Wanawake wanatupeleka mbele wanaturudisha nyuma

Sunday November 11 2018

 

By Kelvin Kagambo

Tulianza vizuri sana – Mungu alituambia nendeni mkaishi kwenye bustani, kwa amani na furaha, bila chembe ya mateso. Na mahitaji yenu muhimu ya maisha yatakuwa mawili tu – kula na malazi. Yaani msosi na sehemu ya kulala, tukasema sawa.

Tukaanza zetu maisha pale Edeni na yalikuwa safi sana kama mwenye bustani yake alivyotarajia.

Lakini ghafla mwanamke akakutana na shetani, wakazungumza mambo chungunzima na moja wapo wakajadili namna ya kuongeza hitaji lingine muhimu la maisha ambalo ni nguo – shetani akamwambia, kuleni tu tunda hili, baada ya hapo mtahitaji mavazi.

Na hivyo ndivyo ikawa, Mwanamke akarudi na tunda kwa mwanaume, akamshawishi, wakala, ndipo wakagundua kumbe wanahitaji kuvaa – na mahitaji muhimu ya binadamu yakawa matatu kuanzia siku hiyo; Chakula, malazi na mavazi.

Lakini wenyewe tukaamua kukubaliana na hali, kwa hiyo hakuna kilichoharibika, tukaanza kuishi tukivaa.

Ila sasa mambo yamebadilika, walewale waliojadiliana na shetani na kusababisha matokeo ya kwamba sasa tunatakiwa kuvaa. Wameanza kuona nguo sio hitaji la muhimu tena, na sasa wameanza kutembea wakionyesha tupu zao.

Watoto wa kike wanatembea bila nguo siku hizi, wanatupa majaribu sana mitaani na mabarabarani humo tunapopishana nao. Wanatunyima kabisa muda wa kufikiria mambo yetu.

Unaweza kuwa unatembea njiani unawaza mambo yako muhimu mara ghafla pap, unakutana na mwanamke kavaa nguo zimefunika robo tatu tu ya mwili wake sehemu iliyobaki yote ipo wazi.

Ukimtazama tu kila ulichokuwa unafikiria unakisahau na kinapotea kabisa kichwani. Inabidi ukishapishana nae uanze upya tena kwa kutafuta kitu kingine.

Kuna ambao kidogo wana huruma, wenyewe wanafunika angalau nusu ya mwili. Hao ndiyo unaopishana nao wakiwa wamevaa shati tu na viatu, basi au wale wanaovaa suruali zilizochanika – yaani kama ndiyo msukuma umetoka zako Chato huko, unaweza sema ‘hili limama limekumbana na liajali ama, au maakili yamechomoka.’ – maana nguo zimechanwachanwa huelewi.

Inawezekana ndiyo fasheni, lakini inawaumiza wenyewe hasa maeneo ya mijini humu. Vinguo vya utupu namna hii si jambo ambalo wanaume wa Kiafirka wa enzi za kati tulikuwa tumelizoea – matokeo yake limekuwa moja ya sababu za ubakaji.

Hatumaanishi kwamba wanawake wanaojidhalilisha kwa kuvaa nusu uchi wadhalilishwe pia kwa kubakwa, wala hatutetei kitendo hicho cha kinyama, ila kwenye ukweli wacha uzungumzwe – kwamba nguo za uchi zinaongeza kwa kiasi fulani matukio ya ubakaji.

Kama vipi tuamue kimoja, kama tunaamua kurudia zamani, kwamba cha muhimu kwenye maisha ni kula na kulala tufanye hivyo kwa ujumla wake – yaani tuache kuvaa kabisa labda tutazoea na kila kitu kitaenda sawa.

Kuliko kuwa vuguvugu. Unakutana na mtu njiani hujui umuelewe kama amevaa au yuko utupu – Bora tujue moja.

Advertisement