Ziara ya JPM inatufundisha makubwa

Sunday September 9 2018

 

Rais John Magufuli anaendelea na ziara yake maalumu katika baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa. Ziara hii imezidi kutufumbua macho juu ya masuala ya wananchi kukosa mawasiliano mazuri na viongozi wa ngazi za chini, au kukosekana kwa uwajibikaji kati ya wananchi na viongozi wa ngazi ya chini.

Ziara hii inatuonyesha changamoto za utendaji wa Serikali katika ngazi za chini na kudhihirisha kuwa watendaji na watumishi wengi wanashindwa kuendana na kasi ya Rais ya kushughulikia matatizo ya wananchi.

Ziara hii inamfanya Rais akutane na matatizo ambayo yamekuwa sugu na kudharauliwa au kutupwa na watendaji wake, matokeo yake anafika eneo husika anakutana na mambo yaleyale yaliyowahi kuripotiwa kwa viongozi wa chini na hayakufanyiwa kazi.

Katika wilaya ya Bunda mathalani, Rais amekutana na kikongwe aliyeporwa kiwanja, kesi yake ikatatuliwa na Waziri Lukuvi lakini Kamishna wa Ardhi ambaye yuko chini ya Lukuvi akashindwa kuchukua hatua ili kutekeleza maagizo ya waziri, kilichotokea ni jambo hili kurejea kwa Rais papohapo akampigia simu waziri.

Watendaji na watumishi

Watendaji na watumishi wengi wa serikali wanafanya kazi kwa mazoea kuliko kuendana na wakati au kasi ya dunia ya sasa. Uzito huu wa watumishi na watendaji nyakati zingine siyo wa makusudi, ni uzito unaotokana na mazoea.

Masuala mengi ambayo Rais anakutana nayo kwenye ziara zake, kama nilivyowahi kusema wakati anafanya ziara ya Iringa mwaka huu, ni masuala ambayo yalipaswa kuwa yameshatatuliwa kwa uhakika na watendaji wa chini.

Bahati mbaya baadhi ya watendaji na watumishi aidha hawajiamini au wanaishiwa mbinu za kupambana na utatuzi wa matatizo kwa njia za kisasa ambazo kwa kawaida huendana na kasi.

Wilayani Serengeti, Rais amesema kidogo angelimuondoa kazini mkuu wa wilaya hiyo kwa sababu alishindwa kutatua tatizo la ardhi la kikongwe mmoja ambaye ana ulemavu wa macho na ambaye alilifikisha suala lake kwa mkuu huyo wa wilaya lakini hakulifanyia kazi au hakulikamilisha.

Hii ni dalili ya namna ambavyo Rais anatwishwa mizigo mizito, inampasa aanze kushughulikia masuala ambayo yanastahili kushughulikiwa na watendaji wake ambao kila siku wanaishi na wananchi.

Iko haja ya kujenga mitizamo mipya kwa watumishi na watendaji wetu wa Serikali, iko haja ya kuhuisha mifumo yetu ya utunzaji kumbukumbu ili kufanya kila jambo linaloripotiwa kwenye ofisi yoyote ile, liweze kuchorewa chati ya utekelezaji au ufuatiliaji wa jambo hilo kitaalamu.

Iko haja ya kuwekeza kwenye mafunzo ya ziada kwa watumishi, hasa kwenye eneo la huduma kwa mteja na utengenezaji wa chati za ufuatiliaji wa matatizo yaliyoripotiwa, mifumo ya chati hizi itapaswa kuwekwa kwenye kompyuta na kufanya kila idara ya Serikali inayotaka kujua jambo fulani lilikoishia, iweze kufuatilia katika mifumo hiyo na kuliendeleza suala hilo kutokea hapo. Tusipochukua hatua hizo na zingine tutamgeuza Rais kuwa mtatuzi wa kila tatizo la nchi yetu wakati ana wawakilishi kila mahali.

Ufujaji wa fedha

Ziara hii ya Rais imeonesha pia ya kwamba, pamoja na juhudi zake na Serikali yake kusimamia fedha kwa nidhamu kukienda sambamba na kupambana na ufujaji wa fedha, jambo ambalo kwa sasa halibishaniwi tena, juhudi hizo huko mikoani na wilayani zinahujumiwa kwa baadhi ya matukio ya ufujaji wa fedha unaofanywa kwa ushirika wa baadhi ya watumishi na watendaji wa umma na watu wengine walio na mamlaka ya kijamii, kiuchumi au njia zingine.

Kama ufujaji huu si wa sasa basi umewahi kufanywa kipindi cha awamu zilizopita na unaendelea kuwaathiri wananchi lakini watendaji wapya wa serikali kwenye wilaya na mikoa hawauchukulii hatua na kuwawajibisha waliokwamisha au kusababisha ufujaji utokee.

Mara kadhaa Rais alipowahoji watendaji juu ya miradi fulani yenye utata, baadhi ya watumishi au watendaji muhimu wameishia kupiga blabla, kitu chenye maana kuwa wao wenyewe au wamehusika na ufujaji huo, ama hawana taarifa zozote kuuhusu. Yote mawili ni hatari sana.

Eneo mahsusi

Hili ni eneo mahsusi kwa sababu lisiposhughulikiwa mianya ya ufujaji wa fedha za umma itatamalaki na juhudi za Rais za kupambana na rushwa na ufisadi zitatiwa madoa.

Ni muhimu watumishi na watendaji wa serikali kwenye ngazi za mikoa na wilaya wakakumbushwa wajibu wao wa kulinda fedha za umma kwa njia ya wao wenyewe kuwa na taarifa ya uhakika ya miradi mbalimbali inayohusu umma hata kama miradi hiyo inatokana na ubia kati ya Serikali au taasisi zake na mwekezaji.

Ufujaji wa fedha za umma umekuwa ni sababu kubwa inayopelekea shughuli za maendeleo kukwama barani Afrika. Na hapa tunaweza kutumia mfano mzuri unaotoka kwenye moja ya hotuba za Mwalimu Nyerere wakati akifananisha wizi wa nchi zilizoendelea kama India dhidi ya wizi wa Afrika.

Mwalimu Nyerere anasema, ukiwapa fedha zinazolingana wataalamu wa ujenzi wa barabara wa India dhidi ya wale wa Tanzania, wale wa India walau watajenga barabara husika hata kama ni kwa chini ya kiwango. Mwalimu Nyerere akasisitiza kuwa fedha hizohizo ukimpa Mwafrika, hata barabara unaweza kutoiona kabisa na fedha zikaliwa.

Ujenzi wa taasisi imara

Mfano huu usichukuliwe kama kuwakosea nidhamu watu weusi dhidi ya watu wa rangi au nasaba zingine. Mfano huu unatuonyesha ni namna gani ambavyo nchi za Afrika zimo hatarini kuendelea kuporwa rasilimali na uwezo wake, na waporaji wakiwa ni watu wachache wenye dhamana ya madaraka au fedha. Kwa nchi kama ya kwetu, kusingekuwa na Rais kama Magufuli hivi sasa, fedha nyingi zingepotelea mikononi mwa watu wachache.

Hata hivyo, tunayo hatari kubwa mbeleni, Rais Magufuli akimaliza muda wake na kuondoka madarakani, vipi tukipata Rais mwingine asiye na uthubutu wa kupambana na rushwa na ufisadi? Hapa ndipo taifa letu linapaswa kujielekeza kwa muda huu, kwenye kutafuta suluhu ya kudumu ambayo ni ujenzi wa mifumo imara ya kupambana na rushwa, ufisadi na ufujaji wa fedha za umma.

Tutumie “Magufuli Model” (Mtindo wa Rais Magufuli) wa kupambana na ufujaji na kuunasibisha na mifumo na mikakati yetu ya kudumu ya kupambana na tatizo hilo.

Kubadilisha mitizamo

Ujenzi wa mifumo hiyo unaanza kwa kubadilisha kabisa mitizamo ya watumishi wa umma na watendaji na watu wengine juu ya masuala ya ulinzi wa rasilimali za nchi yetu zikiwemo fedha na miradi yake.

Ubadilishaji huo unapaswa kuendana na mabadiliko muhimu ya kisheria na kikanuni ambayo yatatoa nguvu kubwa sana kwa taasisi huru za ngazi za chini na idara za kiserikali za kitaifa ambavyo vitaendelea kuwa na mamlaka makubwa juu ya uchunguzaji na uchukuaji hatua wa masuala mbalimbali ambayo yanahisiwa kuwa na ufujaji au upigaji wa fedha.

Yako masuala ambayo Rais Magufuli anayashughulikia kwenye ziara yake na ukiyachunguza sana unagundua kuwa yalipaswa kuwa yameshashughulikiwa ipasavyo na Takukuru, Polisi, mabaraza ya madiwani, watendaji wa halmashauri, wilaya au mikoa.

Na mengine unakuta yalipaswa kuwa yameshashughulikiwa na wizara, lakini sote tunaona kuwa Rais anafika mahali ndipo watendaji wake wanaanza kukimbizana kuyatatua, au wakiona Rais ana ziara mkoani kwao ndipo wanaanza kupita mitaani kutatua changamoto zilizokuwa zimelala ili tu Rais anapofika waweze kumpa majibu kuwa wamekuwa wakizishughulikia kwa ushahidi. Ujanjaujanja wa namna hii hauwezi kulisaidia taifa.

Watendaji wasimsubiri Rais

Nelson Mandela aliwahi kusema, “Ili uwe kiongozi mzuri ni lazima uwe mkweli kwako na kwa wananchi wako.” Viongozi wetu wanaomsaidia Rais lazima waiishi kauli hii, wawe wakweli kwao binafsi na kwa wananchi wao, waiishi kweli kwenye maeneo yao na matendo yao, wasisubiri ziara ya Rais ndipo wakaanza kukimbizana.

Kama kwa mfano mkoa wa Kilimanjaro una changamoto za maji leo mwaka 2018, changamoto hizo zisakamwe na kuondolewa leo, asisubiriwe Rais atembelee Kilimanjaro mwaka 2020 mathalani, ndipo maelezo ya matatizo ya maji yaanze kushughulikiwa.

Kama kuna jambo ambalo Rais wetu atalisaidia taifa letu, ni kutumia mtindo wake wa uongozi kujenga mifumo inayojitegemea, ili siku akiondoka madarakani anaowarithisha nchi waendelee kukimbia kwa kasi aliyokuwa nayo.

Ninachotamani kukiona ni siku Magufuli akiondoka; tusije kuanza upya tena, tukarudishwa enzi za watumishi na watendaji wa serikali kugeuza ofisi na mali za umma kama za binafsi. Ikiwa JPM ametuondoa kwenye enzi hizo basi na atusaidie tusirudi kabisa.

Julius Mtatiro ni mtafiti na mchambuzi wa utendaji wa Serikali barani Afrika; ni mwanasheria, mfasiri na mtaalamu mshauri wa miradi, utawala na sera. Simu: +255787536759 Barua Pepe; [email protected])

Advertisement