Warioba asimulia ugumu wa kumpata Nyalali kwa uteuzi wa jaji Mkuu 1977

Wednesday April 17 2019
pic warioba

Tangu Tanzania ilipopata uhuru wake mwaka 1961 wamekuwapo viongozi mbalimbali mashuhuri ambao wametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.

Mmoja wa viongozi viongozi hao ni Jaji Francis Nyalali ambaye alikuwa Jaji Mkuu wa Tanzania kwa miaka 23 kuanzia mwaka 1977 – 2000.

Huyu ndiye jaji mkuu anayetajwa kuhudumu katika nafasi hiyo kwa muda mrefu kuliko wote nchini. Ni jaji mkuu anayetajwa kupata nafasi hiyo bila kuwa na muda mrefu katika nafasi ya jaji lakini aliitumikia kwa kipindi kirefu kwa ufanisi na mafanikio.

Katika historia ya Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Nyalali ndiyo viongozi waliotumikia nafasi zao za kuongoza mhimili wa dola kwa miaka 23 mfululizo. Wakati Nyalali akiwa jaji mkuu, Nyerere alikuwa Rais wa Tanzania kuanzia mwaka 1962 – 1985.

Kiongozi mwingine wa mhimili wa dola aliyeshika madaraka kwa muda mrefu ni aliyekuwa spika wa Chifu Adam Sapi Mkwawa.

Mkwawa alishika upika kwa vipindi viwili tofauti, mara ya kwanza kwa miaka tisa kati ya 1964 na 1973; na baadaye kwa miaka 19 kati ya 1975 na 1994 alipomwachia Pius Msekwa.

Advertisement

Kazi aliyofanya Jaji Nyalali inatajwa na majaji kuwa zilijaa uadilifu na zenye heshima.

Hivi karibuni majaji mbalimbali wastaafu na watu wengine waliowahi kufanya kazi na Jaji Nyalali waliungana na familia kuyake katika hafla ya kumbukizi ya mchango wake. Nyalali alizaliwa Februari 3, 1935 na kufariki dunia Aprili 3, 2003.

Warioba na uteuzi wa Nyalali

Akimzungumzia Nyalali, Waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba anasimulia kwamba baada ya aliyekuwa Jaji Mkuu, Augustine Saidi kustaafu mwaka 1977, swali kubwa lilikuwa ni nani atakuwa mrithi wa nafasi yake.

Anasema swali hilo lilikuwa gumu kujibiwa ingawa walikuwepo majaji wengi.

Warioba anasema anakumbuka siku moja aliitwa na Mwalimu Nyerere nyumbani kwake Msasani, wakati huo yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Alipofika, anasema Mwalimu Nyerere alimtaka apendekeze majina ya majaji wanaofaa kuwa jaji mkuu.

“Tulifanya hivyo. Tulimpelekea orodha ya majaji wanaofaa kuwa jaji mkuu, tukawa tunasubiri afanye uteuzi wa nafasi hiyo,” anasema.

Jaji Warioba anasema katika orodha ya majaji walioyoiwasilisha kwa Mwalimu kulikuwa na majaji wazoefu akiwamo Nyalali ambaye alikuwa na miaka mitatu tu kama jaji,” anasema.

Anasema siku moja (ilikuwa Ijumaa, mwaka 1977, Mwalimu Nyerere alimwambia Warioba kwamba anamtaka Nyalali ifikapo Jumatatu asubuhi, Ikulu jijini Dar es Salaam. Anasema suala hilo lilimshtua kwa sababu wakati huo Nyalali alikuwa anafanya kazi yake ya ujaji mkoani Arusha na usafiri wa kumfanya afike Ikulu Jumatatu haukuwapo.

“Nilitafakari Nyalali atawezaje kufika hapa Dar es Salaam Jumatatu. Kwa gari (wakati huo) haiwezekani. Kipindi hicho Jumuiya ya Afrika Mashariki ilikuwa imevunjika na hakuna ndege zinazosafiri. Ilikuwa changamoto,” anasimulia Warioba.

Warioba anasema baada ya kuachana na Mwalimu siku hiyo alimpigia simu Nyalali na kumjulisha kwamba Rais Nyerere anamhitaji Jumatatu. Anasema Nyalali alishtuka na kumuuliza anaitiwa nini, lakini alimwambia hata yeye hajui anachoitiwa na Rais.

Anasema ilipofika Jumapili, walifanikiwa kupata ndege ya jeshi ambayo ilimsafirisha Nyalali kutoka Arusha mpaka Dar es Salaam. Anasema yeye (Warioba) alikwenda uwanja wa ndege (upande wa jeshi) na kumpokea Nyalali na kumpeleka moja kwa moja mpaka nyumbani kwa Mwalimu Nyerere.

Anasimulia kwamba walipofika nyumbani kwake, baada ya kuwakaribisha, Mwalimu alimwita Nyalali katika ofisi yake na kumwacha Warioba akisubiri sebuleni.

Anasema Mwalimu Nyerere na Nyalali walizungumza na baada ya muda walitoka.

“Nakumbuka walipotoka, Nyalali alikuwa mwenye furaha na alinipita, akasahau kama mimi ndiyo niliyempeleka kwa Mwalimu,” anasema Warioba huku viongozi wengine wastaafu na wanafamilia wakicheka.

Warioba anasema siku iliyofuata (Jumatatu) Februari 15, 1977, Nyalali aliapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.

Maneno yaibuka

Kwa mujibu wa Warioba baada ya Nyalali kuapishwa, yaliibuka maneno ya chinichini kutoka kwa majaji wengine ambao walidhani kwamba wao ndiyo walistahili kwa sababu wamekuwa majaji kwa muda mrefu, tofauti na Nyalali ambaye alikuwa na miaka mitatu ya ujaji kabla ya kuteuliwa kuwa jaji mkuu.

Hata hivyo, Warioba anabainisha kwamba sifa mbili ndiyo zilizotumika kumteua Nyalali ambazo ni uongozi na uadilifu. Anasema majaji wengine walikuwa waadilifu lakini walikosa sifa ya uongozi ambayo Nyalali alikuwa nayo.

Uhuru wa mahakama

Katika kuhakikisha mahakama inasimama, Nyalali alikuwa hamvumilii mtu yoyote ambaye aliingilia uhuru wa Mahakama, kwa mujibu a Jaji mstaafu, John Mroso.

Anasema alisimama imara katika kulinda uhuru wa mhimili huo usiingiliwe na mtu yeyote hasa wanasiasa.

Anasema haikuwa kazi ndogo kusimamia uhuru wa Mahakama wakati wa mfumo wa chama kimoja kwa sababu kila mtu aliamini kwamba chama ndiyo kila kitu.

Anasema msimamo wake huo uliungwa mkono na Mwalimu Nyerere na ndiyo maana Mahakama ikabaki kuwa chombo kinachoaminika na kuheshimiwa na watu wote.

“Huwezi kuzungumzia mafanikio ya Mahakama bila kumzungumzia Nyalali. Yeye ndio aliifanya Mahakama kuwa mhimili unaojitegemea.

Wakati anakuwa Jaji Mkuu, Mahakama ilikuwa ni Idara ya Serikali lakini baadaye ikawa ni mhimili unaojitegemea,” anasema Mroso.

Aliishi maisha ya kawaida

Jaji mstaafu, Damian Lubuva anasema alianza kumfahamu Nyalali tangu alipokuwa hakimu huko Musoma mkoani Mara na baadaye alifanya naye kazi kwa miaka saba yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Nyalali akiwa jaji mkuu mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Anasema wakati wote huo, amemfahamu Nyalali kama kiongozi ambaye alizingatia maadili ya kazi na aliifanya kazi yake kwa makini. Alisema Nyalali hakuwa kiongozi aliyependa kujilimbikizia mali bali aliishi maisha ya kawaida.

“Nyalali atabaki katika historia kama alama ya uongozi wa Taifa hili. Kwa kipindi kile, kuongoza Judiciary (Mahakama) kwa miaka 23, haikuwa kazi rahisi. Changamoto zilikuwa nyingi lakini alijitahidi na kuhakikisha mahakama inasimama,” alisema Jaji Lubuva.

Advertisement