Wazazi waaswa kukaa na watoto

Muktasari:

  • Akizungumza baada ya kumaliza kampeni ya kupambana na tatizo la mimba shuleni katika wilaya mbalimbali nchini, Mapalala alisema tatizo hilo linasababishwa na ukimya wa wazazi na walezi na linaweza lisiishe kama hawatajenga tabia ya kuzungumza na watoto wao.

Mkurugenzi wa Shirika linalojihusisha na masuala ya kisaikolojia kwa watoto (REPSSI), Edwick Mapalala amewashauri wazazi na walezi kuzungumza na watoto wao kuhusu afya ya uzazi, badala ya jukumu hilo kuwaachia walimu peke yao.

Alisema wanafunzi wengi wanaingia kwenye uhusiano wakiwa na umri mdogo bila kujua madhara ya kufanya hivyo.

Akizungumza baada ya kumaliza kampeni ya kupambana na tatizo la mimba shuleni katika wilaya mbalimbali nchini, Mapalala alisema tatizo hilo linasababishwa na ukimya wa wazazi na walezi na linaweza lisiishe kama hawatajenga tabia ya kuzungumza na watoto wao.

“Kaa na mtoto mwambie kuhusu mwili wake, mwambie akikutana na mwanaume atapata mimba na ataacha masomo. Mweleze anaweza kujitunza vipi amalize masomo yake salama, kama tusipoongea nao watoto wetu nani ataongea nao? Walimu na wanaharakati ni ziada tu, kazi inapaswa kuanzia nyumbani,” alisema na kuongeza;

“Sio tu mtoto wa kike, watoto wa kiume wanatakiwa kusaidiwa zaidi, waambiwe kuhusu miili yao na madhara wanayoweza kusababisha wakikutana na wasichana. Nina uhakika tukifanya hivi suala la mimba litapungua kwa kiasi kikubwa.”

Mapalala alisema kinachosababisha kuwepo kwa ukatili wa kijinsia kwa watoto, ndoa na mimba za utotoni ni jamii kuacha miiko na misingi ya kimaadili inayopaswa kufuatwa.

“Malezi yanaanzia nyumbani kwenye familia, wazazi mkishindwa hapo basi ni rahisi mtoto kuanza njia zake za ajabu na mwisho ni mimba,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Ofisa mtendaji wa kijiji cha Kiziko, wilayani Mkuranga Benjamin Mwang’ombe alisema tatizo la mimba kwenye eneo lao linachangiwa na baadhi ya wazazi kuendeleza mila potofu ikiwamo watoto kuchezwa.

“Wanapochezwa hawafundishwi kujua afya zao wanafundishwa mambo ya wakubwa na wakitoka hapo wanaenda kujaribu. Mwisho wanaamua kuolewa au kupata mimba wakiwa shuleni,” alisema.

Alisema serikali ya kijiji hicho imeanzisha mpango wa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu ya kupambana na tatizo hilo.

Alisema pia wapo watoto wanaoolewa chini ya umri wa miaka 18, jambo ambalo ni gumu kulizuia.