UCHAMBUZI: Ya Lissu na mnara wa Babeli kila mtu ananena lake

Takribani mwezi mmoja sasa, habari zinazogonga vichwa vya watu ni Tundu Lissu. Bahati mbaya sana suala lake limepata wasemaji wengi hata balozi wa nyumba kumi naye anajitutumua kumjibu.

Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki, ametuchanganya tulio wengi. Kila mmoja anajitwika jukumu la kumjibu lakini baadhi ya wanaojibu ndio kabisa wanaharibu.

Wengi hatujasahau kuwa Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 38 akitoka kikaoni bungeni Dodoma, na kati ya hizo, risasi 16 ziliingia mwilini kwake.

Kwa zaidi ya mwaka amekuwa kitandani Nairobi Kenya na baadaye Ubelgiji, akipatiwa matibabu ya kuokoa maisha yake na amefanyiwa upasuaji mara 22.

Ndiyo, Lissu sasa amepata nafuu na kazi yake kubwa tunayoiona anaifanya ni kuzunguka nchi za Magharibi hususan Marekani, Uingereza na Ujerumani, kuelezea nini kilimtokea Septemba 7, 2017 na baada ya hapo.

Hapa ndipo shughuli ilipoanzia kwani yale anayoyazungumza huko ughaibuni, akihoji mustakabali wa uchunguzi wa shambulio dhidi yake na gharama za matibabu yake, ndiyo mambo ambayo yameifanya Tanzania leo kuimba Lissu, Lissu, Lissu.

Katika vyombo vya habari vya magharibi, Lissu ametoa hoja kubwa tatu, moja ni kutohojiwa kwa mtu hata mmoja tangu ashambuliwe, kuondolewa kwa walinzi na kuondolewa kwa kamera za CCTV.

Mengine ni pamoja na Bunge kutogharamia matibabu yake licha ya sheria kuahidi hivyo, kushamiri kwa ukiukwaji wa haki za binadamu nchini na kuzorota kwa shughuli za kisiasa kwa vyama vya siasa.

Madai haya mazito yalipaswa kujibiwa na mamlaka zenye weledi wa kujibu na si kila mtu kuanzia makada wa CCM, wanaharakati wenye nasaba na CCM, wakuu wa wilaya na hata raia wa kawaida.

Tunafanya makosa makubwa sana kama nchi, kumuachia kila mtu anayejisikia kujibu mambo yanayohusu jinai, wakati sote tunafahamu chombo chenye dhamana ya suala hili ni Jeshi la Polisi. Nilitarajia kwa suala hili la kutohojiwa kwa mtu yoyote, kuondolewa walinzi na CCTV, lingejibiwa na ama Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) au mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya Jinai (DCI) na si kufanya kila jambo la kisiasa.

Kuwaachia watu wasio na weledi wa uchunguzi kuzungumza kuna madhara makubwa na pengine kunaweza kutokea upotoshaji au kuongeza mkanganyiko na chuki kwenye jamii juu ya tukio hili.

Mathalan, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ambaye si mtendaji bali anashughulikia sera, kueleza nyumba wanazokaa viongozi wa Serikali Dodoma hakuna CCTV, imeacha watu vinywa wazi.

Saa chache tu baada ya kuongea haya, katika mitandao ya kijamii kunasambaa taarifa ya polisi ya Septemba 2017 ikieleza kuwa wamepata hadi picha za CCTV. Lugola anaifanya jamii ione kuna jambo nyuma yake.

Hii inakumbusha kisa cha mnara wa Babeli katika vitabu vitakatifu, limetufanya tupoteane na kila mmoja anajibu kwa maoni yake. Wengine wanapojibu ndio wanazidisha utata kuliko kuisaidia Serikali.

Tuviachie vyombo vyenye weledi kujibu hoja za Lissu kuliko kupiga siasa.