa kijicho, kila mmoja anapenda kuwa juu ya mwenzie na kila mmoja anamwona mwenzie hafai kuwa pale alipo ila ni yeye ndiye anayesitahili kuwa pale. Hata sifa zinapotolewa kwa wanaojua hiyo huwa ni unafiki na kujikomba tu hata kama mtendaji anastahili kabisa kupongezwa. Wana msemo wao wa usimsifie mgema.

Wana-CCM wamekubali kwa moyo mmoja kuacha utamaduni wao wa toka mwaka 1977, kilipoanzishwa rasmi chama hicho wa kuendesha kura za maoni ili kuwapata wagombea kwa nafasi mbalimbali za uongozi na uwakilishi wa wananchi ndani ya chama hicho ili tu kuwapisha wageni wapya waliotoka upande wa pili.

Wapo baadhi ya wanachama ambao wanaona siyo jambo la haki kuwapa nafasi za uongozi wanasiasa ambao ni wakuja na kuwaacha wale ambao wamekuwa wakikipigania chama hicho kwa miaka dahari.

Nafasi kama ubunge na udiwani siku si nyingi katika kura za maoni ndani ya chama hicho zilikuwa ni vita ya kufa na kupona iliyopiganwa na wana-CCM katika ngazi mbalimbali za matawi, kata hadi majimbo, leo ghafla wameamua kuachana nayo na kuweka silaha chini.

Inajulikana wazi kuwa kulikuwa na mizengwe na ujanja mwingi katika harakati za kuwania uongozi kwa wagombea, lakini si angalau sura ya demokrasia ilionekana kwa jicho la mchana.

Mikakati ya chama

Chama cha siasa kama CCM lazima kina mikakati ya kuendelea kushikilia dola kwa kuwa na wawakilishi wengi na kinatarajia kuvuna dhahabu mbeleni kwa kuwekeza sasa kwa matarajio kuwa mbinu hii inaweza kufifisha upinzani siku zijazo kwa kuwapotezea watu ambao wangekuwa wanajijenga katika majimbo, kata au mitaa kwa kutumia nafasi walizonazo za ubunge, udiwani au uenyekiti wa mitaa.

Yapo madai kuwa kwa kuondoka kwa viongozi wa upande wa upinzani na kujiunga na chama tawala, basi upinzani na siasa zake zinaelekea kufa au upinzani wenyewe utakufa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Haya ni madai dhaifu sana kwa sababu kwa hali tuliyonayo leo na hata miaka ya nyuma wakati vyama vingi vya kisiasa vilipopigwa marufuku upinzani wa nje ya vyama na ndani ya vyama uliendelea kuwepo, kwani Mungu ameumba binadamu walio tofauti kwa vitu vingi ikiwemo matamanio ya kupata kitu fulani kabla ya kufa na katika harakati hizo ni lazima kuwe na vikwazo na moja ya vikwazo hivyo ni vya kisiasa.

Kilichopo ni kuwa wanaondoka binadamu kutoka kambi ya upinzani kuelekea chama tawala, lakini upinzani utaendelea kuzalisha binadamu wengine kwa upande wake kama kinavyofanya chama tawala.

Chama cha Mapinduzi kinajua kuwa ni rahisi kwa mbunge aliyepo kwa sasa kujiweka sawa kwa uchaguzi ujao kwa sababu ana nyenzo za kufanya hivyo kwa mwamvuli wa mwakilishi wa wananchi.

Hii ni kwa kuwa ana fursa ya kuendesha shughuli za kisiasa na fedha, hivyo kuwa vigumu kwa mgombea mpya na hasa akiwa na muda mfupi kuelekea huko ili kupunguza wanasiasa walio kita mizizi upande wa pili ni kuwavuta sasa.

Kwa sasa ni rahisi kwa sababu chama tawala kina rasilimali kubwa ambayo kwa kuitumia katika jimbo, kata au mtaa mmoja mmoja au miwili inakuwa rahisi kwao kupita lakini inapokuja uchaguzi wa nchi nzima inakuwa tatizo kwa sababu wanapambana na wapiganaji wengi katika eneo kubwa.

Inawezekana kabisa wana-CCM wamekubariana kuwa wapokee wageni, lakini wale wenyeji waendelee kujiimarisha huko na wakati wa kura za maoni ndani ya chama mwaka 2020 wageni wapotee kabisa na wenyeji warudi kushika usukani, sababu siasa ndani ya vyama ni kujuana na mgeni hatakuwa na muda wa kujulikana kwa wanachama wengine hivyo kuwa na nafasi nzuri ya kushinda ubunge, udiwani na hata uenyekiti wa serikali ya mtaa.

Mkakati wa Polepole

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, amekwisha weka mkakati kwa wale wanaotoka upande wa pili kuwa wafanye hivyo kabla ya Desemba mwaka huu.

Akiamini kuna ambao wana hofu kuwa huenda wasipite kugombea kwenye vyama vyao vya sasa, hivyo ni vyema wakijitoa sasa kujiunga na chama tawala, lakini kwa kufanya hivyo wanaweza kuwa wamejinyonga kisiasa kwa sababu anayefuatilia hali ya mambo na siasa za ndani ya CCM, kwao haitakuwa rahisi kama ilivyo sasa. Ndani ya CCM watu wanajuana vizuri sana na hata mpiga kura mmoja mmoja anajulikana kampigia nani.

Hivi sasa majimbo, kata na mitaa karibu yote nchini watu wanatamka waziwazi kuwa wanamtaka nani awe mwakilishi wao msimu ujao kupitia Chama cha Mapinduzi na kampeni zinaendelea nyingine za wazi na nyingine za kificho.

Tunashuhudia jinsi ambavyo vijana wanaopenda michezo hasa mpira wa miguu majimboni wakishindana kugombea kombe, ng’ombe na mbuzi kwa majina ya watu na wanaojua hawana wasiwasi wowote kuwa hayo ni matayarisho kuelekea 2020, hiyo ni mbinu ya kujiweka karibu na wapiga kura ili siku ya siku ikifika isiwe shida kumjua nani ni nani kati waliojitokeza kuwania nafasi ya uwakilishi kutokea CCM.

Watu wenye mamlaka na ukwasi wa kiasi fulani huko majimboni wanapita kwa wanachama wenzao wakiwa na matumaini makubwa kuwa wenzao hawawezi kuwaangusha wakati ukifika.

Kwa kuwa hali ya uendeshaji wa shughuli za kisiasa kwa sasa wapinzani wamebanwa na wanaotawala wanaendelea kufanya siasa inawezekana huko ndiko kuliko na siasa za mashindano, hata uzoefu unaonyesha kuwa Chama cha Mapinduzi mara nyingi kimekuwa kikija na sura mpya za uwakilishi wa wananchi kila mara uchaguzi unapofanyika.

Lakini, upande wa pili ambao kwa miaka mingi umekuwa na watu wale wale ambao wamekuwa wakiendesha vyama kwa vile wanavyoona inafaa na hivyo kudumaza demokrasia ndani ya vyama vyenyewe.

Vyama vya upinzani ni lazima vitake visitake hata kama haviko tayari kushiriki chaguzi ndogo za sasa vihakikishe vinakuja na mbinu ambayo itavifanya visipoteze uwepo wao kwenye maeneo ambayo viongozi wake wamehamia upande wa chama tawala kwa sababu bila kufanya hivyo lengo la chama tawala litakuwa limeshinda kwani nia ni kuwapoteza wapinzani majimboni, kata na mitaa ili iwe rahisi kupata viti vingi vya uwakilishi.

[email protected] 0783 165 487

Advertisement