Zifahamu mbinu bora katika malezi

Sunday February 10 2019

 

By Dk Chris Mauki

Malezi yanawezekana kutolewa kwa watoto wetu au ndugu zetu au hata wa marafiki. Hakuna mzazi au mlezi mwenye kusudi au atakayefurahia kuona mtoto wake anaharibika kimalezi.

Kila mmoja ana hamu ya kuona yale anayoyatamani kwa mtoto au watoto wake yanatimia, ikiwemo malezi mazuri, heshima, elimu bora, kazi bora na hata kupata familia bora.

Mzazi au mlezi ana kiu na ndoto ya kuona anamwandaa mtoto wake kuwa baba au mama bora katika familia yake ya kesho.

Jambo lolote linalotokea na kuonekana kutaka kuharibu ndoto au maono haya ya mzazi huumiza moyo wa mzazi na hata kumkatisha tamaa.

Hii husababisha uhusiano wa baadhi ya watoto na wazazi wao kufa au kulegalega, watoto wengine wametengwa au kufukuzwa majumbani mwao.

Vitu vinavyoharibu uhusiano wa wazazi na watoto wao, na kuwakatisha tamaa kabisa wazazi ni baadhi ya tabia kama vile, utovu wa nidhamu, kujiingiza katika mapenzi, kupata ujauzito, ulevi, uvutaji wa sigara, bangi au dawa za kulevya, ugomvi, utoro wa shule, uvivu na mengine mengi.

Jinsi miaka inavyozidi kwenda na jamii inabadilika ndivyo kazi ya malezi inavyoonekana kuwa ngumu zaidi. Kila mzazi analalamika kuwa watoto wanakuwa mzigo unaoshindikana kubeba mara nyingine.

Kwa uzoefu kama mshauri wa kisaikolojia nina kesi tele za watoto walioshindikana na wale wenye tabia zinazosumbua wazazi au walezi wao.

Hii inaonyesha kuwa tatizo hili ni dhahiri. Tofauti kubwa na miaka ya nyuma wakati wazazi wetu wanakua na kusoma maisha yalikuwa tofauti. Sasa hivi dunia inabadilika kwa kasi kila siku, vyanzo vya taarifa vinaongezeka, vikitoa taarifa nzuri na mbaya, wakati huohuo wazazi hawataki kubadilika, wakiwa na mawazo ya zamani na kulinganisha enzi zao na hizi. Wengi wakionekana kushangaa tofauti wazionazo baina ya vizazi hivi viwili.

Wazazi wengi bado wanaona aibu kuwa wazi kutoa baadhi ya taarifa na msimamo wao kwa watoto wao wakidhani kuwa muda bado au kuona aibu kufanya hivyo mapema. Kumbe jinsi wanavyochelewa ndivyo ulimwengu unawapa taarifa potofu juu ya vitu kama uhusiano, mapenzi, ngono, Ukimwi na magonjwa ya zinaa.

Mambo haya mengi na tofauti hizi nyingi zinachangiwa na jinsi watoto hawa wanavyolelewa na mbinu za malezi ambazo wazazi wamekuwa wakizitumia.

Mara nyingi nimekuwa nikisema kuwa suala si mzazi au wazazi kulazimisha watoto kuwa na nidhamu, suala ni njia au mbinu gani za kujenga nidhamu zinatumika. Wengi wamewaharibu watoto wao wenyewe pasipo kujua na wakati huo wao wakidhani wanawajenga na kuwaadabisha.

Mtiririko huu wa aina za malezi utakusadia kujitambua na ikiwezekana kubadilika, kama wewe ni mlezi sasa itakusaidia kubadilisha mtazamo wako kuhusu malezi na kama sio mlezi basi itakuandaa vema kwa mlezi bora baadae. Nia ya mbinu hizi za malezi ni kurekebisha au kujenga tabia za watoto na kuwaelekeza katika mwelekeo fulani. Tatizo ni kwamba yako makosa mengi katika malezi yanayofanywa na wazazi na badala yake kuleta uharibifu kwa tabia za watoto wao.

Advertisement