Zingatia haya unapotoa ‘home work’ kwa mtoto

Suala la umuhimu wa kazi za nyumbani kwa watoto wa umri mdogo limekuwa mjadala mkubwa miongoni mwa wazazi. Nawafahamu wanataaluma kadhaa wanaotafiti kujua undani wa mazoea haya yanayoendelea kushika kasi hususani kwenye shule binafsi za msingi.

Richard Walker na Mike Horsley waandishi wa kitabu cha ‘Reforming Homework’ wanafikiri utamaduni huu hauna tija. Hoja yao kubwa ni kwamba walimu wengi wanazitumia kazi hizi kuwaridhisha wazazi kwamba wanafanya kazi na matokeo yake wanawanyima watoto muda wa kupumzisha akili baada ya shughuli nyingi za shule. Kazi za nyumbani zinamlazimisha mtoto kutumia muda wa nyumbani kukimbizana na maswali ambayo mwalimu angeweza kuyashughulikia ndani ya kipindi cha darasani.

Pamoja na changamoto hizo, hatuwezi kupendekeza ‘homework’ zipigwe marufuku kwa madarasa ya awali kama ilivyofanyika katika baadhi ya nchi. Tunapendekeza namna nzuri ya kuhakikisha kazi hizi zinakuwa na tija kwa mwanafunzi. Kanuni tatu za kuzingatia.

Kwanza, ushirikishwaji wa mtoto mwenyewe. Watoto hujifunza vizuri zaidi unapowashirikisha kufanya kazi kwa mikono yao wenyewe lakini pia zenye kuwapa changamoto ya kupata ufumbuzi wa tatizo fulani. Mpe mtoto kazi rahisi zitakazomfanya ajione anatatua tatizo. Kwa mfano, kama unataka mtoto atambue herufi Aa, mtake aende nyumbani akatafute vifaa vinavyoanzia na Aa badala ya kumfanya arudie rudie nyimbo alizokuwa anaimba shuleni. Kwa kufanya hivyo unakuwa umemshirikisha kuhusianisha kile alichokifunza shuleni na mazingira yake ya nyumbani moja kwa moja.

Pili ni ushiriki wa familia yake. Watafiti mbalimbali wanatuambia watoto ambao wazazi wao wanahusika moja kwa moja na mchakato wa ujifunzaji wa watoto wao, mara nyingi, hufanya vizuri shuleni. Kwa kuzingatia ukweli huu, mpe mtoto kazi ambazo kwa namna moja au nyingine atashirikiana na wazazi na ndugu zake waliopo nyumbani.

Changamoto, hata hivyo, ni uwezekano wa baadhi ya wazazi kutokuwa na uelewa wa kile ambacho watoto wao wanajifunza shuleni. Nadhani mwalimu atoe kazi zenye kuhusisha mambo ya kawaida ambayo hata mzazi wa kawaida anaweza kuwa na uelewa nayo.

Mfano kama somo linahusu usafi wa mazingira, mwuulize maswali anayoweza kupata uzoefu wa wazazi wake na kisha uheshimu maoni ya mzazi. Kufanya hivi kunamsaidia mtoto kuyaona masomo yake kupitia maisha yake ya kila siku.

Tatu, zingatia muda na uhalisia. Mtoto anahitaji muda wa kucheza, kupumzika, kukaa na wanafamilia wake na shughuli nyingine ambazo, endapo zitapangiliwa vizuri, zinamsaidia kufurahia utoto wake.

Kwa kuzingatia hilo, usimpe mtoto kazi zinazodai zaidi ya dakika 15 kuzikamilisha. Kumbuka lengo kuu la ‘homework’ ni kumsaidia kwenda hatua moja mbele ya kile alichojifunza darasani.