BARAZA LA SALIM: Wanasiasa waache wataalamu serikalini wapumue

Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed (katikati) akizindua utekelezaji wa uzazi wa mpango  visiwani Zanzibar jana wengine ni wadau wa masuala uzazi wa mpango. Picha na Muhammed Khamis.

Tumeona mara nyingi katika maisha kwa historia kujirudia. Mambo mengine huchukua muda mfupi kuyaona tena yamechomoza na mengine hukaa kipindi kirefu ndio hujirudia.

Mwenendo huu wa kurudia jambo ambalo halipendezi haufai na tuyawache kuwa sehemu ya historia na tusiukaribishe na kuupokea.

Katika miaka ya nyuma yalisikika watumishi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wakiwemo wataalamu, walilalamika kwamba walikuwa wanaingiliwa na wanasiasa katika utendaji wao wa kazi za kila siku.

Waliokuwa mstari wa mbele kuingilia watendaji ni wale walioitwa makamisaa wa kisiasa waliowekwa kila ofisi, zikiwemo zile zinazoendesha mambo kitaalamu kama za walimu, wahandisi na madaktari.

Mambo yalikwenda ovyo kwa hali iliyosikitisha na kutisha. Kwa mfano, makamisaa wa kisiasa waliwadhalilisha madaktari waliochelewa kufika kazini, hata waliokesha usiku uliopita kuwatibu watu waliopata ajali za magari.

Miongoni mwa maamuzi waliyoyafanya ni kuwageuza madaktari kuwa wahudumu kwa kuwalazimisha kusafisha wodi za wagonjwa, kupiga deki vyoo na kukosha masufuria ya vyakula jikoni.

Walimu waliingiliwa madarasani kuchunguzwa walivyosomesha na hawa makamisaa ambao wengi hawakuwa hata na elimu ya darasa la nne.

Matokeo yake madaktari wengi, walimu na wataalamu wa fani mbalimbali walikimbilia nchi ajirani na wengine kwenda mbali zaidi na hasa nchi za Ghuba ambapo elimu na utaalamu wao ulithaminiwa na kuanza maisha mapya.

Wengine wapo huko mpaka leo na baada ya kustaafu wanaendelea vizuri na maisha na watoto wao waliopata elimu nzuri sasa wanafanya kazi na kuwasaidia wazee wao.

Hii ni sehemu ya historia ya Zanzibar baada ya mapinduzi na si mara nyingi kuzungumziwa kutokana na taswira yake mbaya.

Kama miaka 20 iliyopita serikali iliwaomba samahani baadhi ya hawa wataalamu walioondoka na kuwaomba warudi nyumbani kutumikia nchi yao na wapo waliokubali, lakini wengine walikataa.

Yaliowakuta yalitosha na kushukuru yalitokea kwa sababu yaliwafungulia milango ya kuwa na maisha bora wao na familia zao nje ya Zanzibar.

Sasa tunasikia minong’ono ya hapa na pale ya historia ile mbaya kujirudia katika baadhi ya sehemu za kazi.

Hivi karibuni, Waziri wa Afya, Hamad Rashid Mohamed amewataka wananchi wawaachie wataalamu wa afya watekeleze majukumu yao kwa weledi ili wapate huduma bora na salama. Alisema utashi wa kisiasa, fitina na majungu unaofanywa katika sekta ya afya haufai kupewa nafasi kwa sababu unachangia kuchafua utendaji.

Heko waziri, hapa umenena na inafaa kupongezwa. Lakini tukubali upo udhaifu unaohitaji kumulikwa na hili lifanywe kwa uadilifu na wataalamu wanaosimamia sekta hizo.

Sishangai kuona historia hii inajirejea. Miongoni mwa sababu zilizofanya nione hivyo ni kauli za baadhi ya viongozi kuwataka viongozi wa CCM popote walipo kusimamia utendaji kazi serikalini ili kuhakikisha ilani ya uchaguzi ya chama hicho inatekelezwa.

Kauli hizi zinatoa sura ya viongozi wa CCM kuwa ndio wasimamizi wa idara na taasisi za serikali na sio waliochaguliwa kushika nafasi za uongozi sehemu hizo.

Unapotoa matamshi haya yenye utashi wa kisiasa ni sawa na kumpa rungu asiyestahiki kupewa na wapo ambao wakishapewa mamlaka hayo ndio hucharuka kufanya watakavyo.

Watu hawa huamua kukomoa wataalamu ili waonekane ni watendaji wazuri wa chama katika kusimamia ilani ya uchaguzi. Badala ya kutengeneza huchafua.

Lazima tuchukue tahadhari katika kuonyesha njia za uongozi na usimamizi wa shughuli za serikali. Kuingiza mambo ya vyama katika serikali au kufungua matawi ya chama katika taasisi hizo kama tulivyofanya zamani kutaleta usumbufu tutakaokuja kujutia.

Upo muhimu wa kujifunza na kutosahau tulikotoka ili kuhakikisha historia mbaya tuliyoiona Zanzibar miaka ya nyuma ambayo nimeielezea kwa muhtasari haijirudii.

Hata viongozi wa serikali kama mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya waache wataalamu wapumue na waongozane katika kazi zao na sio wanasiasa kujifanya wataalamu wa afya, ufundi, kilimo au ufugaji wakati hawana elimu ya msingi ya fani hizo.

Uongozi ni kuonyesha njia na si kujivisha kilemba cha ukoka cha utaalamu na joho la ujuzi wa mambo ambayo wenzako wamechukua miaka kuyasomea na muda mrefu kuyafanyia kazi.

Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed (katikati) akizindua utekelezaji wa uzazi wa mpango visiwani Zanzibar. Wengine ni wadau wa masuala uzazi wa mpango. Picha ya Maktaba