Kitwanga: Ni aibu Tanesco kutangaza kukata umeme

Thursday May 9 2019

 

By Julius Mnganga, Mwananchi [email protected]

Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga amesema ni aibu kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutangaza kukata umeme.

Amesema hayo wakati Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe akiwa ametangaza kuwa majaribio ya treni ya umeme katika kipande cha kwanza cha reli ya kisasa (SGR) yataanza karibuni.

Treni hiyo ya mwendokasi inayokwenda kwa kasi ya kilomita 160 kwa saa itafanya majaribio kati ya Dar es Salaam na Morogoro na usafarishaji wa abiria na mizigo utaanza rasmi Desemba.

Pi, wakati hayo yakiendelea, Serikali inaendelea kuhamasiaha ujenzi wa viwanda ili nchi ifikie uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, lakini changamoto ya umeme wa uhakika inaonekana ni tatizo.

Ni nadra umeme katika maeneo tofauti kutokatika kwa siku, hali inayosababisha maeneo mengi ya biashara kuwa na jenereta ili kukabiliana na tatizo la nishati hiyo muhimu.

Na hilo ndilo ambalo Kitwanga analiangalia zaidi.

Advertisement

“Tanesco haitakiwi kuridhika kutangaza kukata umeme. Badala yake wanatakiwa waumize vichwa kutafuta suluhu ya kudumu,” anasema Kitwanga, ambaye alikuwa waziri kwa takriban miaka sita, alipofanya mahojiano na Mwananchi nyumbani kwake jijini Dodoma.

“Ni aibu kwa Tanesco kutangaza kukatika kwa umeme. Ikiwezekana wafikirie miaka 50 au zaidi ijayo.

“Haya matangazo yao tarehe fulani, siku fulani umeme utakatika kuanzia muda fulani mpaka muda fulani tunayoyasikia hayapendezi. Tena huwa wanafanya hivi proudly (kwa kujiamini). Sasa hivi tuna viwanda halafu unakosa umeme... ni sawa na binadamu akose hewa.”

Anasema juhudi zinahitajika katika kupata umeme wenye uhakika.

Tayari Serikali imeanza mchakato wa ujenzi wa mradi wa umeme katika Mto Rufiji, maarufu kama Stigler’s Gorge utakaozalisha megawati 2,100.

Lakini Kitwanga anasema anaamini kiwango hicho cha umeme hakitoshi kwa kuwa kunahitajika kuzalisha walau megawati 5,000 kutokana na kwenye makaa ya mawe, gesi megawati 5,000 na vyanzo vingine kama upepo na jua megawati 5,000.

Mchanganyiko huo wa vyanzo mbalimbali, Kitwanga anasema, utasaidia kumaliza kero ya kukatika kwa umeme na kuwataka wataalamu wa wizara ya nishati kufikiri namna ya kupata vyanzo mbadala.

Kitwanga ambaye ni mbunge wa Misungwi anasema kuna mataifa, mfano Korea Kusini hawafahamu chochote kuhusu kukatika kwa umeme na wamefika hapo kutokana na uwezo wao wa kufikiri na kusimamia mipango waliyonayo.

“Nashauri kuwa na vyanzo vingi (vya umeme) ili kimoja kikisumbua unahamia kwenye kingine na isitokee umeme unakatika. Ni gharama zaidi kushusha uzalishaji viwandani kuliko kubadili chanzo cha umeme,” anasema naibu wziri huyo wa zamani wa nishati na madini.

Kukiwa na hazina ya zaidi ya futi trilioni 57.5 za ujazo za gesi asilia, baadhi ya viwanda vinavyotumia nishati hiyo havipati kiasi cha kutosha kukidhi mahitaji yao ya kila siku kufanikisha uzalishaji. Kutokana na hali hiyo, anasema baadhi ya viwanda vinavyotumia gesi hiyo vimepewa notisi ya kufungwa.

Licha ya upatikanaji usio wa uhakika, mbunge huyo alibainisha bei kubwa ya nishati hiyo nchini ikilinganishwa na ya soko la dunia lakini Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu anasema Serikali inazo taarifa hizo na inazifanyia kazi kuhakikisha wawekezaji hao wanaenelea na uzalishaji.

Miongoni mwa viwanda vinavyokabiliwa na uhaba huo wa gesi asilia ni cha Dangote kilichopo mkoani Lindi kilichounganishwa tangu Agosti mwaka jana na hadi sasa kinatumia kati ya futi milioni 15 hadi 20 za ujazo kwa siku pamoja na vingine vilivyopo mkoani Pwani.

Hii ni mara ya pili uzalishaji wa Kiwanda cha Dangote unatikiswa kutokana na kukosa umeme wa kutosha. Mwanzo hali hiyo ilipojitokeza hata kikasimamisha uzalishaji, Rais John Magufuli alikipa sehemu ya Mgodi wa Ngaka ili kichimbe mkaa wa mawe

Reli ya kisasa

Sehemu ya kwanza ya reli ya kisasa itakuwa na vituo sita ambavyo ni Dar es Salaam ambayo ni stesheni kubwa, Morogoro, Pugu, Soga, Ruvu na Ngerengere.

Vituo hivi vyote vitakuwa na mahitaji muhimu ya kibinadamu kama vile migahawa, huduma za benki, maegesho ya magari, maduka ya kisasa na sehemu za mapumziko.

Itakapokamilika, reli hii itafika mikoa ya Kigoma na Kagera hivyo kuiunganisha Bandari ya Dar es Salaam na nchi jirani na kuongeza biashara kati ya Afrika na dunia kupitia bandari hiyo.

Kitwanga anasema ili kuongeza tija ya reli hii ni lazima kuwe na vituo maalumu vya uwekezaji jirani na stesheni ili kuruhusu usafirishaji wa malighafi au bidhaa zitakazokuwa zinazalishwa.

“Uwekezaji uliofanywa hauwezi kurudishwa kwa nauli za abiria au gharama za kusafirisha mizigo.

“Ni lazima sekta ya viwanda ichangamke ili mzigo mkubwa zaidi usafirishwe. Faida za reli zitoke sekta nyingi nyinginezo,” anasema Kitwanga.

Licha ya viwanda vitakavyozalisha bidhaa tofauti, anasema mikakati enelevu inahitajika kuimarisha kilimo biashara.

Endapo sekta hiyo itawekewa mazingira mazuri, anasema SGR na Shirika la Ndege lililofufuliwa inawagusa waulima wengi zaidi watakaotumia miundombinu hiyo kusafirisha mazao yao pamoja na viuatilifu muhimu kwa gharama nafuu.

Hata mataifa yaliyoendelea zaidi ambako wanatreni zinazokimbia kwa mwendokasi kati ya kilomita 360 kwa saa hadi 560 kwa saa, manufaa yanajidhihirisha kutokana na kushamiri kwa maeneo mengine ya uchumi.

Advertisement