Wape watoto nafasi ya kuwa na marafiki

Muktasari:

  • Malezi yamekuwa ni changamoto kubwa sana hali ambayo huwafanya wazazi wengi hasa wale wazazi wanaowajengea watoto uzio fulani kwenye familia. Mtoto akitoka shule ni kufungiwa ndani tu, kuangalia katuni au kuwa na michezo ya ndani tu na akitoka nje kucheza basi wazazi wapo karibu.

Tuanze kwa kujiuliza swali–Je, wewe kama mtu mzima dunia yako ingekuwaje kama usingekuwa na marafiki hata wa kukujulia hali tu? Bila shaka ungekua mpweke sana na pengine ungekuwa na msongo wa mawazo. Vivyo hivyo, watoto wako pia wanakua na hisia hizo pale ambapo hawana uhuru wa kuchagua marafiki na kuwa na muda na marafiki zao.

Malezi yamekuwa ni changamoto kubwa sana hali ambayo huwafanya wazazi wengi hasa wale wazazi wanaowajengea watoto uzio fulani kwenye familia. Mtoto akitoka shule ni kufungiwa ndani tu, kuangalia katuni au kuwa na michezo ya ndani tu na akitoka nje kucheza basi wazazi wapo karibu.

Pengine mtoto huyu ana marafiki lakini marafiki hawa kwa njia moja ama nyingine wana uhusiano wa karibu na wazazi wake; yaani wazazi wao ni marafiki basi na watoto wanalazimika kuwa marafiki. Sio vibaya wao kuwa na uhusiano mzuri ila isiwe lazima kwao kuwa marafiki wa karibu.

Ni vyema mtoto akawa huru kuchagua rafiki wa kucheza naye shuleni na hata nyumbani. Wewe kama mzazi unaweza kumsaidia kuchagua marafiki wema kwa kumshauri achague marafiki wenye maadili mema kama wewe ulivyojitahidi kumfundisha. Tumia muda kuchunguza tabia za marafiki aliowachagua mwanao kisha umshauri kuhusu marafiki hawa endapo utaona sio rafiki wazuri.

Ni vyema pia ukayafanya makazi yako kuwa sehemu rafiki kwa marafiki wa watoto wako kujumuika na kufurahi pamoja. Hii itakusaidia kujua tabia za marafiki hawa na pia itasaidia kuwaweka salama watoto wako kwasababu watacheza na kufurahi nyumbani kwako na sio sehemu zingine usizofahamu. Ukiona watoto wanakwepa kuja nyumbani na hawawaleti marafiki zao nyumbani ujue kuna tatizo. Inawezekana wewe ni mkali sana na hauwapi uhuru wa kuchagua marafiki wanaowataka wao.

Katika jamii yetu kuna familia chache sana amabapo watoto wa rika tofauti wanakaribishwa na kucheza kwa uhuru nyumbani. Ukizichunguza hizi familia, utagundua kuwa wazazi wanawajali marafiki wa watoto wao kama marafiki zao wenyewe. Sio kwamba watoto wataruhusiwa kutokuwa na adabu au kufanya vitendo vya ajabu kwenye nyumba hizi. La hasha! Wanakuwa na tabia njema kwasababu mzazi anawaheshimu na kuwajali kwahiyo watajitahidi wasivunje uhusiano huo.

Kumbuka kwamba watoto hufurahi zaidi wanapokuwa na marafiki zao. Zile zawadi unazowapa zinakuwa nzuri zaidi wakiweza kuzitumia pamoja na marafiki zao. Wajumuishe marafiki zao hata kwenye mitoko yenu ya kifamilia.

Siku zote fungua milango kwa watoto kufurahi nyumbani kwako na watoto wenzao na utawasaidia kuepuka mengi kwa dunia ya sasa yenye changamoto za kila namna. Utajua wanacheza michezo gani, wanaongea lugha gani na kujua tabia zao kiundani zaidi. Huu ni mwanya mzuri kwa mzazi kumfundisha mwanao na marafiki zake kile unachoona ni sahihi na pia kuwarekebisha pale wanapokosea.