Simu ya mkononi na fursa za kukuza uchumi wa Tanzania

Thursday April 4 2019

 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Unaitumiaje simu yako ya mkononi? Majibu yako yatadhihirisha ni kwa kiasi gani unashiriki kuchangia uchumi kuelekea kuipata Tanzania ya viwanda yenye uchumi wa kati.

Ripoti Shirikisho la Kampuni za Simu (GSMA) kuhusu mchango wa simu za mkononi ijulikanayo kama Digital Transformation in Tanzania inabainisha umuhimu wa sekta ya mawasiliano kufanikisha mpango wa kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kati.

Kwa sasa, sekta hiyo inachangia asilimia 5.2 kwenye pato la Taifa huku ikitoa zaidi ya ajira milioni 1.5 na endapo Serikali itaweka sera za kuvutia uwekezaji, ikaboresha miundombinu hususan vijijini na kuyafanyia kazi malalamiko ya kodi, itakua zaidi na kuongeza mchango wake kwa nchi.

Mbali na kufikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati, mchambuzi mwandamizi wa huduma za simu wa GSMA, Kenechi Okeleke anasema itafanikiwa kutimiza malengo endelevu ya Umoja wa Mataifa.

“Imebaki miaka sita mpaka mwaka 2025 kutimiza malengo ya kubadili uchumi wa Tanzania. Kuna changamoto ya miundombinu isiyojitosheleza na ujuzi lakini kwa kutumia teknolojia ya dijiti mpango huu unaweza kufanikiwa kwa urahisi kuliko kawaida,” alisema Okeleke.

Takriban Sh6 trilioni zimewekezwa kwenye sekta ya mawasiliano nchini hivyo kuwahudumia zaidi ya watu milioni 43.6 wanaomiliki laini zilizosajiliwa kupata huduma. Kati yao, kuna milioni 23.1 wanaotumia intaneti na milioni 23.3 wanaotumia huduma za fedha.

Advertisement

Akizungumza kwa niaba ya chama cha la watoa huduma za mawasiliano (Tamnoa), mkurugenzi wa uhusiano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano anasema ripoti hiyo inatoa picha halisi ya namna mitandao ya simu inavyoweza kushiriki katika maendeleo ya watu.

“Mpaka sasa mitandao ya simu inatoa huduma na taarifa mbalimbali katika sekta tofauti, zipo huduma za elimu na afya pamoja na huduma za fedha ambazo zimejumuisha watu wengi wa maeneo tofauti,” anasema Singano.

Mmliki wa duka la nguo la Judie Collections lililopo Sinza jijini hapa, Judith Boaz anasema kwa asilimia kubwa bidhaa zake anaziuzia mtandaoni.

“Teknolojia inatutaka tuwe hivyo. Wateja wengi wanapatikana katika mitandao ya kijamii hivyo nikileta mzigo napiga picha naweka instagram au Whatsapp status watu wakipenda nawapelekea,” anasema Judith.

Mkazi wa Tabata, Ahsante Christopher anasema simu imerahisisha maisha kwa kiasi kikubwa kwani yeye binafsi awaweza kufanya mambo mengi bila kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine.

“Simu zinapunguza gharama, zinaokoa muda na kutunza kumbukumbu sahihi kwa ajili ya usalama wa biashara,” anasema Ahsante.

Advertisement