Watahiniwa walivyolinda rekodi za ufaulu kidato cha pili

Tuesday January 29 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Uchambuzi wa Mwananchi wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyotangazwa wiki iliyopita, unaonyesha kuwa matokeo ya watahiniwa waliofanya vizuri yanaakisi kile walichokifanya katika mtihani wa kidato cha pili mwaka 2016.

Sio tu watahiniwa waliofanya vizuri, hali hiyo ya ‘ kulinda rekodi’ ya ufaulu inajionyesha pia kwa shule zilizofanya vibaya.

Mwanafunzi bora kitaifa

Kama unafikiri Hope Mwaibanje amekuwa mwanafunzi wa kwanza katika matokeo ya kidato cha nne kwa kibahati, umekosea. Amelinda rekodi ya kuwa kinara wa masomo.

Alichokifanya kidato cha nne, ndicho alichokifanya mwaka miaka miwili iliyopita alipokuwa kidato cha pili.

Katika matokeo ya kidato cha nne, Hope amepata daraja la kwanza la alama saba ambalo ndilo daraja kubwa zaidi katika mfumo wa upimaji wa mitihani ya kidato cha nne nchini.

Kinachosisimua zaidi kwa Mwaibanje ni namna alivyoweza kulinda ufaulu wake. Katika matokeo ya kidato cha pili, alipata alama A katika masomo tisa ukiwa ni ufaulu wa daraja la kwanza.

Katika mtihani huo wa kidato cha pili ambao matokeo yake yamekuwa sawa kwa alama na ya kidato cha nne, Hope alipata matokeo yafuatayo: Uraia-A, Historia- A, Jiografia – A, Kiswahili- A, Kiingereza- A, Fizikia- A, Kemia- A, Biolojia- A na Hisabati- A.

Ufaulu huo huo umejirudia tena katika mtihani wa kidato cha nne. Amepata daraja la kwanza akiwa na alama saba kwa kupata A kila somo.

Watahiniwa wengi wamepata daraja la kwanza la alama saba, wakiwamo wanafunzi 41 wa shule ya St Francis iliyoshika nafasi ya kwanza kitaifa, Lakini kwa Mwaibanje kuongoza kitaifa ni dhahiri alipata alama kubwa zaidi kuwazidi watahiniwa wenzake wengi waliopata alama hizo.

Inawezekanaje?

Sio ajabu kwa mwanafunzi kupata alama A katika masomo yake, Mwaibanje mwenyewe anasema siri ya ufaulu huo ambao bila shaka umechangia kuiinua shule yake ni kusoma kwa kujituma.

“Shuleni kulikuwa na ushindani mkubwa katika masomo na mimi nilitokea shule za mtaani, ila nilijituma kutimiza nia yangu ya kuwa daktari bingwa wa moyo,’ anaeeleza.

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet), Cathleen Sekwao anasema inawezekana mwanafunzi kupata alama A masomo yote, japo katika uzoefu wake wa kufundisha aliwahi kushuhudia ufaulu huo mara moja ndani ya miaka 25.

Anasema mwanafunzi anayepata alama A masomo yote ni yule mwenye akili za masomo, anayejituma kusoma, walimu wazuri na vifaa vyote vya kujifunzia. “Kuna zile akili za kuzaliwa wanafunzi wanaopata alama A mara nyingi huwa wanazo hizo, lakini jitihada katika kujisomea na walimu wazuri,” anasema na kuongeza:

‘’Mazingira ya shule pia yanaweza kumfanya apate alama A na jitihada za wazazi katika kufuatilia na kuhakikisha wanampatia mahitaji yote ya msingi.’’

Shule ya kwanza kitaifa

Kuna shule huwa hazibahatishi. Moja ya shule hizo ni St Francis Girls ya mkoani Mbeya.

Unajua kuwa ilichofanya katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2018 na kuwa kinara wa matokeo hayo kitaifa ndicho ilichokifanya mwaka 2016 katika matokeo ya kidato cha pili?

Katika matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa wiki iliyopita, shule hiyo ilikuwa na watahiniwa 91 ambao wote walipata daraja la kwanza, wakiwamo 41 waliopata daraja la kwanza la alama saba.

Inavyoonekana moto huu haukuanza 2018, hata 2016 katika matokeo ya kidato cha pili mambo shuleni hapo yalikuwa motomoto. Wanafunzi wote 92 waliokuwapo walipata daraja la kwanza.

Cha kustaajabisha zaidi ni kuwa katika matokeo ya kidato cha pili, wanafunzi hao wote walipata daraja la kwanza la alama saba.

Inawezekana ugumu wa mitihani ya kidato cha nne, uliwagusa wanafunzi wengi hivyo kushindwa kulinda rekodi ya ufaulu wa A saba. Katika mtihani huo wanafunzi 41 kati ya 91 ndio waliopata daraja la kwanza la alama saba.

Shule za mwisho nazo?

Moja ya shule za mwisho katika matokeo hayo ni Kwediboma iliyopo mkoani Tanga. Kati ya watahiniwa 99 waliofanya mtihani, 75 wamepata daraja sifuri, 19 daraja la nne na wanafunzi watano daraja la tatu. Hakuna daraja la kwanza na la pili.

Katika mtihani wa kidato cha pili mwaka 2016, shule hiyo ilikuwa na watahiniwa 106 waliopata daraja la nne, watano walipata daraja la tatu na watatu daraja la pili.

Kama ilivyo kwa matokeo ya kidato cha nne, katika matokeo ya kidato cha pili, hapakuwapo pia wanafunzi waliopata daraja la kwanza na la pili.

Advertisement