TUONGEE KIUME: Wanawake washindane na ufanisi binafsi, si wanaume

Sunday March 10 2019

 

Juzi tulikuwa tunasherehekea kimataifa siku ya wanawake — Yaani dunia kwa pamoja tulikuwa tunawakumbusha mama zetu, dada zetu, shangazi, bibi na binti zetu kuwa nafasi yao katika maisha inafahamika, inathaminiwa na umuhimu wao unaonekana kuanzia ngazi za familia, kitaifa hadi kimataifa.

Kwamba labda bado mwanamke au wanawake hawajafikia wanapolenga lakini hilo linawezekana kama wataendelea kung’amua changamoto kubwa zinazowakabili na kuzifanyia kazi.

Hapa kwenye changamoto kuna tatizo — binafsi nakubaliana karibu na dunia nzima kwamba mwanamke ni muhimu duniani. Na ukifuatilia utagundua utofauti mkubwa uliopo kati ya mwanamke na mwanaume ni jinsia tu.

Isipokuwa wanawake wanafeli sehemu moja — kutaka kuithibitishia dunia kwamba wao wanaweza kuwa kama mwanaume au zaidi ya mwanaume. Hii ni propaganda inayowamaliza kila siku pengine bila wenyewe kufahamu.

Milele daima mwanamke hawezi kuwa kama mwanaume na haitakuja kutokea — Ndiyo, kama ambavyo milele daima mwanaume hawezi kuwa kama mwanamke na haitakuja kutokea kwa sababu utofauti wetu na wao upo kwenye upande wa kijinsia tu, jambo ambalo kama utaamua kuchunguza si ambalo limetufanya wanaume kuonekana ni wenye daraja la juu zaidi ya wanawake — bali ni utendaji ndiyo umetuweka hapa.

Sisemi kwamba wanawake si watendaji, hapana. Ninachomaanisha ni kwamba, tangu mwanzo wa maisha ya dunia, wanawake hawakuwa wakipata fursa sawa ya kuonyesha uwezo wao wa utendaji, karibu asilimia 75 ya kila kilichogundulika ulimwenguni sasa kimefanyika na mwanaume kwa sababu wanaume walikuwa wanapewa nafasi ya kufanya na kuonyesha. Hii imetengeneza daraja, wanaume tukaonekana ni wafanisi zaidi.

Sasa kunakowarudisha nyuma wanawake ni kutaka kuthibitisha kwamba wao wanaweza kuwa kama mwanaume. Nadhani, kwa sasa hawatakiwi kushughulikia hilo, wanatakiwa wageuzie jicho kwenye utendaji. Wanapopata nafasi, wafanye kitu kwa ufanisi kuzidi kawaida, yaani washindane na ubora binafsi kuliko kushindana na mtu aliye nje.

Nadhani hii ni kanuni inayowasaidia hata watu wengi waliofanikiwa. Kama unataka kufanikisha jambo pambana na wewe mwenyewe. Tuwaambie mama zetu, binti zetu, wake zetu, shangazi zetu, bibi zetu na kila mwanamke anayetuzunguka kuwa; Wanawake wanatakiwa kupambana na ufanisi wao wenyewe , si kujilinganisha na kushindana na wanaume.

Kwa lugha rahisi ya mfano ni kwamba, kama mwanamke atapewa nafasi ya uongozi leo hii, shabaha yake inatakiwa kuwa kiongozi bora — sio kuongoza kwa ubora zaidi ya wanaume waliowahi kuongoza.

Tunafahamu bado kuna changamoto kubwa ya kupata hizi nafasi, kwa sababu bado si wenye roho wote wanataka kutoa fursa zilizopo mikononi mwao kuwapa wanawake. Lakini hakuna kisichokuwa na changamoto chini ya jua. Mahubiri zaidi kuhusu nafasi kutolewa bila kujali jinsia yafanyike, na wanaopata nafasi wazitumie vizuri.

Advertisement