Mchango wa wadau kwenye kilimo unavyojidhihirisha kijiji Welezo

Licha ya Serikali kutenga bajeti finyu kwa ajili ya kilimo, ushiriki wa sekta binafsi na wadau wengine ni muhimu katika kuongeza tija kwa wakulima nchini.

Hili linajidhihirisha katika Kijiji cha Welezo kilichopo Shinyanga vijijini ambako kutokana na matumizi ya mbegu bora na kuwapo kwa mashine ya kisasa ya kukoboa na kuuweka mchele katika madaraja tofauti, wakulima wananufaika zaidi tofauti na ilivyokuwa miaka michache iliyopita.

Kikundi cha Shyrice chenye wanachama saba katika kijiji hicho, wanajivunia kazi ya mikono yao iliyowapa mafanikio kutokana na juhudi walizozifanya. Kikundi hicho kinatumia mbegu bora ambayo imeongeza mavuno wanayopata kiasi cha kujenga ghala kubwa.

Wakati ghala hilo likijengwa kutokana na mtaji walioukuza kwenye kikundi chao cha Vicoba waliko na hisa, mafunzo ya matumizo ya mbegu bora na kilimo cha kisasa kutoka Shirika la Oxfam kupitia mradi wake wa Rudi (Rural Urban Development Innitiative) mwaka 2014, mavuno yao yaliongezeka maradufu.

Mmoja wa wakulima hao, Winfrida Mlale anasema analima mpunga tangu mwaka 1997 na kwa miaka mingi alikuwa anapata magunia mawili au matatu kwa ekari.

“Baada ya kuanza kutumia mbegu bora mwaka 2014 kwenye ekari zangu tatu nimeweza kuanza ujenzi wa nyumba na watoto wangu nawalipia ada bila tatizo. Nashukuru kwa mafunzo ya mbegu bora,” alisemaWinfrida.

Wakulima hao wanatumia mbegu ya mpunga aina ya TXD 3016; Saro 5 iliyofanyiwa utafiti na chuo cha uzalishaji mbegu Dakawa ambayo mavuno yake huwa kai ya magunia 28 hadi 40 endapo mkulima atazingatia hatua muhimu zinazoshauriwa.

Mmoja ya watafiti wa mbegu hiyo, Hezron Tusekelege anasema mbegu hiyo ilianza kutumka tangu mwaka 2002 baada utafiti wa muda mrefu na sasa hivi imeenea Tanzania nzima hata jirani kama Burundi, Rwanda, Kenya na Uganda.

Katibu wa Shyrice Group, Monica Jilabi anasema kutokana na mashine waliyonayo, wakulima wengi wameachana na uuzaji wa mpunga badala yake wanauza mchele wa madaraja tofauti.

Kwa sasa anasema mashine wanakoboa magunia 90 hadi 120 kwa siku kwa gharama kwa bei ya Sh50 kwa kilo moja.

“Lengo la hii mashine ni kuwasaidia wakulima kuongeza thamani na kupata faida. Kuuweka mchele kwenye madaraja tunatoza Sh5 kwa kila kilo moja,” anasema Monica.

Ufanisi

Akitoa taarifa ya uzalishaji, Monica anasema mwaka 2016 walikoboa kilo 1,024 za mpunga ambazo ziliongezeka mpaka kilo 52,010 (tani 52) mwaka 2017 na mwaka jana wakakoboa zaidi ya kilo 100,000.

Kwa mwaka huu, “mpaka sasa tumekoboa kilo 88,859 ambazo ni za mwaka jana. Kiwango cha uzalishaji kinaweza kushuka kutokana kuchelewa kwa mvua kwani mbegu nyingi zimeishia ardhini.”

Meneja mradi wa Rudi, Stephano Mpangala anasema juhdi zao zinalenga kuimarisha kipato cha wakulima. Kutokana na juhudi zilizoonyeshwa na Shyrice Group, Oxfam ilivutiwa kuwapa mashine ya kukobolea mpunga na kupanga madaraja ya mchele.

“Wanawake hawa hujipatia kipato cha uhakika hapa. kwa hiyo hii sio mashine ya kukoboa mpunga tu bali ni mkombozi wa wengi,” anasema.

Licha ya faid ahizo mbili, wakulima wananufaika zaidi na pumba zinazopatikana mshineni hapo kwani huzitumia kwa namna nyingine ambayo haikuwapo awali.

Wakati pumba laini hutumika kama chakula cha mifugo, Mpangala anasema zile ngumu wanazitumia kutengeneza matofali na wanakamilisha mpango wa kuwafundisha namna ya kutengeneza mkaa kutokana na makapi hayo.

Mtaalamu huyo wa Oxfam anaamini endapo watafanikiwa kuwajengea uwezo wakulima hao kutumia pumba hizo kupata nishati ya kupikia, matumizi ya kuni na mkaa yatapungua hivyo kusaidia kuhifadhi mazingira.

Kwa muda mrefu, serikali haijafanikiwa kutenga walau asilimia 10 ya bejteti nzima kwa ajili ya sekta ya kilimo kama inavyotaka baadhi ya mikataba ya kimataifa iliyosaini ukiwamo wa mwaka 2003 ulioridhiwa jijini Maputo na ule wa mwaka 2014 huko Malabo.

Nchi za Afrika zimekubaliana kutenga kiasi hicho kutokana na sekta ya kilimo kuajiri zaidi ya asilimia 80 ya nguvu iliyopo. Kwenye mipango yake, Serikali inatoa nafasi kubwa kwa sekta binafsi kushiriki kukuza kilimo.