Zitto alivyomnasa Maalim Seif kujiunga ACT-Wazalendo

Muktasari:

  • Wakati huo CUF ilikuwa kwenye mgogoro wa uongozi. Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba alijiuzulu kwa kile alichodai ni kupinga Ukawa kumsimamisha Edward Lowassa aliyetoka CCM kuwa mgombea urais lakini wenzake CUF, kumuunga mkono Lowassa.

Uchaguzi Mkuu 2015, CUF chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu, Seif Sharif Hamad, ilikuwa katika muungano wa vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) – Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD.

Chama cha ACT-Wazalendo kinachoongozwa na Zitto Kabwe kiliomba kujiunga Ukawa lakini kilikataliwa. Kulikuwa na sababu mbili kwa Ukawa kuikataa ACT.

Sababu ya kwanza ni Chadema. Uongozi wa juu wa ACT na ambao uliasisi chama hicho, asilimia 90 walitoka Chadema baada ya migogoro na kufukuzana. Zitto alikuwa naibu katibu mkuu wa Chadema, wakagombana, mgogoro ukafika mahakamani, akafukuzwa.

Aliyekuwa katibu mkuu wa ACT, Samson Mwigamba na mshauri wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo walifukuzwa Chadema. Baada ya hapo waliiasisi ACT na sasa wapo CCM. Na watu wengine katika safu ya uongozi, kwa sehemu kubwa walitoka Chadema. Hivyo, kuikaribisha ACT Ukawa ilikuwa kuikwaza Chadema, chama kilichokuwa na msuli mkubwa zaidi ndani ya Ukawa.

Sababu ya pili ni kile ambacho kinaonekana ni propaganda, hasa kutoka Chadema wakati wa uchaguzi 2015, kwamba ACT ni chama kilichopewa ufadhili na CCM ili kuvuruga nguvu ya upinzani. Kwa hiyo, ACT hakikuwa chama chenye kuaminika Ukawa.

Wakati huo CUF ilikuwa kwenye mgogoro wa uongozi. Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba alijiuzulu kwa kile alichodai ni kupinga Ukawa kumsimamisha Edward Lowassa aliyetoka CCM kuwa mgombea urais lakini wenzake CUF, kumuunga mkono Lowassa.

Baada ya kujiuzulu CUF, Lipumba alitimkia Rwanda aliposema alikwenda kufanya utafiti na aliporudi, alihusishwa chinichini kuwa na ushirika na Zitto na ACT. Maneno hayo yalikuzwa na mikutano ya viongozi hao Mtwara na Lindi, kipindi Zitto akiwa kwenye mgogoro na Chadema, huku kesi ya uanachama wake ikiwa mahakamani.

Wakati malumbano ya uongozi yanaanza CUF, hasa baada Lipumba kufuta kujiuzulu na kutaka aendelee na uenyekiti wake, aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julius Mtatiro alijibishana mtandaoni na Profesa Kitila, wakati huo alikuwa bado ACT.

Kitila alijenga hoja ya kushauri maridhiano kati ya upande wa Lipumba na Seif, lakini Mtatiro alimjibu: “Kitila wewe ni mwalimu wangu. Tunajua kila kitu na vikao vyenu na Lipumba mwaka 2015. Usitake niyaseme yote hapa.”

Kwa vile hoja hiyo ilitolewa na Mtatiro ambaye alikuwa timu ya Seif, ni wazi hicho ni kipimo kingine kwamba wakati wote, kabla na baada ya Uchaguzi 2015, Zitto alionekana ni kijana wa Lipumba, hivyo ACT kwenye macho ya timu ya Seif, ilionekana kuwa chama chenye kumuunga mkono Lipumba katika mgogoro wa uongozi uliokuwapo.

Upepo ulivyobadilika

Tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu 2015, Zitto alijipambanua bila kuchoka kuhusu kupigia kelele kile anachoamini kuwa Seif alishinda Uchaguzi wa Rais Zanzibar Oktoba 25, 2015, kisha matokeo kufutwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salim, kisha uchaguzi kurudiwa Machi 20, 2016.

Zilikuwapo pia nyakati za Zitto kuelewana kisha kupishana kauli na wenzake katika vyama vya upinzani. Hata hivyo, hakuna wakati ambao Zitto amekuwa mkali dhidi ya CCM na Serikali, huku akibeba sauti halisi ya upinzani, kama baada ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kupigwa risasi Septemba 7, 2017.

Tangu wakati huo, Zitto amekuwa sauti inayopigia kelele utawala bora. Akipaza sauti kuhusu unyama aliotendewa Lissu. Akiwasemea Wazanzibari kuhusu anachoamini kuwa Seif alipaswa kutangazwa mshindi wa urais mwaka 2015. Akikosoa sera za uchumi na kuchambua hali ya uchumi.

Hayo ndiyo mambo ambayo mwaka jana, mmoja wa wasaidizi wa Seif, Jussa Ismail aliandika Facebook na kumpa sifa nyingi Zitto, kwamba ni mwanasiasa mahiri na mwanamageuzi mkomavu. Hicho kilikuwa kielelezo kuwa timu Seif walishaweka imani yao kwa Zitto.

Imani hiyo kwa Zitto si kwa timu ya Seif peke, hata Chadema mara nyingi wameonekana kusimama pamoja na Zitto.

Wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alimtaja Zitto kuwa sehemu ya waliompa faraja yeye na mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), Esther Matiko walipokuwa mahabusu kwa zaidi ya siku 100.

Alipokuwa anajibu maswali ya waandishi wa habari, waliohoji ni kwa nini wameamua ACT na siyo chama kingine, Seif alisema, kabla ya kufanya uamuzi walizungumza na vyama mbalimbali vya upinzani. Vyote vilikuwa tayari kuwapokea, kila chama kikawa na masharti yake, ila ACT walikuwa na masharti nafuu kwao.

Hapohapo ikumbukwe kuwa Desemba mwaka jana, Seif aliitisha mkutano Zanzibar wa vyama takriban 10. Baada ya mkutano huo, walitoa Azimio hilo na maudhui yake.

Rais wa 32 wa Marekani, Franklin Roosevelt aliwahi kusema: “Katika siasa hakuna kinachotokea kama ajali. Kikitokea, unaweza kupatia kwamba ndivyo kilipangwa.”

Sasa rejea jibu la Seif kuwa alikutana na vyama mbalimbali kuuliza uwezekano wa kuwapokea endapo mahakama ingeamua Lipumba ni mwenyekiti halali wa CUF.

Ongeza kuwa Seif ndiye aliitisha mkutano Zanzibar na kuunda Azimio la Zanzibar. Ona namna Zitto alivyolibeba. Utaona kuwa alijenga ushawishi mkubwa kwa Seif kuliko vyama vingine.

Ipo hoja kuhusu Chadema, mambo mawili unaweza kupatia. Mosi, changamoto ya mgawo wa majimbo Ukawa mwaka 2015. CUF walilalamika kuchezewa faulo na Chadema, ingawa hayakuwa malalamiko rasmi. Pili, Seif bila shaka aliona angejiunga Chadema angemezwa, ameona bora wajiunge ACT ambako wamepokelewa kwa uzito na shukurani kubwa.