Jifunze kugundua tabia za wafanyakazi

Kuna tabia zisizojificha. Tabia kama chuki, ugomvi, ubabe na uvivu. Mtu anapokuwa nazo unahitaji kufanya kazi ya ziada kuzibaini na kuchukua hatua stahiki.

Lakini zipo tabia nyingine zinazochukua muda mrefu kuzibaini. Wakati mwingine unaweza kuzigundua wakati tayari umeshaingia kwenye matatizo.

Hapa nakuonyesha baadhi ya makundi ya watu unaoweza kukutana nao kazini na namna ya kufanya nao kazi.

Mkamilifu aliyepitiliza

Huyu ni mfanyakazi anayejituma kutekeleza majukumu yake. Kwa kawaida ana shauku ya kuona matokeo yanakuwa vile anavyotaka; hawezi kuvumilia makosa yanayofanywa na mwingine.

Muda wake mwingi anautumia akifanya kazi kusudi afikie viwango vyake.

Tatizo la mfanyakazi wa kundi hili ni kutokuamini kuna mtu mwingine anaweza kufanya kazi kwa ubora anaoutaka yeye, kwa hiyo ni mgumu kukasimisha majukumu yake kwa wengine.

Akiwa kiongozi, ni aina ya mtu anayeweza kukufanya ukakosa pumzi kwa kukufuatilia. Moyo wake unapenda kuwadhibiti wengine, kuwanyima raha watu. Unapofanya naye kazi jua hutakaa umridhishe. Fanya unachoweza.

Muasi

Huyu ni mfanyakazi anayependa kuonekana yuko kinyume na wenye mamlaka. Siku zote atakuwa kinyume na uongozi na anaweza kufanya kitu chochote kuonyesha haheshimu taratibu za kazi, hasikilizi maazimio ya vikao na maagizo ya wakubwa wake, kwa sababu amani yake ni kuonekana anajitambua.

Mara nyingi tabia hii ya kupinga kila kitu kinachofanywa na wengine huenda sambamba na tabia ya kutokukubali kukosolewa.

Tabia hii ya kuthubutu kumpinga bosi wake humtengenezea umaarufu fulani kwa wenzake kazini. Kila anapopingana na wakubwa wake, wafanyakazi wengine, ambao kwa kawaida ni waoga humchukulia kama shujaa. Ni ushujaa huu unaomfanya awe mlevi wa malalamiko na kushutma kwa wakubwa wake kazini na wakati mwingine kusuka mipango ya kuwachafua au kuwaangusha.

Badala ya kumwelekeza cha kufanya au kumkosoa, mpe taarifa unayofikiri anaihitaji. Epuka kuwa sehemu ya mipangilio yake ya kuwachafua wengine.

Mwathirika

Kwa haraka haraka, huyu anaonekana kuwa mtu mwema, mwenye busara na anayejali hisia za watu wengine. Ingawa anaweza kuwa na huzuni hapa na pale, ni mtu mwenye bidii na unayeweza kufanya naye kazi vizuri na matokeo yakaonekana.

Tatizo lake ni kwamba anaumizwa mno na kila anachosikia au kuhisi wengine wanasema. Huyu ni mtu anayeweza kukosa amani na kazi kwa sababu tu bosi amesema kitu kwenye kikao. Kwake kila kinachosemwa kinamhusu yeye. Mara nyingi atajiona ni mtu asiyependwa na matokeo yake hujitenga na watu akijihisi ni mhanga wa mahusiano yake na watu.

Unapofanya kazi na mtu wa namna hii mtie moyo. Tambua kazi anayofanya na mhakikishie kuwa yeye ni mtu makini. Kuzungumzia pungufu wa watu mbele yake kunatafsiriwa kama kumsema.

Mpenda ‘drama’

Huyu ni mfanyakazi anayependa kuonekana na watu. Mwongeaji kupindukia na wakati mwingine hajui kuchagua kipi aseme wapi na kwa namna gani.

Ukiwa naye lazima ufurahi kwa sababu anajua kufurahisha. Upande wake mzuri ni kwamba unaweza kumkosoa hadharani, kesho asikumbuke kilichotokea.

Pamoja na uso wa bashasha, ukimsikiliza kwa makini unagundua wakati mwingine kicheko chake kinaficha mengi.

Moyo wake unaweza kuwa na ubaya ambao si rahisi kuubaini. Saa nyingine anakuwa mtu wa kusambaza maneno asiyo na uhakika nayo.

Mgundue mapema na usimpe nafasi ya kuwa karibu sana na wewe. Kama siyo lazima, epuka kumweleza mambo yako muhimu.

Mwota ndoto

Ukisimkiliza unaweza kufikiri umekutana na Bill Gates au Warren Buffet. Ni mtu anayefikiri na kuongelea mambo makubwa wakati mwingine yasiyotekelezeka. Mnapozungumzia mradi unaotakiwa kuukamilisha atakuonyesha namna gani mtafanikiwa na amejipanga kufanya nini. Wakati mwingine anaweza kuwa aina ya mtu anayependa kutangaza mafanikio yake hata kama ni kwa kutia chumvi.

Unahitaji umakini unapofanya kazi na mtu wa namna hii. Kwanza, usisikilize sana kile anachokisema kwa sababu mara nyingi hakimaanishi. Mnapopanga jambo jitahidi kuwa na mbadala wake. Lakini usikose amani kwa kuamini simulizi zake za mafanikio. Mengi hayana ukweli.

Mpenda raha

Huyu anajipenda kupindukia. Huvalia nadhifu kuliko wengine na hushindana na watu kuhusu vitu na nafasi. Kwake thamani ya kazi ni starehe. Wakati mwingine hushindwa kufanya kazi kwa ufasaha shauri ya kuweka mbele starehe.

Upo uwezekano pia akawa na uhusiano wa karibu na watu wa jinsia nyingine kwa lengo la kukidhi tamaa za mwili.

Kwake urafiki na mtu wa jinsi nyingine lazima uishie kwenye mapenzi. Akiwa kiongozi kazini hutumia nafasi yake kuwanyanyasa wengine kingono.

Kuwa makini unapofanya kazi naye. Tengeneza mipaka iliyo dhahiri na akufahamu misimamo yako.

Inaendelea

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano 0754870815, twitter: @bwaya