UCHAMBUZI: Zitto naye amelalamika, polisi wachukue hatua

Januari 5, mwaka huu, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe alibandika malalamiko yake kwenye akaunti yake ya Twitter kuhusu kuwapo mpango wa kumdhuru.

Zitto aliandika akitumia Kiingereza ya pili Kiswahili, kwamba kuna mpango huo wenye maudhui ya “Vita ya Mwisho Kuleta Nidhamu Kamili.”

Hoja si Zitto kulalamika, bali kuhoji kwa nini kunakosekana uharaka wa kudhibiti vitisho au hujuma za kuichafua nchi?

Septemba 7, mwaka juzi, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana, ikiwa ni siku chache baada ya kulalamika kuhusu kufuatwafuatwa.

Wakati Zitto akilalamika Twitter, Lissu alifanya mkutano wa waandishi wa habari na kueleza jinsi alivyokuwa akifuatwafuatwa. Kilio chake hakikusikika. Alipigwa risasi na mpaka leo, ukiwa ni zaidi mwaka mmoja na hajapona.

Hii ni miaka miwili na miezi miwili tangu kada wa Chadema, Ben Saanane, atoweke Novemba 2016. Ben pia kabla ya kupotea, alitoa taarifa za vitisho lakini hakupewa msaada.

Je, kupotea kwake ni matokeo ya vitisho alivyokuwa anapokea? Waliompiga risasi Lissu, ndiyo haohao aliolalamika walikuwa wakimfuatilia? Polisi wangekuwa kwenye wakati mzuri wa kulizungumza kama wangeeleza wamefikia wapi katika upelelezi.

Ikiwa polisi hawatapuuza malalamiko ya Zitto, maana yake watakuwa wamejifunza kutokana na makosa yaliyotokea awali. Wakinyamaza hali inaweza kuwa yaleyale. Na ikiwa ni yaleyale, swali ni je, nini kinatafuta kwa nchi? Polisi wanapaswa kuwa macho na kufanyia kazi hata minong’ono. Sasa watu wanapaza sauti, tena ni viongozi wa wananchi, kisha malalamiko yao yanapuuzwa.

Jeshi la polisi lazima litambue kuwa usalama wa nchi unaweza kujaribiwa katika njia mbalimbali. Kuna watu wanaweza kushambulia wapinzani au kuwatisha ili kuipaka matope Serikali. Ni wajibu wa polisi kufanya kazi yake ili kuuweka ukweli katika mstari wake.

Mwaka 2015, alipofariki dunia Boris Nemtsov ambaye alikuwa mpinzani namba moja wa Rais Vladimir Putin, macho yote yalielekea kwa Putin kwamba ndiye mhusika mkuu.

Sababu ni kuwa Nemtsov alikuwa akijiandaa kutoa chapisho lenye kuonesha namna Putin alivyohusika na vita vya Ukraine, pia alikuwa ametoa jarida lenye kuonyesha namna rushwa ilivyokithiri kwenye Serikali ya Putin.

Baada ya Putin kuona anaandamwa kuhusu kifo cha Nemtsov, aliagiza vyombo vifanye kazi na kuhakikisha watuhumiwa wanakamatwa. Na kweli, wahusika wa mauaji ya Nemtsov walikamatwa.

Nadharia mbili kati ya tano zilizoandikwa na idara za usalama ni; Mosi, wapinzani wenyewe waliamua kumuua Nemtsov kwa lengo la kutaka ionekane ni kifo cha kisiasa.

Pili, kundi la pembeni lilitekeleza mauaji ili kusababisha mvutano kati ya wapinzani na Rais Putin, hivyo kuwafanya wananchi waone nchi yao si salama.

Ujumbe kutoka Urusi unaweka uzito kuhusu chuki za kisiasa na namna ambavyo watu wenye nia mbaya na nchi wanaweza kuharibu amani kwa kushambulia upande mmoja kati ya pande mbili zinazosuguana kisiasa.

Ilielezwa kuwa hata vyombo vya usalama, viliingiwa kigugumizi kuchunguza kifo cha Nemtsov, kwani ndani ya dola kulikuwa na hisia kuwa Putin ndiye alimuua. Baada ya Putin mwenyewe kuwaambia wachunguze, ndipo wakajiridhisha kwamba Rais si mhusika na walipopeleleza waliwapata wahusika.

Aliyekuwa Rais wa Ufilipino, Ferdinand Marcos alikufa anaapa kutohusika na kifo cha aliyekuwa mpinzani wake, Ninoy Aquino, lakini aliyemwelewa

Ninoy alipigwa risasi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Manila, Agosti 21, 1983, alipokuwa anarejea nyumbani kutokea Marekani alikokuwa kwa matibabu.

Tukio la Ufilipino linaelimisha kuwa mahali ambapo hakuna maelewano ya kisiasa kati ya watawala na wapinzani, inawekana kabisa kutokea mtu au kikundi cha watu na kuamua kuvuruga amani ya nchi. Polisi wasipuuze malalamiko ya Zitto.