KUTOKA LONDON : Watanzania wengi bado hatuelewi nini saladi na faida yake kiafya

Muktasari:

  • Ukweli ladha ni muhimu ndiyo. Ila si ajabu leo ukienda mahoteli ya weusi ndani na nje ya Afrika vyakula jazwa sana chumvi, pilipili na sukari. Matokeo maradhi ya figo yanatusakama. Figo kazi yake kuchuja kisichofaa mwilini ili kukitoa kama mkojo.

Baada ya makala kuhusu saladi wiki jana, mwananchi mmoja aliniandikia baruapepe kuniunga mkono. Watanzania bado tunaona kula majani ni kujidunisha, akatathmini.

Desturi, mtazamo na mazoea yetu Waafrika ni kuendekeza ladha....

Ukweli ladha ni muhimu ndiyo. Ila si ajabu leo ukienda mahoteli ya weusi ndani na nje ya Afrika vyakula jazwa sana chumvi, pilipili na sukari. Matokeo maradhi ya figo yanatusakama. Figo kazi yake kuchuja kisichofaa mwilini ili kukitoa kama mkojo.

Sasa...mmh.

Je, nini maana ya kula?

Hatusemi lengo la kula si kushiba. La hasha. Azma pia ni kuurutubisha mwili. Miili yetu ni kama shamba. Yatakiwa kustawishwa na kupaliliwa. La sivyo maradhi na utapiamlo hutuvamia. Matokeo? Wastani wa maisha yetu Waafrika mafupi SANA. Kama tulivyoona wiki jana ili mwanadamu aishi sawasawa - kila siku ahitaji aina nne za vyakula, yaani, virutubishi: Wanga, Protini, Madini na Vitamini. Wanga hutupa nguvu. Mahindi, unga, viazi, ndizi (za kupikwa) na mchele. Hivi hutofuatiana kikabila, nchi na bara. Mathalan kwa Wazungu wanga uliozoeleka ni viazi Ulaya na ngano (mikate, Pasta nk). Bara Asia ni ngano na mchele. Marekani ya Kusini ni sawa na Afrika.

Pili - protini. Ujenzi wa mwili. Protini ipo katika nyama na mboga za majani. Kwetu tumezoea mboga zilizopikwa (mchuuzi). Kwa mfano mtu akila wali kwa kisamvu, anaona kamaliza siku. Kumbe hiyo ni nusu tu ya kisa kizima ki-afya.

Kama wanga, kila bara na mataifa hutofautiana.

Nilipotembelea Paraguay, miaka ya 1990 nilishangaa namna nyama ilivyo tamu na inavyopewa kipaumbele. Ukanda wote wa Argentina, Paraguay na Uruguay una nyanda maarufu za “Pampas.” Hapo mifugo hulelewa vizuri kama Umasaini. Hivyo nyama ni protini kuu. Brazili iko hivyo hivyo, ila kinyume na Paraguay, Wabrazili huzingatia sana chakula chenye uwiano na Saladi zao makini sana.

Tatu na nne ni Madini na Vitamini. Mwili unapokosa madini- haufanyi kazi ipasavyo. Kazi kuu ya madini ni kuhimili mifupa, damu na kiwiliwili. Ukosefu wa madini hukaribisha maradhi makubwa kama “uchovu wa kudumu.”

Takwimu za kiafya zinadai, asilimia 25 ya watu duniani wanakosa madini. Upungufu huu husababisha udhaifu wa kinga maradhi (kuugua ovyo) na ubongo kutofanya kazi sawasawa. Kwa wanawake ukosefu wa chuma husababisha maradhi ya Anemia. Ugonjwa huu wa damu huleta uchovu na mwanamke akiwa mjamzito anaweza hata kupoteza mtoto. Kwa watu wa makamo au wazee ukosefu wa Magnesium unakaribisha maradhi ya moyo, kupinda mgongo (kibiongo) na kuchoka haraka.

Vyakula vya madini ni mboga mbichi za majani (katika Saladi), mbegu (korosho, karanga, mbozi mbichi nk) maharage, nyama nyekundu na samaki.

Kazi kuu ya vitamini ni kuukinga mwili na maradhi, kuukuza, kuhakikisha ngozi, nywele na viungo vinafanya kazi. Vitamini ni katika matunda, nyanya na mboga mbichi.

Ulaji Saladi basi hukidhi sana mahitaji ya madini na vitamini. Tunapokula wanga na protini tu bila kujali aina ya tatu na ya nne, tunadunisha maisha yetu. Mboga mbichi au matunda huliwa siku moja moja – kama sikukuu au wageni wakifika- ilhali ZATAKIWA KILA SIKU.