MAGONJWA NA TIBA: Wanawake wajihadhari maumivu sugu ya kiuno

Wiki iliyopita, nilipokea ujumbe mfupi kutoka kwa mmoja wa wasomaji wa safu hii ukisema hivi: “samahani daktari, mwaka mmoja uliopita, nilipimwa na kugundulika nina uvimbe kwenye ovari ya kushoto. Baadaye nikapata ujauzito ambao kwa bahati mbaya uliharibika ukiwa na miezi minne.

Baada ya mimba kuharibika, nimekuwa nikipata maumivu makali ya kiuno yasiyokoma. Nimejaribu kutafuta matibabu lakini wapi na bado nina maumivu makali ya kiuno. Hali hii inaniogopesha na mbaya zaidi, sasa hivi nayapata hata wakati wa kushiriki na baada ya tendo la ndoa.

Kwa kuwa madaktari hawajagundua tatizo, haiwezi kuwa ni dalili ya saratani?” Rose alimaliza kwa kuuliza.

Si Rose peke yake. Nafahamu wanawake wengi wanasumbuliwa na maumivu ya kiuno hata wakati wa kushiriki tendo la ndoa yanayodumu kwa muda mrefu.

Lakini dhana kuwa maumivu makali ya kiuno ni dalili ya saratani ni hofu isiyo na sababu na kukosa uelewa wa kutosha juu ya ugonjwa huo.

Ni kweli maumivu ya kiuno na mgongo yanayodumu kwa muda mrefu ni moja ya dalili kuu za saratani kuna sababu nyingine nyingi zinazoweza kusababisha maumivu haya hata wakati wa tendo la ndoa.

Matatizo ya kiafya kama vile maambukizi sugu kwenye njia ya mkojo, uvimbe kwenye mfuko au mayai ya uzazi na sehemu nyingine au sababu za kisaikolojia huchangia mwanamke kuhisi maumivu ya kiuno au wakati wa tendo la ndoa.

Mwanamke anaweza kuwa na tatizo moja kati ya haya au zaidi na kumsababishia maumivu yenye dalili zinazofanana hivyo ni vigumu kutambua chanzo halisi.

Iwapo maumivu yatadumu kwa zaidi ya miezi sita, ni dhahiri mwanamke huyo anahitaji msaada wa kitabibu. Hivyo, anashauriwa kupata ushauri wa daktari.

Je, Rose ana sababu ya kuhofu kuhusiana na hali hii? Kwa wanawake wengi, kupata maumivu ya kiuno na mgongo hasa baada ya mimba kuharibika kama ilivyotokea kwa Rose ni hali ya kuogopesha.

Kutokana na sura ya tatizo hili, kuna kitu hakipo sawa na Rose ana kila sababu ya kuwa na hofu hasa tukizingatia ukweli kuwa anapata maumivu haya kwa muda mrefu.

Hivyo, ninamshauri Rose na mwanamke mwingine anayepata maumivu ya kiuno, kutokwa damu wakati wa kushiriki tendo la ndoa kufanya vipimo kuchunguza magonjwa ya saratani. Maumivu ya kiuno yanayodumu na chini ya kitovu, mara nyingi ni dalili ya saratani ya ovari.