Wimbi la utekaji linavyoongeza hatari kwa askari wasiovaa sare

Muktasari:

  • Polisi JamiiPolisi Jamii au Ulinzi Shirikishi ni mkakati wa utendaji kazi wa Jeshi la Polisi. Lengo kuu ni kuweka mazin-gira ya ushirikiano baina ya wanan-chi na Polisi kutatua matatizo ya jamii ikiwemo uhalifu.
  • Mfumo wa polisi jamii una faida kuu zifuatazo ambazo haziwezi kupatikana kika-milifu chini ya mfumo uliozoele-ka wa utendaji wa kazi za polisi. Faida hizi ni: polisi kufanya kazi na wananchi, kujenga mazingira ya kuaminiana, kuweka mazingira ya ubia, kuhama-sisha ubunifu na kupata ufumbuzi stahimilivu wa kero za wananchi

Mwanzoni mwa Karne ya 19, mhalifu konkodi, Eugene Francois Vidocq alipoamua kubadilika na kutumia mbinu zake za ujahili kuisaidia Serikali ya Ufaransa, dunia ilipokea na kupanua mfumo wa vyombo vya usalama kuwa na mashushushu ili kurahisisha kunasa wahalifu na mitandao yao.

Mwaka 1811, Vidocq alianzisha mtandao wake wa mashushushu, ukiitwa Surete Nationale, yaani Usalama wa Taifa. Mtandao huo ulifanya kazi za kuzisaidia mamlaka za nchi kuwanasa wahalifu na makundi yao. Surete nationale kwa sasa ni jeshi rasmi la polisi, liitwalo National Police.

Muongo wa tatu wa Karne ya 19, aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza, Sir Robert Peel (kipindi akiwa waziri wa mambo ya ndani, alianzisha mtindo wa kutumia mashushushu katika jeshi la polisi la nchi hiyo, The Metropolitan, kisha Marekani ilifuata mwanzoni mwa karne ya 20, polisi New York walipoanzisha idara maalumu waliyoiita Italian Squad.

Katika kila nchi kuna mashushushu, wapo wenye kufanya kazi ndani au nje ya nchi. Wapo wa idara za itelijensia vilevile polisi wanaotumika kwa kazi maalumu. Umuhimu wake ni mkubwa katika kulinda na kuzuia uhalifu wa aina mbalimbali kwa nchi na wananchi.

Askari kanzu wa polisi

Shushushu wa polisi au askari kanzu, kwa maana ya askari asiyevaa sare rasmi za jeshi. Askari kanzu lina upana mkubwa, linamtafsiri kila askari asiyevaa sare. Ndani ya jeshi la polisi, askari wa aina hiyo wanatumika zaidi kitengo cha itelijensia wanaoshughulika na upelelezi wa masuala mazito, kama hili na Mo Dewji.

Hivi sasa Tanzania imekumbwa na hali ya wasiwasi kuhusu vitendo vya utekaji. Hivi karibuni, mfanyabiashara Mohammed Dewji alitekwa na watu ambao mpaka sasa hawajafahamika na kumshikilia kwa siku nane kabla ya kumwachia.

Mo alitekwa na watu wenye bunduki ambao walimchukua katika Hoteli ya Colosseum, Oysterbay, Dar es Salaam na kumpakia kwenye gari. Gari hilo baadaye lilitelekezwa na watekaji katika viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam, siku ambayo walimwachia huru Mo.

Tatizo endelevu

Kati ya Machi na Aprili mwaka jana, mwanamuziki wa Hip Hop nchini, Ibrahim Mshana ‘Roma Mkatoliki’, akiwa na wenzake watatu, walitekwa na watu wasiojulikana na kuwashikilia kwa takriban siku tatu. Akina Roma walikuwa studio ya muziki ya Tongwe Records, Oysterbay, walipovamiwa na watekaji.

Kwa mujibu wa maelezo ya Roma na wenzake, ni kwamba watekaji walikuwa na bunduki pamoja na pingu. Walivyochukuliwa walidhani ni polisi lakini ikawa kinyume chake. Waliwapiga, kuwavunja meno na kuwaachia majeraha na alama mbalimbali zenye kuonyesha kwamba walipewa msoto mkali.

Jinsi mwandishi wa habari wa kujitegemea, aliyekuwa akiripoti gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda, alivyopotea, hisia za karibu zaidi ni kwamba alitekwa. Kuna watu waliokuwa wamevalia kiraia walikuwa naye kwenye gari, wakaongozana mpaka kwa mkewe shambani kufuata ufunguo wa nyumba yao, baada ya hapo hakuonekana tena. Mkewe alikuta nyumbani kumepekuliwa.

Hisia za awali zingeweza kukwambia watu walioongozana na Azory ni polisi waliokuwa katika mavazi ya kawaida. Hata hivyo, baada ya Azory kupotea jumla, jawabu ambalo lina nguvu zaidi ni kuwa wale watu hawakuwa polisi, isipokuwa ni watekaji. Mtanzania aliyefuatilia tukio la Azory anawaza jinsi ya kujilinda dhidi ya watu wenye kuvaa kiraia wenye kujiita polisi.

Ben Saanane, kada wa Chadema aliyekuwa msaidizi binafsi wa Freeman Mbowe, alitoweka tangu Novemba 2016 na hakuna taarifa za ulipofikia uchunguzi wa tukio hilo.

Ndani ya Bunge Aprili mwaka jana, Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, alidai kutekwa na watu aliowaita maofisa wa usalama.

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, alikwenda mbele zaidi na kuvituhumu bungeni vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutofanya kazi sawasawa na kujikuta vikigongana kwa majibu kuhusu Saanane, namna alivyopotea na watu walio nyuma ya kupotea kwake.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Kigoma, Simon Kanguye, inaelezwa alifuatwa nyumbani kwake na watu waliodhaniwa ni polisi. Baada ya kitambo kirefu kupita na kutafutwa vituo vyote vya polisi bila mafanikio, jawabu la karibu ni kuwa wale waliomchukua ni watekaji. Hapohapo ongeza kwamba mitaani kuna watu hujifanya maofisa wa polisi na wengine usalama. Hujivika wasifu bandia ili kufanya utapeli.

Hatari kubwa kwa askari

Kutokana mlolongo wa matukio ya utekaji, tuhuma dhidi ya maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa zilizoelezwa ndani ya Bunge mwaka kupitia Zitto na Bashe, vilevile tabia za watu kujivalisha uhusika bandia na kujifanya ni polisi au mashushushu wa usalama, hatari kubwa ipo kwa askari kanzu.

Mwananchi mwenye kufuatilia habari za matukio ya utekaji kwa ukaribu, anayeishi akizongwa na fikra kuhusu watu wasiojulikana. Akifuatwa na askari halali wa jeshi la polisi ambao hawajavaa sare, akiwatilia shaka atakuwa na kosa gani? Ikiwa kuna ambao walitii na kujikuta kwenye mikono ya watekaji?

Kuna askari wasiovaa sare lakini wanatembea na bunduki, mwananchi anaweza kuwatofautisha vipi na watekaji au majambazi? Akipiga mayowe ya wezi na wananchi wakianza kurusha mawe, yule mpiga moyowe kosa lake litakuwa lipi? Ni dhahiri atafanya hivyo kulinda usalama wake kutokana na hali halisi ya utekaji ilivyo.

Wapo askari hutembea na magari ya kiraia, nao huvaa kawaida na bunduki hubeba. Ikitokea wanamfuatilia mtu kwa tuhuma za uhalifu, wanamfikia na kumwamuru asimamishe gari. Akikataa kusimama au kwa hofu kwamba watu hao wanaweza kuwa watekaji, akiamua kuligonga gari lao ili kujinusuru, itakuwaje?

Izingatiwe kuwa mtu huyo ambaye anasimamishwa na polisi wasio na sare, anajua simulizi ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alivyofuatiliwa na gari nyeupe aina Nissan Patrol. Watu wenye bunduki waliokuwemo ndani yake wakamshambulia kwa risasi nyingi.

Wengine wanamiliki silaha za moto kihalali. Wanajua kuhusu utekaji na visa vyote vya watu wasiojulikana. Je, akisimamishwa na polisi wasio na sare, yeye akilini akawaza ni jamii ya watu wasiojulikana, kisha akatoa silaha yake na kuanza kujihami, italeta sura gani na mazingira ya sasa yanajaza hofu?

Siku moja nilishuhudia gari dogo, likigonga daladala Eicher kwa nyuma eneo Bondeni, Mbezi Beach, Dar es Salaam. Lile gari dogo lilikuwa na kasi sana. Bila shaka lilikuwa linawahi tukio. Ndani yake kulikuwa na watu waliovaa kiraia lakini wana bunduki. Dereva na kondakta walipolifuata lile gari dogo kuomba waelewane kwa sababu wao ndiyo waligonga, waligoma.

Bahati iliyokuwapo ni kwamba gari lile dogo liliharibika sana, kwa hiyo haikuwezekana kuliondoa. Watu kwenye daladala na mashuhuda wengine wakawa wanasema watu hao ni polisi, wengine wakatilia shaka kwamba inawezekana ndiyo hao watu wasiojulikana. Hofu imeshakuwa kubwa.

Hofu hiyo ndiyo ambayo inaleta wasiwasi kuhusu usalama wa askari kanzu. Ni kwa namna gani itakuwa rahisi kueleweka kuwa wao si jamii ya watu wasiojulikana ikiwa wananchi wataanza kuwatuhumu na kuwashambulia? Askari wanahitaji angalizo kubwa la kikazi kipindi hiki.