Yajue mahitaji ya kuku wakati wa joto

Shughuli za kilimo na ufugaji zinategemea kwa kiwango kikubwa hali ya hewa ya mahala husika.

Zipo shemu zenye hali ya mvua nyingi kwa kipindi kirefu au baadhi ya sehemu hupokea vipindi vya mvua zaidi ya mara moja kwa mwaka, huku nyingine mvua hunyesha kwa msimu mmoja.

Tofauti hizi za kimazingira huleta tofauti pia katika shughuli za wakulima na wafugaji. Sehemu zinazopata mvua nyingi huambatana na shughuli nyingi za kilimo zaidi kuliko ufugaji. Sehemu zinazopata mvua kidogo hujishughulisha zaidi na ufugaji kuliko kilimo au vyote kwa pamoja.

Makala haya yanajadili zaidi juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabia ya nchi katika maeneo ya joto kwa sasa. Hali ya hewa ina mchango mkubwa katika uzalishaji wa mazao na mifugo.

Japo mifugo sio kitu kinachohitaji kunyeshewa mvua kama mazao, lakini hali ya joto au ubaridi hubadilisha mfumo wa matumizi ya chakula kwenye miili ya mifugo.

Wakati wa joto la kawaida mifugo hukua na kuzalisha vizuri bila kuhitaji ubunifu sana. Hii ni kwa sababu mifugo hutumia nguvu ya kawaida kujikimu na mazingira hivyo nguvu nyingine ya chakula inayobaki huenda kufanya shughuli za ukuaji na uzalishaji.

Kwa upande mwingine, wakati wa baridi mifugo huhitaji nguvu nyingi kukabiliana na baridi kutunza joto la mwili na mwili kufanya shughuli za ukuaji na uzalishaji. Wakati wa baridi mifugo huhitaji chakula kingingi pia hupata njaa na hamu ya kula sana.

Wakati wa joto sana joto la mwili hupandishwa na hali ya hewa ya mazingira husika na kusababisha mifugo kutafuta namna ya kupoza miili yao. Hali hii ikitokea mifugo huwa na tabia kinyume na tabia wakati wa baridi.

Wakati wa baridi mifugo hupenda kula lakini wakati wa joto hususia chakula na kupendelea kunywa maji kila wakati ili kupoza mwili.

Chakula hupandisha joto la miili ya mifugo, hivyo ni wakati mzuri wafugaji kutazama mabadiliko ya hali ya hewa na kugundua huduma inayohitajika kwa kuku na mifugo wengine.

Wakati wa joto ukuaji na uzalishaji wa kuku hupungua kutokana na kunywa maji zaidi badala ya kula chakula na kujenga mwili. Utaona wafugaji wanaofuga kuku wa nyama na mayai wakilalamika juu ya kuku wao kushindwa kukua haraka kama ilivyokuwa wakati wa joto la kawaida.

Pia, utasikia wengi wakilalamikia kuku kulowesha mabanda na kuanza kutuhumu chakula au mbegu ya kuku waliochukua kuwa sio nzuri na mengine.

Lakini je, umeangalia hali ya hewa katika sehemu unayofugia? Bila shaka wafugaji wengi wa kuku hawajui kwamba joto na baridi huathiri mifugo.

Kuloa kwa banda au kutokua kwa kuku au kutozalisha vizuri kama joto la mazingira liko juu ni jambo la kawaida. Joto kali husababisha kuku kunywa maji mengi na kujisaidia majimaji ambayo watu wengi husema kuku wanaharisha na kulowesha banda.

Nini ufanye mfugaji?

Kwanza, tambua mabadiliko ya hali ya hewa na tabia za kuku wako.

Pili, wakati wa joto lisha kuku chakula kingi mapema asubuhi jua halijachemka na jioni sana jua limepoa na wakati wa usiku ubaridi ukiwa umetawala.

Tatu, wape kuku vitamini mara kwa mara ili kushawishi ulaji wa chakula na kupunguza upotevu wa maji mwilini wakati wa joto.

Nne, fungua madirisha ili hewa ipite kwa wingi au punguza idadi ya kuku bandani angalau robo ya idadi ya kuku unayoweka wakati wa joto la kawaida. Tano, tumia chakula bora kiasi cha kuwafanya kuku wasipate upungufu wowote kutokana na hali hiyo.