Waweka vyeti kabatini na kujiajiri kilimo cha mbogamboga

Muktasari:

Hata hivyo, huu siyo mtazamo wa kijana msomi wa fani ya masoko, Obison Obadia na wenzake watatu walioamua kuweka vyeti kabatini na kuunda kikundi cha kilimo na kuachana na tamaa ya kusubiri ajira ofisini.

Msomi yeyote huringia vyeti vyake, kwa kuwa ni kati ya vitu vya thamani kubwa kwake.

Kwa mtafuta ajira, vyeti havichezi mbali, asipoviweka katika bahasha na kutembea navyo ataviweka mahali rahisi kuvifikia.

Hata hivyo, huu siyo mtazamo wa kijana msomi wa fani ya masoko, Obison Obadia na wenzake watatu walioamua kuweka vyeti kabatini na kuunda kikundi cha kilimo na kuachana na tamaa ya kusubiri ajira ofisini.

Anasema kwa mara ya kwanza yeye na wenzake ambao ni wahitimu wa elimu ya juu walikutana mwaka 2016 katika semina iliyoandaliwa na mbunge wa Segerea Bonna Kaluwa, iliyolenga kutoa mafunzo kwa vijana na wajasiriamali wadogo. “Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kundi hili; tulikubaliana kuanzisha miradi mbalimbali ya kilimo itakayolenga kutuongezea kupato pamoja na kutoa elimu kwa wahitimu wa vyuo ambao ndiyo waathirika wakubwa wa tatizo la ajira nchini,” anasema Obadia.

“Katika kundi hili, kila mmoja wetu ni mkulima, kwa hiyo tukasema kwa nini tusitumie fursa hii kushawishi wenzetu wengine ambao wapo mtaani na hawana ajira kuingia kwenye kilimo?”

Anasema kikundi chao kiitwacho Kilimo Mkombozi, kinajishughulisha na kilimo cha mbogamboga maeneo ya Kisarawe, Mlandizi, Rufiji, Kigamboni na Mwasonga.

Kwa nini walichagua kilimo cha mbogamboga?

Obadia anasema chaguo lao la pekee lilikuwa kilimo cha mbogamboga kwa kuwa hakihitaji muda na nguvu nyingi kusimamia.

Anasema kingine kilichowasukuma kuingia kwenye kilimo hicho ni soko hasa baada ya kubaini mazao ya mboga yana soko kubwa katika jiji la Dar es Salaam. “Ukiangalia katika jiji hili, mboga nyingi zinatokea mikoa ya Morogoro na Pwani hivyo kwetu hii ni fursa kwa sababu tuna uhakika wa soko,” anaeleza Obadia.

Pia, anasema mbogamboga ni mazao yanayoweza kumpatia mkulima faida ndani ya muda mfupi akitolea mfano mchicha kuwa unavunwa baada ya wiki tatu na matembele ambayo huvunwa ndani ya siku 40.

“Mazao jamii ya mbogamboga hayana changamoto kubwa katika kuyasimamia ukitoa mazao mengine ambayo yanataka usimamizi wa karibu. Mbogamboga hazihitaji usimamizi mkubwa; ni rahisi kusimamia na hakihitaji mtu kuwa na mtaji mkubwa wa kuanzia,’’ anafafanua.

Obadia anasema wanalima mboga kama vile matembele, mchicha, majani ya maboga, sukuma wiki pamoja na majani ya kunde.

Pia, anasema kwa siku wana uhakika wa kuingiza zaidi ya Sh 200,000 katika kila mashamba yao.

Mafanikio

Obadia anasema kikubwa wanachojivunia kama sehemu ya mafanikio ni kutoa elimu kwa vijana 30 waliohitimu elimu ya juu na kuwashawishi kuingia kwenye ajira ya kilimo.

“Ukiangalia hivi sasa zaidi ya vijana 100,000 wanahitimu elimu ya juu kila mwaka, lakini wanaopata ajira ni asilimia 20 pekee, huku wengine wakiishia mitaani bila kazi ya kufanya,”anasema.

Hata hivyo, anasema kikubwa zaidi ni kuwa kila mmoja katika kikundi chao amefanikiwa kujenga nyumba na kununua gari kwa ajili ya kurahisisha utembeleaji wa miradi.

Changamoto

Katika kila mafanikio changamoto hazikosekani, kikundi cha kina Obadia kinalia na soko la nje.

Obadia anasema wanatamani siku moja wauze mbogamboga nje ya nchi lakini hawajui namna ya kulifikia. “Tunazalisha mboga nyingi lakini tunaishia kuziuza hapahapa nchini. Tulitamani na sisi siku moja tusafirishe mboga zetu nje ya nchi, lakini hatuna wa kutuunganishia kwa sababu ushiriki wa Serikali kuhusu kutafuta masoko hasa kwa wakulima ni mdogo,” anaeleza na kutaja changamoto nyingine kuwa ni kutokuwa na uwezo wa kununua vifaa vya kisasa vya kulimia.

Kilimo kinalipa

Pamoja na changamoto katika kilimo, Obadia anasema kilimo kinalipa ila kinachotakiwa ni usimamizi na kujitoa. Anasema Sh200,000 wanayopata kwa siku, ni uthibitisho kuwa kilimo kinaweza kuwakomboa vijana wakaachana na tamaa ya kuajiriwa.

“Kitu kingine ambacho pengine watu hawafahamu ni kwamba kilimo ni biashara, hivyo kuna kupata na kukosa, cha msingi mkulima hatakiwi kukata tamaa.

“Hii ipo katika biashara yoyote; ukiisimamia vizuri unapata faida na pia ukisimamia vibaya unaweza kupata hasara na kukukatisha tamaa.”

Serikali na kilimo kwa vijana.

Kwa mtazamo wake, anaamini Serikali haijawa na mwamko wa kusaidia na kuwapa motisha vijana kuingia kwenye kilimo kama njia mojawapo ya kujiajiri wenyewe.

“Serikali na taasisi mbalimbali zitafute namna ya kuwawezesha vijana ikiwamo kutafuta mashamba, kuwapelekea wataalamu wa kilimo ambao watawasimamia, kutafuta masoko, kutoa mikopo midogo. Kwa hili, vijana hawatosumbuka kutafuta ajira kama ilivyo sasa

“Tunahudhuria kwenye semina mbalimbali tunazungumza na vijana; kila unayemuuliza anakwambia yupo tayari kulima lakini hana mtaji na hajui akilima atamuuzia nani,” anasema Obadia.

Wosia kwa vijana

Obadia anawaasa vijana wa Kitanzania kuachana na kasumba ya kupenda kuajiriwa ili waonekane kuwa wanafanya kazi katika kampuni kubwa hata kama wanalipwa mshahara kidogo.

Anasema njia pekee ya vijana kuinua maisha yao ni kupitia kilimo na siyo lazima kiwe cha mazao ya mbogamboga, bali mazao yoyote yenye tija.

“Pia, kwa wale wenzangu ambao tunatumia mitandao ya kijamii, tuitumie vizuri kwa kutangaza miradi yetu na siyo kutuma au kutumiana picha zisizofaa. Mfano, mimi na wenzangu tulifahamiana kupitia mitandao ya kijamii kabla hatujaonana na kupanga mikakati yetu,’’ anasema Obadia.